2992; Ukomo wa watu wengine.

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi hawafanikiwi kwenye maisha yao kwa sababu wana ukomo ambao wamejiwekea kwenye fikra zao.

Wanakuwa wamefunga fikra zao kwa nini kinachowezekana na nini hakiwezekani.

Wanapokuona wewe ukiwa na fikra za kufanya makubwa, wanakuambia haiwezekani.
Kukuambia kwao haiwezekani, siyo kwamba haiwezekani kweli, bali huo ndiyo ukomo uliopo kwenye fikra zao.

Hakuna wa kuweza kukuambia wewe nini kinawezekana na nini hakiwezekani.
Hiyo ni kwa sababu hakuna mwenye maono kama uliyonayo wewe wala msukumo ulionao.

Watu wote walioweza kufanya makubwa hapa duniani, walipitia kupingwa na kukatishwa tamaa.
Wengine walionekana huenda wana matatizo ya akili.
Lakini kwa kuamini kwenye kile walichotaka sana na kung’ang’ana nacho, leo dunia inanufaika sana kupitia wao.

Unachukuliaje pale watu wanapokuambia ndoto kubwa ulizonazo haziwezekani?
Unachukuliaje pale wewe peke yako ndiye unayefanya kinyume na kundi kubwa la watu wanaokuzunguka?

Sisi binadamu ni rahisi kufuata mkumbo, lakini mafanikio makubwa hayajawahi kutokea kwenye mkumbo.
Ni lazima uweze kusimama mwenyewe, usimamie picha unayoiona kwenye fikra zako, utumie msukumo mkubwa ulio ndani yako.

Mafanikio makubwa yapo kwa wachache kwa sababu wao ndiyo wanaoweza kuvumilia upweke wa kusimama wenyewe, wanaoweza kupuuza kupingwa na kukatishwa tamaa na wengine.
Je wewe umejitoa kiasi gani kuhakikisha kweli unazifikia ndoto kubwa ulizonazo?

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe