2985; Usipoteze hiyo kazi ambayo umeshaweka.

Rafiki yangu mpendwa,
Tofauti ya kufanikiwa na kushindwa siyo akili wala juhudi zinazowekwa.

Wanaofanikiwa na wanaoshindwa hawatofautiani sana kiakili.
Na juhudi wanazokuwa nazo pia hazitofautiani sana.

Tofauti kubwa ya wanaofanikiwa na wanaoshindwa inaanzia kwenye msimamo.
Wanaofanikiwa wanapeleka juhudi zao kwenye jambo moja kwa muda mrefu.
Wakati wanaoshindwa wanahamisha hamisha juhudi zao kwenye mambo mengi.

Hivyo hata kama watu hao wawili watafanya kazi au biashara kwa muda sawa, tofauti yao kubwa itaanzia kwenye msimamo wa ufanyaji.
Anayefanikiwa anakuwa amekusanya juhudi zake zote kwenye kitu kimoja kwa muda wote na hivyo anaweza kuleta matokeo ya tofauti.
Wakati anayeshindwa anakuwa ametawanya juhudi zake kwenye mambo mengi na kuishia kupata matokeo ambayo ni hafifu.

Ili kujikumbusha hili na kuacha kuwa kikwazo chako mwenyewe kwenye mafanikio, kila mara unapaswa kujikumbusha kwamba hupaswi kupoteza kazi ambayo tayari umeshaiweka.

Kila unapotaka kuacha kile ambacho umekuwa unafanya na kuanza kitu kipya, jikumbushe kuna kazi ambayo umeshaiwekeza kwenye hicho unachotaka kuacha.
Swali ni je upo tayari kupoteza kazi yote hiyo na kwenda kuanza upya?

Kama ni maji ya kisima umekuwa unapampu, kisha ukaona yanachelewa kutoka na kuamua kuachana nayo, tambua kuna maji yako njiani kuja.
Je upo tayari kuyapoteza maji hayo yarudi chini kwa wewe kuacha na kwenda kwenye mambo mengine?

Kama ni maji unachemsha na unaona kama yanachelewa kuchemka hivyo kutaka kuachana nayo, swali ni je upo tayari kupoteza moto wote ambao tayari umeshaenda kwenye maji hayo?
Kwa sababu kwa kuacha yatapoa na yakipoa utahitajika kuanza upya kuyachemsha.

Kama unaweka juhudi na huoni matokeo, siyo kwamba juhudi hizo zimepotea, bali bado zinajikusanya ndiyo ziweze kuzalisha matokeo makubwa.
Wajibu wako ni kuendelea kuweka juhudi hizo ili ziendelee kukusanyika na kukupa matokeo makubwa sana.
Pale unapokata tamaa na kuacha kufanya, unakuwa umepoteza juhudi zote za nyuma unazokuwa umeweka.

Usikubali kupoteza juhudi zote ambazo umeshaweka mpaka sasa.
Endelea na mapambano, mambo makubwa na mazuri yapo mbele yetu.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe