2990; Usalama na Uhuru.

Rafiki yangu mpendwa,
Sisi binadamu huwa tuna mahitaji mbalimbali kwenye ngazi mbalimbali za maisha yetu.

Hitaji la chini na la msingi kabisa huwa ni usalama.
Huwa tunapenda kuwa na uhakika kwamba maisha yetu yanaweza kuendelea bila ya kikwazo chochote.

Hitaji la juu kabisa ni uhuru.
Huwa tunapenda kuwa huru, kuyaendesha maisha yetu kwa namna tunavyotaka sisi wenyewe.

Lakini kwa bahati mbaya sana, usalama na uhuru ni vitu ambavyo huwa haviendi pamoja.
Ni asili ya maisha kwamba ukitaka kuwa salama kabisa huwezi kuwa huru na ukitaka uhuru kamili, lazima uwe tayari kupoteza usalama.

Uhuru unahusisha kuchukua hatua za hatari, ambazo zina nafasi kubwa ya kushindwa na zinaondoa uhakika wa usalama.
Kwa kuwa uhuru unahusisha hatari, hatari hizo zinaondoa hali ya usalama.

Usalama unahusisha kuwapa wengine jukumu la kuchukua hatua za hatari ambazo hazikuathiri wewe moja kwa moja.
Japo utakuwa salama, lakini manufaa utakayopata ni madogo sana ukilinganisha na wale wanaochukua hatua za hatari.
Usalama ni kuwapa wengine jukumu la kuyaendesha maisha yako, ambapo mafanikio yako siyo kipaumbele kikubwa kwao.

Kuna usalama kwenye kuendesha biashara ndogo, ambayo upo mwenyewe na wewe ndiyo kila kitu. Huna wafanyakazi wa kukusumbua na unawahudumia wateja wako wachache vizuri.
Usalama huo unakuwa kikwazo kwako kukua zaidi kibiashara na kuingiza kipato kikubwa.

Uhuru wa kibiashara unatokana na kukuza biashara kwa viwango vya juu, ambalo linahusisha kuwa na watu wengi, ambao pia wanakuja na changamoto zao. Hilo linakuwa na hatari mbalimbali ambazo zinapunguza sana usalama.

Tukirudi kwenye uhalisia, akili zetu huwa zinakimbilia zaidi kwenye usalama. Ndivyo asili ilivyotujenga ili kuhakikisha tunaendeleza maisha yetu.
Lakini uhalisia ni kwamba hakuna usalama wa asilimia 100. Kila kitu kina hatari zake.

Chochote tunachoweza kuona kina usalama, ukichunguza kwa makini, utagundua bado kina hatari ndani yake.
Watu hudhani ajira ni njia salama ya kuingiza kipato, lakini ajira zina hatari ya mtu kupoteza, tena kwa sababu zilizo nje ya uwezo wake.
Kadhalika biashara ndogo, hatari ya kushindwa bado ipo, licha ya mtu kudhibiti kila kitu peke yake.

Hivyo basi, tunapaswa kuacha kujidanganya na usalama na kwenda kwenye uhuru moja kwa moja.
Tupambanie zaidi uhuru badala ya kuhangaika na usalama.
Tukazane kupata udhibiti badala ya kuwapa wengine udhibiti huo.

Uzuri ni kwamba, ukiwa na uhuru mkubwa, unakuwa na kiwango kizuri cha usalama pia, japo siyo kwa asilimia 100, kwa sababu hatari haziepukiki.

Ni lazima ujue na kukubali kwamba maisha ya mafanikio yameambatana na hatari mara zote.
Kama huwezi kuvumilia hatari yoyote, huwezi pia kuyavumilia mafanikio makubwa.
Lakini sasa, hata usipofanikiwa, bado unakuwa kwenye hatari, tena wakati mwingine hatari ambayo ni kubwa zaidi.

Tukishajihakikishia chakula, mavazi na malazi, kinachofuata kinapaswa kuwa ni kupambana kujijengea uhuru mkubwa.
Japo hilo litatuweka kwenye hatari, lakini hakuna kisichokuwa na hatari kwenye maisha.
Kitendo tu cha kuwa hai, ni hatari ya kifo, unatembea na hatari ya kifo muda wote.
Hivyo tunapaswa kuacha kuhangaika sana na usalama na badala yake tuhangaike zaidi na uhuru.

Badala ya kukazana kuwa salama, kazana kuwa huru.
Usalama ni kulinda goli usifungwe, maana yake huwezi kupata ushindi, lakini pia una hatari ya kufungwa.
Uhuru ni kushambulia ili ufunge goli, unakuwa kwenye hatari ya kufungwa, lakini pia una nafasi ya kushinda.
Uhuru utakuweka salama, lakini usalama hauwezi kukuweka huru.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe