2994; Tatu bila.

Rafiki yangu mpendwa,
Haya maisha ni sawa na mchezo wa mpira wa miguu.
Urahisi au ugumu wa sisi kupata ushindi unategemea sana uelewa wetu wa pale tunapoanzia na juhudi tunazoweka.

Kwenye mpira wa miguu, timu inayokuwa nyuma kwa magoli, yaani ambayo inakuwa imefungwa, inakuwa kwenye nafasi kubwa ya kushindwa.
Na kadiri muda unavyokwenda huku timu ikiwa nyuma, ndivyo kushindwa kunakuwa kwa uhakika.
Timu inayokuwa nyuma kwa magoli inapaswa kuweka juhudi za ziada ili iweze kupata

Kwenye mchezo wa maisha, watu wengi wanashindwa kwa sababu wanaanza wakiwa nyuma kwa magoli, lakini wanacheza kawaida badala ya kuweka juhudi za ziada.
Wanakuwa wanalinda goli kuliko kushambulia ili kupata ushindi.

Tunaanziaje nyuma kwenye huu mchezo wa maisha?
Kwa wengi, tunaanza huu mchezo tukiwa tayari tumefungwa magoli ya kutosha.
Hivyo ili tumalize kwa ushindi, tunalazimika kuweka juhudi kubwa mno.

Kuzaliwa kwenye nchi masikini unakuwa unaanza ukiwa umefungwa goli moja, yaani ni moja bila, unaingia kwenye mchezo ukiwa tayari umefungwa.
Hiyo ni kwa sababu kwenye nchi masikini mazingira na mifumo mingi inakuwa kikwazo kwa mtu kufanikiwa.
Kwa kuzaliwa kwenye nchi masikini, unapoteza muda mwingi kuhangaika na mambo yasiyokuwa na tija kabisa.
Kuna vikwazo vingi vinavyokuwa nje ya uwezo wako, ambavyo vitapoteza sana muda na fedha zako.

Kuzaliwa kwenye nchi masikini na familia masikini unakuwa umefungwa magoli mawili kwa bila kwenye kipindi cha kwanza cha mchezo.
Hiyo ni kwa sababu unapozaliwa kwenye familia masikini, unakuwa huna pa kuanzia, yaani unaanzia sifuri.
Lakini kama hiyo haitoshi, unakuwa na kundi kubwa la wanaokutegemea.
Hivyo hata ukipiga hatua kidogo, utavutwa nyuma na kundi hilo la wategemezi.

Kuzaliwa kwenye nchi masikini, familia masikini na ukawa na tabia za kimasikini ni tatu bila kwenye kipindi cha pili cha mchezo.
Yaani tayari umeshafungwa magoli matatu na mchezo upo kwenye kipindi cha pili.
Kupata ushindi katika hali kama hiyo ni lazima uweke juhudi kubwa mno, juhudi zisizo za kawaida kabisa.
Tabia za kimasikini zina nguvu kubwa ya kumkwamisha mtu asiweze kupiga hatua kwenye maisha.
Hata kama ataweka juhudi kiasi gani, bado tabia hizo zitakuwa kikwazo kwake.

Tabia za kimasikini zipo nyingi, lakini kubwa zinazowakwamisha wengi ni uvivu na uzembe. Uvivu ni kutokufanya kile ambacho mtu anapaswa kufanya. Na uzembe ni kukifanya kwa namna isiyo sahihi.
Uvivu na uzembe ni vikwazo vikubwa sana kwa mtu kuweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yake, hata kama amedhamiria kwa kiasi gani.
Kadiri mtu anavyochelewa kuachana na tabia hizo za kimasikini, ndivyo anavyojiweka kwenye nafasi kubwa ya kushindwa.

Unapogundua kwamba umezaliwa kwenye nchi masikini na familia masikini, halafu una tabia za kimasikini, unahitaji kupambana mno. Huhitaji kuangalia wengine wanafanya nini au wanafanyaje, wewe unapaswa kupambana kufa na kupona. Maana kadiri unavyochelewa ndivyo unavyozidi kuukosa ushindi unaoutaka.
Na hata kama umeshazivuka tabia za kimasikini, bado unahitaji kuendelea kujisukuma zaidi ili uweze kuvuka vikwazo vingine ambavyo tayari vinakuzuia usipate mafanikio makubwa.

Ndiyo, unaanza ukiwa nyuma, lakini hiyo haimaanishi kwamba huwezi kupata ushindi mkubwa unaoutaka.
Ushindi unaoutaka unawezekana, ila jitihada utakazopaswa kuweka siyo za kawaida ni za juu sana, ambazo kwa hali ya kawaida utaonekana kama unajitesa.

Siyo wajibu wako kuwafurahisha na kuwaridhisha wengine.
Wajibu wako ni kupata ushindi kwenye maisha.
Na kwa bahati mbaya sana unaanza ukiwa nyuma.
Hivyo huna budi kuweka juhudi za ziada.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe