2966; Kwa nini usiwe wewe?

Rafiki yangu mpendwa,
Kwa mambo yote makubwa unayotaka kufanya au kufikia, tayari kuna wengine wanafanya au wameshafikia.
Swali kubwa unalopaswa kujiuliza ili likusukume ni kwa nini na wewe pia usiwe?

Kuna vipindi ambavyo watu huwa wanalalamikia sana biashara. Uchumi unakuwa mgumu na wateja wanakosa nguvu ya kununua.
Lakini hata mambo yawe magumu kiasi gani, kuna wateja wanaoendelea kununua, tena kwa wingi.
Swali muhimu sana unalopaswa kujiuliza na kujijibu ni kwa nini wasinunue kwako?

Hii dunia ina mabilionea wengi sana.
Afrika pia inao mabilionea wengi.
Tanzania tuna bilionea mmoja anayejulikana kwa viwango vilivyo wazi.
Kama kumeweza kuwepo hao mabilionea, hasa kwa mazingira ambayo na sisi pia tupo, swali ni kwa nini na wewe usiwe mmoja kati ya mabilionea hao?

Katika siku yoyote ile, kuna watu wananunua bidhaa au huduma unayouza, watu ambao unao uwezo wa kuwafikia na kuwahudumia.
Swali ni kwa nini watu hao wasipate mahitaji yao kwako?

Nikujibu kwa nini hutakuwa wewe.
Sababu kubwa kabisa ni hutaki.
Ndiyo, hutaki tu.
Najua unaweza kuwa unabisha, kwa kutoa sababu na visingizio mbalimbali.
Lakini mwisho wa siku ukweli unabaki kwamba huwi wewe au hupati kwa sababu hujataka hasa kutoka kwenye moyo wangu.

Sitaki nitumie nguvu na muda mwingi kukushawishi kwenye hili.
Nataka upitie mifano yako mwenyewe, angalia vitu vyote ambavyo umewahi kuvitaka sana kwenye maisha yako, lakini ukakutana na magumu na changamoto katika kufanyia kazi.
Kwa kuwa ulikuwa unataka sana, hukukatishwa tamaa, badala yake ulipambana kweli na mwishowe ukapata ulichotaka.

Kwa upande wa pili, kuna vitu unakuwa umetamani kuvifanya au kuvipata, lakini hujajitoa hasa.
Kwa vitu vya aina hiyo umekuwa unakutana na magumu na changamoto mbalimbali, ambazo umekuwa unazikubali kama kikwazo.

Somo kubwa tunalopata hapa ni kupata au kukosa tunachotaka inaanzia ndani yetu wenyewe.
Mambo ya nje yana mchango mdogo sana.
Maamuzi hasa na matokeo yanaanzia ndani.
Kama mtu anakitaka kweli kitu na hayupo tayari kutokukipata, lazima atakipata. Inaweza kuchukua muda mrefu, lakini mwisho anakipata.

Magumu, vikwazo na changamoto huwa ni kikwazo halisi kwa wale ambao hawajajitoa hasa kupata wanachotaka.
Lakini kwa wale waliojitoa hasa, ambao wameamua watapata wanachotaka hata iweje, hakuna kinachowazuia.
Chochote kinachopita kwenye njia yao, kinakuwa sababu ya wao kufika kule wanakotaka kufika.

Je wewe umejitoa kiasi gani kuhakikisha unapata kweli kile ulichodhamiria kweli kukipata?
Je umejihakikishiaje kwamba hata kama wateja wanaonunua ni wachache, basi wananunua kwako?

Unaweza kuwa na kupata chochote unachotaka kama utaamua kweli kukipata na kujitoa kwa kila namna kuhakikisha kweli kwamba unakipata.
Usikubali kuyumbishwa, jua kile hasa unachotaka na inyeshe mvua au liwake jua, lazima upate unachotaka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe