2951; Njia yangu au njia kuu.

Rafiki yangu mpendwa,
Zipo njia nyingi sana za kuweza kumfikisha mtu kwenye mafanikio anayoyataka.

Uwepo wa njia hizo nyingi ulipaswa uwe ni uhuru mkubwa kwa wengi, kwa kuwaonyesha wanaweza kupata wanachotaka.

Lakini badala yake njia hizo nyingi zimegeuka kuwa usumbufu mkubwa kwa wengi.
Kwani watu hawakai kwenye njia moja kwa muda wa kutosha kuwaletea matokeo wanayotaka.

Wanakaa kwenye njia moja kwa muda mfupi na pale wanapoona matokeo yanachelewa, wanahamia kwenye njia nyingine.

Huo umekuwa ndiyo mzunguko wa wengi kwenye maisha na kusababisha wasifanikiwe, siyo kwa sababu hawazijui njia, ila kwa sababu wamepotezwa na njia nyingi zilizopo.

Kuna mambo mawili makubwa ya kufanya kwenye hili;

Moja ni kuchagua njia yako ya mafanikio.
Katika njia nyingi zilizopo, chagua njia yako itakayokuwa kuu na ya msimamo kufika kwenye mafanikio makubwa.
Kaa kwenye njia hiyo bila kuyumbishwa na chochote.
Endelea kujifanya kuwa bora zaidi kadiri unavyokwenda.

Mbili ni watu unaojihusisha nao.
Unapaswa kuwazuia wasiwe watu wa kuhangaika na kila njia, kwani wataweza kukusumbua na hayo mahangaiko yao.
Ili usionekane unawalazimisha, wape njia mbili; watumie njia yako au watumie njia kuu.

Unajaribu kuwazuia watu unaojihusisha nao wasihangaike na njia nyingi na kupoteza nguvu na muda wao.
Unawataka wafuate njia yako ili muweze kushirikiana na kwenda vizuri pamoja.
Au unawataka watumie njia kuu, ambayo inaeleweka na ni ya uhakika.
Njia kuu ni ile ambayo ina ushahidi wa wengi kuitumia na wakaweza kupata matokeo bora kwa uhakika.
Usiwape nafasi ya kuhangaika na kila njia huku wakiwa hawazalishi matokeo unayoyataka.

Hii inahusisha wafanyakazi wako, washirika wako, wateja na wengine wote wanaojihusisha na wewe.

Kama kuna mtu unashirikiana naye na kila mara amekuwa anakuja na njia mpya ya kufanya mambo wakati njia za nyuma bado hazijaleta matokeo mazuri, mweleze njia mbili za kushirikiana na wewe, njia yako au njia kuu.

Watu wanapenda sana njia za mkato.
Lakini kiuhalisia, njia za mkato huwa ni ndefu kuliko njia zilizo sahihi.
Hivyo mtu anayeiacha njia sahihi kwa sababu ameona anachelewa, huyo anakwenda kujichelewesha zaidi.

Ili usicheleweshwe na uzembe wa watu kutokuelewa hiyo dhana ya njia sahihi na matokeo, watake watu wanaoshirikiana na wewe wafuate njia yako au njia kuu.
Hilo linawasaidia kuondokana na usumbufu wa njia nyingi.
Na pia inawafanya watu wakae kwenye njia moja kwa muda mrefu mpaka kupata matokeo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe