3009; Umasikini na uaminifu.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye makala ya ukurasa wa 3008 uliopita niliandika;
‘Hakuna kitu kama masikini mwenye furaha,
Au masikini mwaminifu.
Furaha na uaminifu haviwezi kukaa pamoja na umasikini.’

Kila mtu alikubaliana na upande kwamba hakuna masikini mwenye furaha.
Na hilo liko wazi kwamba huwezi kuwa na furaha kama huna uhakika wa wapi utapata fedha ya kula kesho, au unakosa mahitaji mengine muhimu.

Lakini baadhi ya watu hawakukubaliana na upande kwamba hakuna masikini mwaminifu. Waliona kuna masikini ambao wapo vizuri tu kwenye eneo la uaminifu.
Na mimi nalikataa hilo kata kata.
Hakuna masikini ambaye ni mwaminifu.

Kwa kuanza, kitendo tu cha kuwa masikini kinamweka mtu kwenye hali ya kukosa uaminifu.
Masikini ni rahisi kushawishika kudanganya au kudokoa ili kupata kitu fulani anachoshindwa kupata kwa sababu ya umasikini wake.
Kwa mfano kama una njaa na huna fedha ya kupata chakula, ni rahisi kwako kuhalalisha kudanganya ili upate chakula.
Ni wachache sana ambao wapo tayari kusimamia ukweli kwenye hali za aina hiyo.

Jambo la pili na kubwa kabisa ni umasikini ni matokeo ya kufanya au kutokufanya vitu fulani.
Ndani ya kila mmoja wetu tayari upo uwezo mkubwa wa kupata chochote ambacho anataka.
Kama mtu ni masikini, kuna namna ameshindwa kutumia uwezo mkubwa ambao tayari anao.
Je unadhani ni uaminifu kushindwa kutumia kitu ambacho tayari kipo ndani yako?
Jibu ni hapana, kama unashindwa kutumia vizuri kitu chenye manufaa ambacho unacho, unakosa uaminifu kwako mwenyewe na hata kwa wengine pia.

Tatu na mwisho tunakubaliana umasikini ni dhambi kubwa sana kwenye maisha, ambayo tunapaswa kupambana nayo ili kuitokomeza kabisa kwenye maisha yetu.
Je unadhani dhambi inaweza kuwa na uaminifu?
Jibu ni hapana, dhambi na uaminifu haviwezi kwenda pamoja.
Unakuwa na dhambi pale unapokosa uaminifu.
Hivyo kitendo tu cha kuwa masikini, tayari unakuwa umekosa uaminifu.

Umasikini ni mbaya,
Umasikini ni dhambi,
Umasikini ni kukubali kuishi maisha ambayo siyo ya hadhi yako.
Hatupaswi kuuremba na kuubembeleza umasikini kwa namna yoyote ile.
Ni adui tunayepaswa kumpa kila aina ya jina baya na kumshambulia kisawasawa.
Maana yeye mwenyewe anapopata nafasi anatushambulia kikatili.

Kuutetea umasikini kwa namna yoyote ile ni kuukaribisha na kuukumbatia kwenye maisha yako, kitu ambacho kinafanya uendelee kuwa masikini.
Umasikini ni adui ambaye hastahili huruma yoyote kutoka kwako.
Unapaswa kumshambulia kwa silaha yoyote unayoweza kuwa nayo.

Hata kama unaanzia kwenye umasikini, usikubali kwamba wewe ni masikini.
Kamwe usijiite masikini, bali jiite tajiri uliye kwenye matengenezo.
Uchukie na kuukataa umasikini na mambo mengine yote yanayohusiana nao.
Umasikini ni adui ambaye hahitaji huruma wala utetezi wako, bali mpe adhabu anayostahili.
Umasikini unatesa na kudhalilisha, hupaswi kuuonea huruma kwa namna yoyote ile.
Ushambulie na kuuangusha ili kuweza kujenga maisha bora kwako.

Nimalizie kwa kusema kwamba kama inabidi ushawishiwe kwamba umasikini ni mbaya na haustahili utetezi wowote, basi itakuwa vigumu sana kwako kutoka kwenye umasikini huo.
Hatua ya kwanza kwenye vita yoyote ni kumpa adui jina baya, ili uweze kumshambulia bila kujali.
Kwenye mapambano yako na umasikini, upe majina yote mabaya na ushambulie bila ya huruma.

Achana na jamii inayoonekana kutetea umasikini na masikini kwa nguvu kubwa.
Huo ni mkakati wa kuwafanya masikini wajisikie vizuri na kuendelea kubaki kwenye umasikini wao, kitu kinachowafanya watawalike kirahisi kwenye jamii.
Wewe ukatae na uchukie umasikini, usiutetee kwa namna yoyote ile.
Adui mtesi hahitaji huruma yako, ni wa kuangushwa na kuvunjwavunjwa.

Umasikini hauendani na furaha,
Umasikini hauendani na uaminifu,
Tuupinge, kuukataa na kuushambulia umasikini kwa kila namna bila ya kuuonea huruma.
Maana wenyewe ukipata nafasi, unatutesa sana bila ya huruma yoyote.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe