2973; Wape sababu ya kukuheshimu.

Rafiki yangu mpendwa,
Tunajifunza mambo mengi kwenye biashara na mauzo.
Na mengi sana tunayojifunza yameegemea kwenye kuwajali sana wateja na kuweka maslahi yao mbele.
Hayo ni mambo yenye nguvu na ushawishi mkubwa kwa wateja.

Lakini pia kuna wateja wanachukulia kujali kwetu kama sehemu ya kutaka kutunyanyasa.
Kwa kuwa tumechagua kuwajali sana na kuweka maslahi yao mbele, wanaona tuna uhitaji mkubwa na bila wao hatuwezi kuendesha biashara zetu.

Na hapo ndipo wanaanza manyanyaso yao.
Wanaanza kutupangia ni kwa namna gani tuendeshe biashara zetu, ili kuendana na matakwa yao.
Wanatutaka tuwauzie kwa bei ndogo hata kama ina hasara kwetu.
Wanataka tuwakopeshe, kwa ahadi kwamba watalipa baadaye, lakini tukishafanya hivyo wanakuwa wasumbufu sana kwetu.

Hayo yanatuchanganya na kutuweka njia panda, tunajikuta hatujui nini tufanye katika hali hizo.

Hapa tunakwenda kujifunza mambo muhimu ya kufanya na kuzingatia ili wateja watupe heshima kubwa kwa namna tunavyowajali.

Kwanza kabisa tunahakikisha kuna vitu tunawapa wateja wetu ambavyo hawawezi kuvipata kwa wafanyabiashara wengine wowote.
Siyo lazima iwe bei nafuu, japo kama unaweza hilo litakuwa zuri.
Inaweza kuwa huduma bora kabisa ya kuwajali na kuweka maslahi yao mbele.
Inaweza kuwa uhakika wa kupata bidhaa au huduma wakati wote anapokuwa na uhitaji.
Inaweza kuwa uharaka wa kupata kile wanachonunua.
Inaweza kuwa huduma za ziada wanazopata baada ya manunuzi.
Au inaweza kuwa jinsi unatatua changamoto wanazokutana nazo kwenye kile unachowauzia.

Kwa vyovyote vile, hakikisha wateja wanaponunua kwako kuna thamani kubwa wanayoipata ambayo hawawezi kuipata kwa wafanyabiashara wengine wowote.
Ni wewe uchague tu thamani gani utakayowapa kisha jenga msimamo hapo.

Halafu basi, mteja atakapoleta kiburi na kutaka kukupangia namna gani uendeshe biashara yako, mjibu tu kwa unyenyekevu kwamba kwa upande wako hilo limeshindikana.
Mweleze wazi ungependa sana kumhudumia na kumpa thamani, ila kama ameshindwa kwenda na utaratibu uliopo, itashindikana kumhudumia vizuri.

Hapo utamwacha aende huko kwingine ambapo anaona ataweza kuwapangia jinsi ya kuendesha biashara.
Na huko ataikosa ile thamani aliyokuwa anaipata kwako.
Hilo litamfanya arudi kwako, na atakaporudi atakuwa tayari kufuata utaratibu uliopo.
Akirudi mpokee vizuri, mshukuru kwa kurudi na mpe thamani kubwa kama ambavyo umekuwa unatoa.
Usimwonyeshe kisirani kwamba wewe umeshinda na yeye amehangaika bure.
Onyesha kumjali zaidi na mhudumie vizuri.
Yote hayo yatamfanya mteja afuate utararibu ulioweka ili asikose thamani unayotoa.
Itawafanya wakuheshimu na kufuata maelekezo unayowapa.

Utaweza kufanya hili kama tu una thamani ya tofauti unayowapa wateja na una wateja wengi ambao umewatengeneza na unaendelea kuwatengeneza.
Kama hakuna cha tofauti ambacho wateja wanapata kwako, ambacho hawawezi kupata kwingine, na kama huna wateja wengi uliowatengeneza, utajikuta ukiwa mateka kwa wateja wachache ulionao.
Watakupelekesha wanavyotaka wao na wataiua biashara yako kwa ubinafsi wao.

Hakikisha wateja hawachanganyi kujali kwako kwa kuona ni udhaifu.
Chora kabisa mstari ambao mteja akiuvuka anakuwa amejikosesha mwenyewe kile unachouza.
Kisha weka juhudi kubwa sana kuhakikisha unatoa thamani kubwa na unatengeneza wateja wengi.
Hakikisha kwa upande wako una machaguo mengi kuliko mteja na hilo ndiyo litakalokupa nguvu.

Kuna wateja watajichanganya, kwa kudhani wataweza kukupangia uendesheje biashara yako. Na hapo ndipo watashangaa namna utakavyokuwa tayari kuwaacha waende na wakifika huko nje, hawatakuwa na budi bali kurudi.

Nisisitize sana haya mawili; TOA THAMANI KUBWA WASIYOWEZA KUIPATA KWINGINE na KUWA NA WATEJA WENGI SANA UNAOWATENGENEZA NA KUWAHUDUMIA.
Hayo mawili ndiyo yatakayokupa nguvu kubwa ya kusimamia yale uliyopanga kwenye biashara yako na hata kuiendesha biashara yako kwa furaha kubwa.

Kuwa tayari kumpoteza mteja yeyote na biashara isitetereke sana.
Hata kwa wateja ambao tayari wanaelewa thamani yako na kuiheshimu, usibweteke, hakikisha unatengeneza wengi zaidi wa aina hiyo.
Kwani watu huwa wana tabia ya kuzoea vitu na kujisahau.
Mteja wako mzuri anaweza kudhani unachompa anaweza kupata popote.
Na hilo litamfanya aanze kuwa na kiburi na kukupangia uendesheje biashara yako, akijua hutakuwa na uthubutu wa kumpoteza.
Ni katika nyakati kama hizo ndiyo utamshangaza kwa jinsi utakavyokuwa tayari kumpoteza, ukijua hakuna atakapoweza kwenda kupata thamani unayompa.
Na pia ukijua akiondoka, kuna wengine tayari wanashika nafasi yake.

Kumbuka hukuingia kwenye biashara unyanyasike maisha yako yote.
Ungetaka hivyo ungeweza kuajiriwa na wengine na maisha yako yakaenda hivyo.
Umeingia kwenye biashara ili ujijengee uhuru mkubwa wa muda, kipato na maisha kwa ujumla, ufanye yale unayotaka na kufurahia kufanya.
Kama hutatoa thamani kubwa na kutengeneza wateja wengi, wateja watakunyanyasa na kukunyima uhuru ulioufuata kwenye biashara.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe