2989; Tusipingane na asili.

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna mambo yanayokuwa yanatokea, ambayo tunaweza kuwa hatukubaliani nayo au yanakuwa kikwazo kwetu.
Kwa kuwa tunataka kupata vitu fulani tunavyotaka, tunaona ni wajibu wetu kukabiliana na hayo yaliyotokea ili yasiwe kikwazo kwetu.
Na hapo ndipo tunapotengeneza matatizo makubwa yanayogharimu muda wetu mwingi na kuwa kikwazo kwa mafanikio makubwa zaidi.

Kama jambo lipo kwa asili, kujaribu kupingana nalo au kulijaribu ni kujisumbua bure.
Ndani yako unaweza kufikiri ni kitu rahisi kufanya na kilicho ndani ya uwezo wako.
Lakini siyo rahisi kihivyo, ni sawa na kutaka kubadili jua lisiwe linachomoza upande wa mashariki, badala yake lichomozee magharibi.

Kuna mambo mengi ya asili tumekuwa tunahangaika nayo na mara zote tunaangukia pua, ila bado hatujifunzi. Hapa tutaangalia machache.

Moja; uwezo wa watu.
Watu wana uwezo tofauti tofauti na hilo ndiyo limekuwa linaleta matokeo tofauti hata pale watu wanapofanya kitu kimoja.
Huwa tunadhani watu wote wanalingana, lakini siyo, hivyo kuwapeleka wote kwa usawa imekuwa inatugharimu sana.
Na kubwa ambalo limekuwa linatugharimu ni kuwapa watu vitu ambavyo vipo juu ya uwezo wao.
Kwa tamaa zao wanaweza kuahidi wanaweza, lakini uwezo wao unakuwa kikwazo na wanashindwa vibaya.
Kwa mfano unatafuta wafanyakazi, halafu unakutana na watu ambao hawana chochote cha kufanya kwa muda mrefu na hapo ukaona umepata wafanyakazi kirahisi. Hapo unapaswa kushtuka, kwa nini watu hao hawana kitu cha kufanya kwa muda mrefu? Hicho ni kiashiria kwamba uwezo wao ni mdogo. Sasa kama utaenda kuwapa majukumu makubwa kuliko uwezo wao, umejitengenezea matatizo.

Mbili; tabia za watu.
Sehemu kubwa ya maisha ya watu yanaendeshwa na tabia ambazo wanazo. Huwa tunajenga tabia, kisha tabia zinatujenga.
Tabia huwa ni ngumu sana kuvunja, hasa tabia ambazo ni mbaya.
Huwa tunakutana na watu wenye tabia za aina fulani na ambazo ni kikwazo kwetu, ila kwa sababu tunakuwa tunawahitaji sana, tunajiambia tutawabadili hizo tabia.
Hili ni jaribio la kupingana na asili ambalo halijawahi kumwacha mtu yeyote salama.
Haijalishi unatamani kiasi gani kumbadili mtu, hilo halipo ndani ya uwezo wako.
Ndiyo, mtu anaweza kubadilika kama akiamua na kudhamiria kweli, ila siyo kubadilishwa na wengine.
Na hata pale mtu anapoahidi kubadilika, usichukulie kama tayari hayo ni mabadiliko. Mabadiliko ni magumu hata kwa mtu mwenyewe, hivyo usijipe matumaini hewa.
Ni bora uanze na watu ambao tayari wana tabia unazozitaka, badala ya kujaribu kupingana na asili kwa kutaka kuwabadili watu tabia.

Tatu; hisia za watu.
Sisi binadamu ni viumbe wa kihisia, japo huwa hatupendi kukubali hilo.
Huwa tunafanya maamuzi yetu yote kwa hisia kwanza, kisha kuyahalalisha kwa mantiki.
Tunatamani sana tungekuwa watu wa kufanya maamuzi kwa mantiki, lakini hicho ni kitu ambacho hakipo kabisa.
Tunatamani pia wengine tunaojihusisha nao pia wangefanya mambo yao kwa mantiki, lakini hilo pia haliwezekani.
Tunahitaji hamasa na motisha ili kufanya chochote kile, hivyo pia ndivyo ilivyo na kwa wengine.
Hata kitendo cha kuamka tu kitandani, kinahitaji hamasa na motisha.
Tunapaswa kujipa hamasa na motisha kila mara na pia tunapaswa kuwapa hayo wengine.
Inaweza kuchosha kuwahamasisha watu kila mara, hasa wale unaojihusisha nao kwa muda mrefu, lakini huna namna nyingine. Acha usiwape hamasa na motisha na utaacha kupata matokeo unayotegemea kupata.

Kuna mengi sana kwenye asili ambayo hatupaswi kupingana nayo wala kujaribu kuyabadili. Haya matatu tuliyojifunza hapa yamekuwa ndiyo chanzo cha matatizo mengi tunayokutana nayo.

Ili kupunguza matatizo na changamoto nyingi tunazokutana nazo kwenye maisha, tukumbuke na kuzingatia haya matatu;
Moja; watu wanatofautiana uwezo, wape watu mambo yanayoendana na uwezo wao.
Mbili; watu huwa hawapendi kubadilika, hivyo anza na wale ambao tayari wana tabia unazotaka, badala ya kujiambia utawabadili watu tabia.
Na tatu; watu wanafanya maamuzi kwa hisia, mara zote wape hamasa na motisha ili wafanye maamuzi unayowataka wafanye.
Usijaribu kwenda kinyume na hayo matatu kama kweli unayataka mafanikio makubwa.

Pamoja na kujifunza haya hapa, bado utajaribu kwenda kinyume nayo, utaona unaweza kuwapa watu mambo yaliyo juu ya uwezo wao, unaweza kuwabadili na wanapaswa kufanya maamuzi kwa mantiki.
Ninachoweza kukuambia ni kila la kheri kwenye hayo mateso ya kujitakia na yasiyokuwa na manufaa yoyote.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe