2972; Hatari umeibeba wewe.

Rafiki yangu mpendwa,
Kuendesha biashara kuna changamoto nyingi sana.
Kila wakati kuna kitu unakuwa unapambana nacho.

Kama hiyo haitoshi, kuna hatari kubwa unayokuwa umeibeba kila siku kibiashara.
Changamoto unazokabiliana nazo kibiashara zinakuwa na hatari ya kuweza kupelekea biashara kufa.

Tatizo zaidi ni kwamba hatari yote ya biashara yako umeibeba wewe.
Chochote kinachotokea kwenye biashara, wewe ndiye utakayeumia kuliko wengine wote.

Cha kushangaza, kuna watu ambao wanataka wakupangie uendesheje biashara yako, wakati wao hawabebi hatari yoyote uliyonayo.

Watu hao watakuwa na uthubutu wa kukupinga kwenye baadhi ya hatua muhimu unazochukua kwa ukuaji wa biashara yako.

Pale unapojisukuma kwa kuweka juhudi zaidi ili kutatua changamoto za biashara watakuona kama unajitesa na kukutaka uende kawaida.

Watu hao hujiona kama wana wajibu wa kukueleza nini unapaswa kufanya na nini hupaswi.
Lakini inapokuja kwenye hatari, hawataki kabisa kuhusika nayo.

Tatizo kubwa ni kwamba kwenye jamii zetu, kila mtu ana maoni kwenye kila kitu.
Hata kama mtu haelewi kitu kwa undani, bado anakuwa na maoni yake.
Na zaidi, watu huwa wapo tayari kutoa ushauri hata kama hawajaombwa.
Wanaona tu kitu kwa nje na kukimbilia kutoa ushauri wao.

Wewe unapaswa kuwa makini sana na watu gani unaowasikiliza na kuchukua ushauri wao.
Kwanza jua kuna kitu unakiona wewe kwenye fikra zako ambacho wengine hawaoni.
Watu kukimbilia kukupa maoni na kukushauri kwa mambo waliyoona kwa nje na hawajajua kwa ndani, ni jambo unalopaswa kulipuuza kabisa.

Unapuuza kwa sababu unajua maoni na ushauri ambao mtu anatoa haujakamilika.
Lakini pia hakuna hatari yoyote watoa maoni na ushauri wanakuwa wanaingia.

Kuongea ni rahisi sana, kila mtu anapenda kufanya hivyo.
Hatari ipo kwenye kuchukua hatua, ambapo ni wachache sana wanaofanya hivyo.

Jikumbushe hulazimiki kuchukua maoni na ushauri wa kila anayejitolea kukupa.
Hatari yote umeibeba wewe, picha ya wapi unaenda unayo wewe.
Jiamini na fanya maamuzi sahihi ambayo yanapunguza hatari na kukupeleka kule unakoelekea.

Watu wengi huziona biashara ni nzuri na rahisi kwa kuangalia kwa nje.
Wanakuwa hawajui moto unaokuwa unaendelea ndani, ambapo kila wakati kazi kubwa ni ya kuzima moto.
Usisahau hili kwenye kila maamuzi unayofanya ya kibiashara.

Unaweza kusikiliza maoni na ushauri kadiri unavyotaka.
Lakini inapokuja kwenye kutekeleza, jikumbushe hatari umeibeba wewe peke yako.
Hivyo fanya maamuzi yenye tija, hata kama kwa wengine yanaweza kuonekana ni ya kipuuzi.

Usibabaishwe na wale wanaokulazimisha ufanye vitu vya aina fulani kwa sababu ndivyo wanavyoona wao.
Jua hatari ilipo na fanya maamuzi sahihi kulingana na hatari hiyo.

Watu wengi wanapenda sana kuongea, lakini hakuna anayependa kuwajibishwa kwa yale aliyoongea.
Hilo tu likupe funzo kubwa kuhusu uzito unaopaswa kuweka kwenye yale wengine wanakuambia.
Kama mtu hayupo tayari kugharamia kile anachoongea, inakudhihirishia wazi uzito wa hicho anachokuambia.
Kama kingekuwa muhimu na cha uhakika, angekuwa tayari kubeba hatari yake.

Tusidanganyike, mambo siyo rahisi na wala hayatakuja kuwa rahisi.
Kama maoni na ushauri unaotolewa na kila mtu ungekuwa unafanya kazi, changamoto nyingi za kibiashara zisingekuwepo.
Lakini kuendelea kuwepo kwa changamoto hizo na hatari za biashara kufa, ni kiashiria jinsi maoni na ushauri mwingi unaotolewa bure na kirahisi kabisa havina thamani yoyote.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe