2954; Biashara yenye mauzo ya faida.

Rafiki yangu mpendwa,
Takwimu za kibiashara kila mara huwa zinasikitisha sana.

Kati ya biashara mpya zinazoanzishwa, asilimia 80 huwa zinakufa ndani ya miaka miwili tangu kuanzishwa kwake.

Haijalishi ni biashara ya aina gani na inafanywa na nani, hatari ya biashara mpya huwa ni kubwa sana.

Hiyo ni kwa sababu kuna mambo mengi yanakuwa hayajulikani kuhusu biashara na soko lengwa.

Ili biashara iweze kukua na kustawi, inahitaji kuwa na mauzo yenye faida.

Kwa msingi huo, changamoto kubwa zinazopelekea biashara nyingi kufa ni mbili.

Ya kwanza ni kukosekana kwa mauzo. Kama tunavyojua kwamba mauzo ndiyo moyo wa biashara.
Bila mauzo hakuna fedha inayoingia kwenye biashara na bila mzunguko wa fedha hakuna biashara.

Ya pili ni kukosekana kwa faida. Mauzo yanaweza kuwepo, lakini yasiwe na faida.
Mauzo yasiyokuwa na faida ni hatari kubwa sana kwenye biashara.
Kwani fedha zitaingia kwenye biashara, ila zinakuwa chache kuliko zile zinazotoka.

Ukishahakikisha mauzo yapo kwenye biashara, tupia jicho lako kwenye fedha.
Unachopaswa kuhakikisha ni fedha inayoingia kwenye biashara inakuwa nyingi kuliko inayotoka kwenye biashara.

Kuna vitu vingi sana unavyopaswa kuhakikisha vimekaa sawa ili mauzo yapatikane na yawe ya faida.
Kuna vikubwa viwili vya kuzingatia.

Cha kwanza ni aina ya wateja.
Wateja hawafanani, kuna ambao manunuzi yao yanakuwa ya faida kubwa.
Halafu kuna ambao manunuzi yao ni ya faida ndogo.
Unapaswa kujenga wateja sahihi wa biashara na kwa namba sahihi ili biashara iweze kujiendesha vizuri.

Cha pili ni gharama za kuendesha biashara.
Fedha huwa ina tabia moja, ikiwepo huwa haikosi matumizi.
Hivyo kama huna nidhamu kali ya fedha, unaweza ukauza sana na bado biashara ikashindwa.
Kama utakosa nidhamu kali ya fedha, ukawa unatumia fedha kwa sababu ipo, haitakuchukua muda kabla biashara haijakushinda.

Jenga wateja bora na sahihi, wateja ambao wanaelewa thamani unayowapa na siyo wanaoangalia bei tu. Wateja wa bei wanaweza kufanya biashara iende, lakini siyo watakaoiwezesha ikue.
Lazima utoe thamani kubwa na kuwalenga wanaoielewa ili kufanya mauzo makubwa na yenye tija.

Halafu kuwa na bajeti unayoifuata kwa msimamo wa hali ya juu. Usitumie fedha kwa sababu ipo, bali tumia kwa sababu ulipanga.
Ukiwa na fedha, dharura huwa ni nyingi, hivyo jitenganishe na fedha za biashara.

Kama hufanyi mauzo ni shida.
Na kama hufanyi mauzo yenye faida ni shida pia.
Zingatia hayo mawili makubwa ili uweze kujenga biashara yenye mafanikio makubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe