2964; Onyesha kazi yako.

Rafiki yangu mpendwa,
Wakati upo shuleni, ulifundishwa namna sahihi ya kufanya hisabati.
Kila swali la hisabati lilikuwa na sehemu tatu.
Sehemu hizo ni swali, kazi, jibu.
Katika kujibu maswali hayo ya hisabati hukutakiwa tu kutoa jibu sahihi, bali ulitakiwa kuonyesha njia uliyotumia kupata jibu hilo.
Mara nyingi, hata kama ulikosa jibu, bado ulipata sehemu ya alama kwa kazi uliyoonyesha.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye maisha yetu ya kila siku.
Kuna changamoto ambayo ndiyo swali, kuna kuchukua hatua ambako ndiyo kazi ya kufanya kwenye changamoto hiyo na kuna matokeo ambayo ndiyo jibu.
Kama ilivyo kwenye hisabati, hata kwenye maisha, unaweza kupata sehemu ya alama kwa kuonyesha kazi, hata kama jibu siyo sahihi.

Kuonyesha kazi ndiyo kitu tunachoita kukaa kwenye mchakato.
Watu wengi wamekuwa wanahangaika na njia za mkato ili kupata haraka matokeo wanayotaka.
Lakini ushuhuda upo wazi, mwisho wao umekuwa siyo mzuri.
Hata pale walipoanza kwa kupata matokeo mazuri, waliishia kwenye anguko baya sana.

Lakini wale wanaokaa kwenye mchakato sahihi, hata kama matokeo wanayoanza nayo siyo sahihi, kitendo tu cha kukaa kwenye mchakato kinawapa manufaa makubwa sana.

Twende kwa mfano ili tuelewane vizuri.
Kuna watu huwa wanaanzisha biashara, wanatumia njia zisizo halali na kupata matokeo makubwa mwanzoni.
Wanaweza kusifiwa kwa matokeo hayo, lakini huwa haichukui muda wanapata anguko kubwa na kuharibu sifa yao yote.
Lakini kuna ambao wanaanzisha biashara, wanafuata mchakato sahihi lakini kutokana na mambo yaliyo nje ya uwezo wao, biashara zinashindwa.
Kupitia kuonyesha kwao kazi, kwa kukaa kwenye mchakato sahihi, watu hao huendelea kuaminika na kuungwa mkono, kitu kinachokuja kuwapa matokeo makubwa na mazuri sana mbeleni.

Hivyo basi rafiki yangu, wajibu wako mkubwa ni kuonyesha kazi yako, kwa kukaa kwenye mchakato sahihi mara zote.
Haijalishi sana ni matokeo gani unayopata sasa, kukaa kwenye mchakato sahihi ni ushindi wa kwanza na muhimu.
Kwa kuendelea na hilo, unakuwa na uhakika wa ushindi mkubwa sana kwenye matokeo baadaye.

Kukaa kwako kwenye mchakato sahihi ni kinga nzuri kwako pale mambo yanapokwenda tofauti na matarajio yako, kitu ambacho huwa kinatokea mara nyingi sana.

Watu watakuja kwako na njia za mkato, wakikuonyesha majibu ili uyanakili tu.
Lakini kama hutaweza kuonyesha kazi iliyokufikisha kwenye majibu hayo, umejenga nyumba juu ya mchanga bila ya msingi imara.
Kuanguka ni swala la muda tu.

Kukaa kwenye mchakato kamili na sahihi muda wote ni hitaji muhimu sana kwenye safari yako ya mafanikio.
Epuka sana njia za mkato, zitaishia kukuacha na mikato mingi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe