2967; Haifai kwangu.

Rafiki yangu mpendwa,
Tofauti kubwa ya watu waliofanikiwa na walioshindwa ni hii; waliofanikiwa wanaona suluhisho kwenye kila tatizo, wakati walioshindwa waliona tatizo kwenye kila suluhisho.

Waonyeshe waliofakiwa njia fulani yenye matokeo mazuri kwa wengine na wataona jinsi gani njia hiyo inaweza kuwafaa na wao pia.
Lakini mwonyeshe aliyeshindwa njia fulani yenye matokeo mazuri kwa wengine na watakuonyesha kwamba haiwezi kufanya.

Watakuambia wazi; “Hiyo njia inaweza kufanya kazi kwa wengine na ikawanufaisha, lakini kwa upande wangu haiwezi kufanya kazi kwa sababu…. “
Hapo watakuorodheshea sababu nyingi za kwa nini njia hiyo haiwezi kufanya kazi kwao.
Na watakuwa wanajivunia kabisa hilo wanalofanya, wakiona ni jambo la kishujaa.

Hiyo haina tofauti na mtu mwenye kiu, ambaye anaelezwa kuna maji ambayo wengine wanakunywa, kisha yeye anasema hayo maji yanaweza kuwafaa wengine ila siyo yeye.
Cha haraka utakachopata kwenye hayo majibu ni huyu kiu haijamkamata kweli kweli.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa wale wanaochagua kanuni za mafanikio, wanakuwa hawana kweli kiu ya mafanikio.
Kila unapoona mtu anasema kinachofanya kazi kwa wengine kwake hakitaweza kufanya kazi, jua hapo umekutana na mtu asiye na kiu ya mafanikio.
Anakuwa na uvivu, uzembe au ujinga, lakini hataki kukiri hayo.

Kwa mwenye kiu hasa ya mafanikio, atafanyia kazi kila njia hata kama hana uhakika nayo, kwa sababu anajua ni bora apotee kuliko kubaki pale alipo ambapo siyo anapopataka.
Anajua njia yoyote itakuwa na msaada kuliko kutokutumia njia kabisa.

Kinachofanya wengi wasingizie njia fulani haziwezi kufanya kazi kwao ni kutokutaka mabadiliko.
Mafanikio yanataka mtu awe tayari kuleta mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yake.
Mabadiliko yoyote yale huwa yanaumiza, wakati matokeo yake siyo ya uhakika.
Wenye mioyo myepesi huwa hawawezi kuyakabili mabadiliko hayo, hivyo huona njia pekee ni kuyakataa.

Kila unapojiambia njia fulani inaweza kufanya kazi kwa wengine ila kwako haiwezi kufanya kazi, jiulize ni uvivu, uzembe au ujinga unaokusumbua?
Kwa sababu kama huna njia unayotumia, njia yoyote ni nzuri kwako kuanzia.

Ni kweli hupaswi kufuata kila njia kama msaafu, utakwenda ukiiboresha kulingana na hali yako.
Lakini njia ni njia, inafanya kazi kwa kila mtu kama inafanyiwa kazi kwa uhakika.

Kwa kila unachojifunza kwa wengine, acha mara moja tabia ya kujiambia hakifai kwako. Badala yake jiulize kinafaaje kwako?

Kwa sababu njia ya kuelekea kwenye mafanikio ni kama ilivyo njia ya kwenda kwenye kisima cha maji, iko wazi kwa kila mtu, ila siyo wote watakaoitumia.

Ni rahisi kuona kila kitu ni kigumu na hakiwezekani kwetu.
Ni rahisi kuchukulia hali zetu ni za kipekee sana ambazo haziwezi kukabiliwa na njia zilizopo.
Lakini hayo yote ni kujitesa na kujichosha, ni kuyafanya mambo yawe magumu kuliko yalivyo kwa uhalisia wake.

Kama kweli unataka kufanikiwa, usitafute tatizo kwenye kila suluhisho au kila njia.
Badala yake ona njia kwenye kila tatizo.
Na kama huoni njia kabisa, angalia ni njia gani ambayo wengine wanatumia na kuwa tayari kuitumia kwa kuboresha zaidi kulingana na hali yako.

Misingi ya mafanikio ni ile ile kwa kila mtu na kila sekta. Kuna hatua za tofauti zinazopaswa kuchukuliwa kulingana na hali husika, lakini misingi ni ile ile, haibadiliki.
Kuikataa misingi hiyo ni kuonyesha jinsi gani huna kiu kubwa ya mafanikio.
Na ni bora ukiri hilo ili ijulikane moja, kuliko kujificha kwenye kichaka cha haiwezi kufanya kazi kwangu.

Sema njia fulani haiwezi kufanya kazi kwako kama tayari unayo njia nyingine inayokupa matokeo bora kabisa.
Lakini kama huna njia ya kukutoa pale ulipo sasa, ambapo hunaridhika napo, kamata njia yoyote inayokuja mbele yako na ifanye ikufanyie kazi.

Kila kitu kinafanya kazi kama kitafanyiwa kazi.
Acha maneno na visingizio na ufanye.
Mambo yote mazuri yako upande wa pili wa kufanya na siyo kwenye maneno au visingizio.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe