3002; Unajiangusha mwenyewe.

Rafiki yangu mpendwa,
Hakuna mtu yeyote anayeweza kukuangusha kwenye maisha yako isipokuwa wewe mwenyewe.

Chochote unachotaka kwenye maisha na hujakipata, hakuna aliyekunyima ila wewe mwenyewe.
Ni wewe ndiye unayejizuia kupata yale yote unayoyataka kwenye maisha yako.

Na picha linaanzia pale unachotaka hakiendani na kile unachofanya.
Unakuwa unataka makubwa sana, lakini unachofanya ni kidogo sana.

Malengo unayokuwa nayo ni makubwa,
Lakini hatua unazokuwa unachukua ni ndogo sana au wakati mwingine hata haziendani na malengo uliyonayo.

Ni sawa na una safari ya kwenda kisiwani, ambapo usafiri ni wa majini, lakini wewe unaenda kwenye kituo cha basi.
Halafu ukiwa pale unalalamika umeangushwa kwa sababu hujapata usafiri.

Malengo yote makubwa ambayo umewahi kujiwekea kwenye maisha yako na hujayafikia, hakuna mwingine aliyekuzuia isipokuwa wewe mwenyewe.

Ndiyo, panaweza kuwa na changamoto mbalimbali za nje, lakini kama unakuwa umejitoa kweli kweli kutoka ndani yako, hakuna cha kukuzuia.

Hivyo sababu pekee ya kushindwa kwenye maisha ni kujizuia wenyewe.
Kutaka na kupanga makubwa, lakini kuchukua hatua ambazo ni ndogo sana na haziwezi kukupa matokeo unayokuwa unayataka.

Halafu sasa, ni kujitesa.
Kuwa na malengo makubwa, halafu kuchukua hatua ndogo, ni kujitesa kinafsi.
Haina maana kuendelea kutaka vitu vikubwa kama haupo tayari kujitoa kafara ili kuvipata.
Ni kujitesa tu bure, kujitamanisha na makubwa ambayo huwezi kuyapata kwa sababu hujitoi vya kutosha.

Kama unajiona huwezi kuishi aina ya maisha unayopaswa kuishi ili kufikia malengo makubwa uliyonayo, ni bora kuachana na tamaa ya malengo hayo makubwa.
Kama unajiona huwezi kukaa kwenye mchakato unaokupeleka kwenye matokeo unayoyataka, ni bora uachane nayo.

Kutamani matokeo na siyo mchakato ni njia ya uhakika ya kujiangusha wewe mwenyewe.
Na sehemu kubwa ya maisha ya watu imepotelea kwenye hilo.
Wanayatamani sana matokeo, lakini wanapuuza mchakato.
Mwishowe wanayakosa matokeo na kuanza kulaumu wengine.

Kama kuna kitu unakitaka na hujakipata, hupaswi kumlaumu mtu mwingine yeyote.
Unapaswa kuwa kwenye mchakato wa kupata kitu hicho bila ya kuchoka.
Au unapaswa kujilaumu kama hata haupo kwenye mchakato.

Yaani kama bado hujapata unachotaka, unapaswa kuwa kwenye mchakato wa kukipata muda wote bila kuyumba.
Na kama upo kwenye mchakato sahihi, hupaswi hata kuwa na wasiwasi, ni swala la muda tu kupata kile unachotaka.

Lakini kama hujapata unachotaka na pia haupo kwenye mchakato wa kukipata, hupaswi hata kuwa unakizungumzia, iwe ni kwa wema au ubaya.
Hujapata unachotaka na haupo kwenye mchakato wa kukipata basi kaa kimya.
Chochote utakachosema hakina maana.
Kwa sababu utakimbilia kulaumu wengine wakati wewe mwenyewe ndiye uliyejiangusha.

Matakwa yako yaendane na hatua unazochukua.
Kama unataka makubwa, lazima pia uchukue hatua ambazo ni kubwa.
Kama haupo tayari kuchukua hatua kubwa, ambazo pia zitakuukiza, ni bora uachane na tamaa za hayo makubwa.
Kwa sababu ni kujitesa na tamaa kama haupo tayari kujitoa kafara kuzitimiza.

Chochote unachotaka kwenye maisha yako kinawezekana kama upo tayari kulipa gharama ya kukipata.
Kama kuna kitu unataka na hujapata, tatizo ni hujalipa gharama unayopaswa kulipa.
Lipa gharama yote unayotakiwa kulipa bila kujali ukali wake na utaweza kupata kila unachotaka kwenye maisha yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe