2963; Imani na matamanio makubwa.

Rafiki yangu mpendwa,
Ili uweze kufikia mafanikio makubwa unayoyataka kwenye maisha yako, unapaswa kuchukua hatua kubwa pia.
Hatua ambazo siyo za kawaida na wengi hawawezi kuzichukua.

Unapaswa kuchukua hatua kubwa kwa namna ambayo wengine wanakushangaa, ya kwamba unawezaje kuchukua hatua za aina hiyo.

Unapaswa kufanya kazi kwa akili sana, nguvu nyingi na kwa muda mrefu.
Unapaswa kujisukuma kupitiliza, ufanye kwa ukubwa na ubora ambao wengine wanabaki wakishangaa.

Inabidi uanze mapema kuliko wengine na uchelewe kumaliza kuliko wengine.
Muda na umakini wako wote unapaswa kuelekezwa kwenye yale unayofanya.

Unapaswa kupuuza kila aina ya usumbufu unaokujia, mwingine ukiwa unatamanisha sana ujihusishe nao.

Kwa kifupi, inabidi usiwe binadamu wa kawaida.
Watu wanatakiwa wakushangae unawezaje yote hayo, maana wao wakijaribu kwa muda mfupi tu wanachemka.

Baadhi ya watu inabidi wawe na wasiwasi na wewe kwamba kuna kitu unatumia au kuna namna hauko sawa.

Wakati mwingine wewe mwenyewe unaweza usijue kwa nini unawesa yote hayo.

Leo nataka nikuambie wazi ni wapi msukumo wa wewe kufanya zaidi ili kupata makubwa unatoka.
Ni kwenye imani na matamanio makubwa.
Hivyo ni vitu viwili vinavyokupa wewe nguvu isiyoelezeka, inayokuwesesha kufanya makubwa sana.

Imani ni pale unapoamini unaweza kupata unachotaka bila ya kuzuiwa na chochote kile.
Hata unapokabiliana na changamoto na vikwazo, unajua ni sehemu tu ya safari.
Hakuna namna unakatishwa tamaa na chochote kile.
Badala yake unakuwa imara bila kuyumbishwa, ukijua ni swala la muda tu wewe kupata unachotaka.
Unaamini sana kwako mwenyewe, kwenye mchakato unaofuata na kwenye nguvu kubwa inayoendesha huu ulimwengu, ambayo inaweza kukupa chochote unachotaka.
Kama imani hii haipo au siyo imara, hakuna hatua kubwa unazoweza kupiga.

Matamanio makubwa ni kile hasa unachokitaka. Hatua unayotaka kupiga na matokeo unayotaka kuzalisha.
Matamanio makubwa yanakupa sana msukumo wa ndani, ambao unakuwesesha kuvuka kila kikwazo unachokutana nacho.
Kwa matamanio makubwa unayokuwa nayo, kila hapana unayokutana nayo unajiambia ni ndiyo ya baadaye. Haikukatishi tamaa, bali inakupa msukumo mkubwa zaidi.
Matamanio makubwa ni moto unaojichochea ndani yako, ambao haukuruhusu utulie wala kuridhika.
Unataka ufanye zaidi ya kile ambacho tayari unafanya.

Unakumbuka ile siku ambayo ulikuwa na safari muhimu ambayo hakuna namna ulitaka kuikosa.
Hivyo ukahitajika kuamka asubuhi na mapema kuliko ulivyozoea?
Siku hiyo uliweza kuamka mapema sana hata kabla ya kengele ya kukukumbusha kuamka haijalia.
Umewahi kujiuliza kwa nini hilo linatokea?
Kwa sababu akili zetu zina uwezo mkubwa sana, pale tunapokitaka hasa kitu, inauelekeza mwili kuhakikisha kinafanyika kwa namna tunavyotaka.
Hivyo ndivyo akili hizo hizo zinavyoweza kuusukuma mwili ufanye zaidi ya mazoea.

Wengi hudhani kuwa na ndoto na malengo makubwa inatosha kuwasukuma kufanikiwa.
Lakini hiyo siyo kweli, msukumo mkubwa wa mafanikio unatokana na imani na matamanio makubwa sana.
Lazima uwe na imani kali na isiyoyumbishwa huku ukiwa na matamanio makubwa yasiyoridhishwa na matokeo ya kawaida.
Weka hayo mawili na utawesa kuhamisha milima kama ilivyoandikwa kwenye vitabu vya dini.

Jenga imani kuu na matamanio makubwa.
Kila wakati chochea hayo mawili ili yasipoe au ukajenga wasiwasi ndani yako.
Na utaweza kuacha alama kubwa sana hapa duniani.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe