2961; Uza maziwa, siyo ng’ombe.

Rafiki yangu mpendwa,
Ukiwa na ng’ombe, ambaye unamkamua maziwa, halafu akajitokeza mtu na kukuambia ng’ombe wako anatoa maziwa vizuri, niuzie maana nina uhitaji sana wa maziwa.
Kama ndiye ng’ombe pekee uliyenaye na ndiye tegemeo kwako, unajua vyema kwamba hutakubali kumuuza ng’ombe huyo, bali utamwambia umuuzie maziwa.

Kadhalika kama umeona kufuga ng’ombe ni changamoto kwako na hivyo unahamia kwenye mifugo wengine, hutamuuza ng’ombe ambaye unamkamua na kwenda kuanza upya.
Badala yake utatafuta mtu mzuri wa kuendelea kumtunza ng’ombe huyo ili aendelee kutoa maziwa na wewe kwenda kuanzisha huo ufugaji mwingine.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye biashara.
Huenda kwa malengo makubwa sana uliyonayo, biashara unayofanya sasa haiwezi kukufikisha.
Huenda huwezi kuikuza kwa viwango vya juu sana au kadiri unavyoikuza ndivyo changamoto zinavyokuwa nyingi.

Haifai uachane na biashara hiyo mara moja na kwenda kuanza biashara nyingine.
Badala yake unapaswa kuiweka biashara hiyo kwa namna ambayo inaweza kujiendesha hata kama wewe haupo, kisha kupeleka nguvu zako kwenye biashara nyingine.
Kwa biashara hiyo kuendelea kuwepo, inakupa kipato cha kukusaidia uweze kuendesha biashara yako mpya bila haraka ya kutaka kuitegemea.

Lakini pia unakuwa umepata funzo kubwa, kitendo cha kuweza kuijenga biashara mpaka kuweza kujiendesha yenyewe bila kukutegemea ni funzo ambalo utaweza kulitumia kwa kila biashara unayokuwa unafanya.

Biashara ambazo wengi wetu tunazifanya sasa haziwezi kutufikisha kwenye ubilionea, hata iweje. Na hilo siyo tatizo, ubilionea ni safari, ambayo siyo ya basi moja. Hakuna bilionea mwenye biashara moja pekee.
Hivyo unachopaswa kufanya ni kutumia biashara yako ya sasa kama darasa. Itumie kujifunza kujenga mfumo wa biashara kwa vitendo, kujenga timu imara na kukuza sana mauzo.
Itumie kujifunza kujenga meneja mzuri, zaidi ya mmoja. Kisha mwache meneja huyo aiendeshe biashara hiyo na wewe uende kuanzisha biashara nyingine, ambayo ina nafasi kubwa zaidi ya kukufikisha kwenye ubilionea.

Kama biashara uliyonayo sasa, ambayo umeshaifanya kwa miaka mingi, bado inakupa changamoto nyingi, kuiacha na kwenda kuanzisha nyingine hakuna muujiza wowote utakaojitokeza kwako na ghafla ukawa bora zaidi kwenye biashara hiyo mpya.
Changamoto kuu za biashara ni zile zile, nenda kila mahali na utakutana nazo.
Watu na mauzo ndiyo changamoto zinazoandama biashara tangu enzi na enzi. Nenda kwenye biashara yoyote ile na kama hujaweza kung’amua kitendawili cha kupata watu bora na kufanya mauzo makubwa, utajikuta unarudi kwenye changamoto zile zile.

Kuweza kujenga mfumo bora wa biashara, ambao unatatua changamoto ya watu na mauzo ni hitaji muhimu sana kwenye mafanikio ya kibiashara.

Tunaiita huduma yetu Bilionea Mafunzoni kwa sababu kubwa na yenye mashiko kwamba unahitaji kujifunza vitu vingi sana kwa vitendo kabla hujaufikia ubilionea.
Sehemu pekee ya kujifunza na ambayo inakupa mrejesho sahihi ni kwenye uwanja wa mbele wa mapambano.

Kila mpango wa biashara (business plan) huwa una faida na ukuaji. Huwezi kukuta mtu ameandaa mpango wa biashara na kusema itakuwa imekufa ndani ya miaka miwili.
Lakini njoo kwenye uhalisia mitaani, asilimia zaidi ya 80 ya biashara mpya zinazoanzishwa huwa zinakufa ndani ya miaka miwili.

Lakini tafiti hizo hizo zinaonyesha kwamba pale biashara mpya inapokuwa inaanzishwa na mtu ambaye alishaendesha biashara nyingine kwa mafanikio, hatari ya kufa inakuwa ni ndogo zaidi.
Unaona hapo, uzoefu una msaada mkubwa.

Tumia biashara yako ya sasa kujifunza kwa vitendo na kujenga uzoefu ambao utaweza kuutumia kwenye biashara nyingine utakazokuja kuanzisha huko mbele, au kuzinunua, kuzijenga na kuziuza.
Kama biashara uliyonayo sasa itakushinda kuijenga vizuri, jua popote utakapokwenda, yatakwenda kujirudia hayo hayo.

Wito wangu ni tupo nyuma ya muda, kwa kulinganisha na lengo kubwa tulilonalo.
Hivyo tukae kwenye viwango, fokasi na kasi kubwa.
Tujiwekee viwango vya juu vya kuendesha biashara zetu, tuwe na fokasi kubwa ili tusisumbuliwe na tuwe na kasi kubwa kwenye kuchukua hatua.

Kuna maana kubwa kwa nini malengo yetu makuu kwenye mwaka huu wa mafanikio ni mfumo, timu na mauzo.
Hapo ndipo penye ufunguo utakaotufikisha kwenye ubilionea kwa uhakika.
Kuweza kujenga biashara inayojiendesha yenyewe bila ya kututegemea, huku ikiweza kufanya mauzo makubwa.

Na pale unapokwenda kuanzisha biashara mpya, ambayo ndiyo biashara ya ndoto zako, utakuwa pazuri sana kama tayari umeshajenga biashara nyingine inayokuingizia kipato cha uhakika, hata kama ni kidogo.

Huyo ng’ombe ambaye anatoa maziwa, usimuuze na kwenda kuanza kufuga mbuzi ambao ndiyo umeona watakulipa sana.
Badala yake weka mtu amlishe vizuri na kuendelea kukamua maziwa, halafu wewe nenda kapambane na hao mbuzi wako.
Fikisha mbuzi nao kwenye mahali wanaweza kufugwa na mwingine bila uwepo wako, mwachie au uza na nenda kwenye kitu kingine.

Utapata faida kubwa kwa kuuza ng’ombe anayetoa maziwa, lakini kama hutakuwa na ng’ombe mwingine anayekupa maziwa, utatumia faida yote uliyopata kununua tena maziwa kwa uliyemuuzia ng’ombe, je hapo unakuwa umefanya nini?

Tunajenga ubilionea kupitia kujenga biashara, popote ulipo sasa ni mahali pazuri pa kuanzia.
Lakini usijiachie, uko nyuma sana ya muda, pambana usiku na mchana upaweke hapo sawa ili uweze kuchomoka na kwenda pengine pakubwa zaidi.
Ila kama hapo padogo patakushinda, huna tumaini lolote kwa pakubwa zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe