2968; Sizitaki mbichi hizi.

Rafiki yangu mpendwa,
Bila shaka unakumbuka moja ya hadithi ambazo tulijifunza shuleni.
Ambapo sungura aliziona ndizi, akaamua azirukie ili aweze kula.
Akaruka na kuruka sana, lakini hakuweza kuzifikia.
Akakazana kuruka tena na tena, lakini bado hakuzifikia ndizi hizo.
Mwisho akajiambia hata hivyo ndizi zenyewe ni mbichi, sizitaki.

Kwa kusoma hadithi hiyo fupi unaweza kumcheka sungura kwa jinsi anavyojidanganya baada ya kukosa kitu alichotaka.
Lakini je umewahi kukaa chini na kufikiria jinsi ambavyo wewe mwenyewe umekuwa unajidanganya pale unapokosa ulichotaka au hata tu kukutana na changamoto kwenye mchakato wa kukipata?

Unapanga kabisa unataka kupata matokeo ya aina fulani, kisha unajua hatua unazopaswa kuchukua ili kupata matokeo hayo.
Unaanza kuchukua hatua hizo na unakutana na magumu na changamoto zinazokuwa kikwazo kwako kupata unachotaka.

Katika hali ya kawaida unafanya nini pale unapokutana na magumu na changamoto hizo?
Unakata tamaa na kuona haiwezekani.
Na hapo ndipo unakuwa mjanja kuliko hata sungura.
Unaanza kujiambia ni kitu kisichowezekana.
Unajiambia hata hivyo siyo muhimu sana.
Unaona kuna mengine muhimu zaidi na kwenda kuyafanya.

Huo ndiyo mzunguko ambao wengi wamekuwa nao maisha yao yote.
Na kwa sababu hakuna kitu ambacho hakina changamoto, wengi wamekwama kufanikiwa kwa sababu ya kuhangaika na mambo mapya kila wakati.

Sasa rafiki yangu, ipo njia ya kukuzuia usijidanganye kama sungura.
Njia hiyo ni kukaa chini na kuandika kabla hujakimbilia kufanya.
Unaandika mpango wako mzima wa kile unachokwenda kufanya.
Na pia unaandika sababu za kwa nini unafikiri ni muhimu kufanya hayo uliyopanga kufanya.
Andika matokeo unayotegemea kupata katika kukifanya.
Na pia andika changamoto na magumu unayoweza kukutana nayo katika kufanya.

Kwa njia hii ya kuandika ni rahisi kurejea kwenye sababu za wewe kufanya kitu na matarajio uliyokuwa nayo.
Kwa kukutana na ugumu, hakuondoi sababu za wewe kuamua kufanya wala matarajio uliyokuwa nayo.
Maandiko yanakuzuia usijidanganye na kukimbilia kuacha ulichopanga kwa sababu tu umekutana na magumu na changamoto.

Hii inakuwezesha ukae kwenye kitu kimoja kwa muda mrefu kabla hujakimbilia kwenye vitu vingine pale unapokutana na magumu na changamoto.

Hakuna chochote utakachofanya ambacho hutakutana na magumu na changamoto.
Sisi binadamu ni rahisi kusahau sababu ya kufanya kitu pale tunapokutana na magumu na changamoto.
Kwa kuwa na tabia ya kuandika sababu za kufanya kitu na matokeo unayotarajia, unajizuia usijidanganye na kuacha pale unapokutana na magumu na changamoto.

Ni heri ujiambie wazi umechoka kuzirukia hizo ndizi kwa sababu zipo mbali kuliko ulivyotegemea.
Kuliko kujiambia kwamba ni mbichi, kwani mwanzo wakati unaamua uzirukie hukuziona ni mbichi?
Kuna sababu za kila tunachoamua kufanya, tusipoziweka bayana sababu hizo, ni rahisi kuzisahau na kujifanganya ambapo hakuna manufaa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe