3000; Aftatu.

Rafiki yangu mpendwa,
Leo ni siku ya elfu tatu ya kuandika kila siku bila kuacha.

Siku hizo elfu 3 zilizopita, nilijipa changamoto ya kuhakikisha kila siku naandika.

Na sharti lilikuwa rahisi sana, kama kwenye siku napata muda wa kuoga, kula, kulala basi pia natakiwa kupata muda wa kuandika.

Sikuanza kujiambia vipi kama…
Wengi wanapotaka kujiwekea malengo au changamoto za aina hii huwa wanaanza na maswali ya vipi kama…
Vipi kama nitaumwa?
Vipi kama nitakosa kifaa cha kuandikia?
Vipi kama nitakuwa eneo lisilokuwa na mtandao?
Na mengine mengi ambayo watu wamekuwa wanatumia kama sababu.

Ushauri ambao nimekuwa nawapa watu pale wanapokuja na maswali ya vipi kama… ni huu; utavuka daraja utakapolifikia.
Kama kuna safari umepanga na njia unayopita ina daraja hatari, haitasaidia wewe kuhofia utalivukaje hilo daraja.
Badala yake unatakiwa kuendelea na safari ukijua kwamba daraja utalivuka pindi utakapolifikia.

Ushauri mwingine muhimu ni kutenga muda wa kufanya mambo muhimu kila siku.
Mambo yote ya msingi kwenye maisha yako, huwa unayafanya kila siku bila kuacha.
Hata uwe umetingwa kiasi gani, bado utatenga muda na kufanya yaliyo muhimu.
Kila siku utasafisha mwili wako, utapata chakula na utapumzika au kulala.
Hakuna siku unayokuwa umetingwa sana kiasi cha kuyaahirisha hayo ya msingi.

Kuna somo kubwa sana tunalojifunza hapo kwenye yale ya msingi.
Kama jambo ni muhimu kweli, muda wa kulifanya huwa unapatikana.

Jipe changamoto ya kufanya kitu kila siku bila ya kuacha hata mambo yaweje.
Chagua kitu kimoja ambacho utakifanya kila siku bila ya kuacha hata siku moja.
Unapochagua kitu hicho, usianze kujiuliza maswali ya vipi kama …..
Wewe jiambie utafanya halafu ufanye kweli bila kuruhusu sababu au visingizio vyovyote kukuzuia.

Kupanga kufanya kitu kila siku na kutekeleza kama ulivyopanga ni ushindi mkubwa sana kwenye siku ya maisha yako.
Kila siku kunakuwa na ushindi ambao unaupata bila kujali siku husika imeendaje.
Siku iwe nzuri au mbaya kwako, tayari kuna ushindi umeshaupata kwa kutekeleza kile ulichopanga kufanya kila siku bila kuacha.

Jambo la mwisho ni unapaswa kuwa na kichwa ngumu sana ili mambo yako yaende kama ulivyopanga.
Kwa sababu kuna mengi yatakayojitokeza na kutaka kuathiri yale uliyopanga.
Ukiruhusu hilo litokee, hata kwa mara chache tu, utajenga mazoea yasiyo sahihi na itakuwa kikwazo kwako kutekeleza kama ulivyopanga.
Kuwa mbishi na kuwa king’ang’anizi hasa ili uweze kufanya kama ulivyopanga.
Kuna wakati utajishawishi kwamba unaweza tu kuacha siku moja kwa yale unayokuwa unapitia.
Hapo ndipo unapopaswa kuelewa kwamba ukisharuhusu mara moja, utaruhusu tena na tena na tena.
Kuondokana na hilo ni kutokukubali sababu yoyote kuwa kikwazo kwako kwenye yale uliyoyapanga.

Je ni kitu gani ambacho umechagua kuwa unafanya kila siku bila kuacha hata siku moja?
Shirikisha kwenye sehemu ya maoni hapo chini.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe