2980; Kubali kupitwa.

Rafiki yangu mpendwa,
Inapokuja kwenye swala la mafanikio, wengi huwa na mtazamo wa kutokukubali kupitwa na chochote.
Lakini huo ni mtazamo ambao unakuwa kikwazo kikubwa kwa wengi kupata mafanikio makubwa.

Tamaa huwafanya wengi kuhangaika na mengi wakidhani watairahisisha safari ya mafanikio, lakini kwa uhalisia wanaishia kuwa wameirefusha safari hiyo.

Elon Musk na Charlie Munger ni mabilionea wawili ambao wote ni watu wa mfano kwangu. Ni watu ambao nimechagua kujifunza kwao kwenye safari yangu ya ubilionea.

Mwaka 2008, kampuni ya Elon Musk inayoitwa Tesla, ambayo inazalisha magari ya umeme ilikuwa kwenye hali mbaya sana kifedha, ilikuwa inakaribia kufilisika.
Elon Musk akihangaika kutafuta fedha kwa watu wengi na moja wa watu hao akawa Charlie Munger.

Musk alipata nafasi ya kuongea na Munger na kumweleza kuhusu kampuni yake na kiasi cha fedha anachohitaji ili kuinusuru na kuifanya iwe kampuni yenye faida.
Munger alimpa Musk sababu nyingi sana za kwa nini kampuni yake itashindwa, na hivyo hakuwa tayari kuweka fedha za kampuni yao ya uwekezaji ambayo anaiongoza pamoja na bilionea mwingine Warren Buffett.

Musk anasema alisikitishwa sana na hilo, akamjibu Munger kwamba ni kweli kuna hatari nyingi za kampuni yake kufa kuliko kupona. Akaendelea kueleza, lakini kama kitu ni muhimu, mtu unakifanya, bila kujali hatari yake.

Waliishia hapo na matokeo yake ni kampuni ya Tesla iliweza kuvuka hatari zote na kuwa yenye thamani kubwa sana kwenye soko la hisa.

Sasa watu wamekuwa wakimcheka Munger kwamba alipitwa na fursa. Kwamba kama angewekeza kwenye kampuni ya Tesla kipindi hicho, angekuwa ameongeza utajiri mkubwa sana kutoka kwenye ukuaji wa kampuni hiyo.

Lakini je, Munger anachukuliaje hali kama hiyo? Anajutia kupitwa na fursa nzuri kama hiyo?
Jibu ni hapana, Munger siyo tu hajutii, bali anafurahia kabisa.
Amekuwa akijinasibu wazi kabisa kwamba hawekezi kwenye maeneo ambayo yeye binafsi hana ujuzi nayo kwa kina.
Na eneo kubwa ambalo yeye na mwendake Buffett hawana uelewa nalo na hivyo kuliepuka ni teknolojia mpya.

Msimamo wao huo umewakosesha fursa nyingi sana za kupata faida kubwa kwenye makampuni yaliyokuwa mapya na ambayo sasa yamekua sana, kama Microsoft, Amazon, Google n.k.

Lakini matokeo yake ni yapi?
Munger na Buffett ni mabilionea wakubwa duniani.
Buffett akiwa amepata nafasi ya kushika namba moja kwenye watu matajiri zaidi duniani kwa kipindi kirefu. Mpaka sasa Buffett yuko kwenye kumi bora ya watu matajiri zaidi.

Kuna mengi sana ya kujifunza kwenye hili tuliloshirikishana hapa, ambapo mengine utashirikisha kwenye maoni hapo chini.
Lakini kubwa kabisa ambalo nataka wote tutoke nalo hapa ni kwamba mafanikio siyo kutokupitwa na chochote. Bali ni kuamua baadhi ya mambo mazuri kabisa yakupite kwa kuwa umechagua baadhi ambayo utakuwa bora zaidi.
Na kwa hayo uliyochagua kuwa bora zaidi yana fursa ya kukupa mafanikio yoyote unayotaka.

Acha kugangaika na kila fursa mpya inayokuja kwako, hasa zile ambazo haziendani na fursa kuu ulizochagua.
Hilo litakupa fursa ya kutumia vyema fursa ambazo tayari umeshazichagua sasa.

Tukumbuke mafanikio yapo kwenye kila eneo, kadiri unavyoweka juhudi na umakini kwenye eneo lolote ulilochagua, ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi kubwa ya kufanikiwa kuliko kuhangaika na kila fursa mpya inayojitokeza, hata kama ni nzuri na ya uhakika kiasi gani.

Hii haimaanishi kwamba utaacha kabisa kufanyia kazi fursa zote mpya. Ila inamaanisha utafanyia kazi fursa mpya kwenye maeneo ambayo tayari umeshayachagua na kupuuza maeneo mengine yote.

Tukubali kupitwa kwenye fursa nyingi nzuri ambazo haziendani na maeneo tuliyochagua ili tupate nafasi nzuri ya kuzama kwenye fursa za maeneo hayo na kupata mafanikio makubwa.

Je ni yapi mengine uliyojifunza kwenye hili la kupitwa? Shirikisha kwenye maoni hapo chini.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe