3024; Kazi itakayokulipa vizuri wakati wote.

Rafiki yangu mpendwa,
Ukitaka upotee na kukosa kabisa mafanikio kwenye hizi zama tunazoishi, sikiliza na fanyia kazi kila aina ya ushauri unaopewa na kila mtu.

Kumekuwa na ushauri mwingi kinzani ambao umekuwa unatolewa na watu wengi kwenye mambo mbalimbali.

Na sehemu kubwa ya ushauri huo huwa ni nini kinalipa au hakilipi.
Watu wanaotoa ushauri huo huwa wanajiamini sana wakati hawana uzoefu au matokeo yoyote kwenye hayo wanayoshauri.

Kwa bahati mbaya sana washauri hao huwa ni mawakala wazuri wa kueneza hali mbaya na kujenga hofu kubwa ndani ya watu.
Huwezi kuwasikiliza watu hao wanavyoshauri kwa kujiamini na ukabaki salama.
Lazima wataacha wasiwasi mkubwa ndani yako ambao utaathiri sana kile unachofanya.

Kila wakati watu hao huwa wanakuwa na habari njema na habari mbaya.
Lakini huwa wanaweka mkazo zaidi kwenye habari hasi ili kuwafanya watu wajawe na hofu na kuchukua hatua fulani wanazozotaka ili wanufaike.

Tutaangalia mifano miwili kuelewa vizuri hii dhana.
Mfano wa kwanza ni kwenye teknolojia.
Kuna watu huwa wanatumia mabadiliko yanayoendelea kwenye teknolojia kutafuta njia za kuwajaza watu hofu ili wajinufaishe nao.
Kila kunapokuwa na teknolojia mpya ambayo wengi hawajaielewa, watu hao huwa wa kwanza kuonyesha ni jinsi gani wale ambao hawajaanza kutumia teknolojia hiyo mpya watakavyopoteza.

Watu wale wale ambao mwaka juzi walikuwa wanakuambia Bitcoin (fedha za kidijitali) ndiyo kila kitu na kama huzimiliki utakufa masikini.
Ndiyo hao hao ambao mwaka jana walikuwa wanakuamboa NFT (umiliki wa picha kidijitali) ndiyo kila kitu na kama huna umiliki huo wewe ni masikini mkubwa.
Na ndiyo hao hao ambao mwaka huu wanakuambia chatGPT (lugha ya kuwasiliana na kompyuta) ndiyo kila kitu na itachukua kazi zote ambazo watu wanafanya.
Ukiwafuatilia watu hao mara zote utajawa hofu na kuona tayari umeshapoteza.

Tukiangalia mfano wa pili ambao ni kwenye mambo ya kawaida.
Watu wale wale ambao mwaka juzi walikuambia ufugaji wa kware ndiyo kila kitu na kama huwafugi utakufa masikini.
Ndiyo hao hao mwaka jana wakakuambia ufugaji wa sungura ndiyo habari ya mjini na kama huna sungura hujui unachofanya.
Na ndiyo watu hao hao mwaka huu wanakuambia ufugaji wa bata ndiyo habari yenyewe, mwingine kote unajichelewesha.
Ukiangalia mambo ni yale yale, kupeana hofu kwa mambo yanayobadilika badilika.

Leo nataka nikutoe hofu zote ambazo umekuwa unajazwa kuhusu kuachwa nyuma kama hukimbizani na kila kitu kinachobadilika.
Nataka nikuambie kazi itakayokulipa vizuri wakati wote na ambayo haitakutaka ukimbizane na kila aina ya manadiliko yanayoendelea.

Kazi hiyo ni mauzo.
Ukijifunza na ukawa muuzaji mzuri na aliyebobea, utakuwa na fursa zitakazokulipa vizuri kwa kipindi chote cha uhai wako.
Ukiwa muuzaji mzuri, haijalishi ni teknolojia gani imekuja, wewe utaendelea kuingiza kipato kikubwa zaidi.
Wauzaji bora hawana hofu ya kitu chochote kuathiri kipato chao, kwa sababu wanajua mauzo yatathaminiwa wakati wote.

Haijalishi ni mabadiliko gani yanayoendelea kiteknolojia, mauzo yataendelea kuwa fursa kubwa kwa sababu bado watu wanahitaji kushawishiwa kuchukua hatua sahihi.
Haijalishi ni ufugaji gani unaolipa zaidi, mauzo yataendelea kulipa kwa sababu hivyo vinavyofugwa vitahitaji watu washawishiwe ndiyo waweze kuvitumia.

Jifunze na uwe muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea na hutakuwa na hofu juu ya mabadiliko mbalimbali yanayoendelea.
Sisemi hutahitaji kubadilika, mabadiliko ni lazima.
Ninachosema ni hutahitaji kuhofia chochote kinaweza kuathiri sana kipato chako, kwa sababu ujuzi unaokuwa nao ni wenye nguvu ya kukulipa kwenye nyakati zote.

Kuwa muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea na hakuna kitakachoweza kuathiri kipato chako kwa kiwango kikubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe