3026; Anza upya kila siku.

Rafiki yangu mpendwa,
Mwanzo wa kitu chochote kile huwa ni wa shauku na hamasa kubwa.
Mtu unapokuwa unaanza kufanya kitu, unakuwa na msukumo wa kuweka juhudi kubwa ili kupata matokeo mazuri.

Msukumo na juhudi hizo za awali huwa zinapelekea mtu kupata matokeo mazuri na kumpeleka ngazi za juu.
Mtu anakuwa amepiga hatua fulani kwenye kile anachokuwa anafanya.

Na hapo sasa ndipo hatari kubwa inapomnyemelea mtu.
Mtu anabadilika, anaacha kushambulia kama alivyokuwa anafanya awali, badala yake anaanza kulinda matokeo ambayo ameshayapata.

Ule msukumo na juhudi za awali zinaondoka na nafasi yake kuchukuliwa na mazoea.
Mtu anaanza kufanya kwa mazoea huku akilinda matokeo ambayo ameshayapata yasipotee.

Hali hiyo ya mazoea na kulinda matokeo ya nyuma ndiyo huwa inawaangusha wengi baada ya kupata mafanikio kidogo.
Watu wanakuwa wanapanda vizuri mwanzoni, lakini baadaye wanapata anguko kubwa.

Kuondokana na hali hiyo ya kupanda na kushuka kimafanikio, unapaswa kuwa unaanza upya kila siku.
Kila siku jichukulie kama ndiyo unaanza kufanya chochote unachofanya.
Sahau hatua zozote ambazo umeshapiga na epuka kutaka kulinda matokeo ambayo umeshayapata.
Wewe jione kama ndiyo unaanza upya, hilo litakusukuma uweke juhudi kubwa na za tofauti kitu ambacho kitakupa matokeo makubwa.

Hakuna kitu kinachoharibu mafanikio kama mazoea na kulinda matokeo ya nyuma.
Hiyo inakupa hali ya kuridhika na kuona kama umeshamaliza kila kitu.
Ni katika hali hiyo ya kuridhika ndiyo changamoto na matatizo mbalimbali hujitokeza na kumwangusha mtu vibaya.

Unapokuwa na mtazamo wa kuanza upya kila siku, unakuwa na msukumo wa kufanya tofauti, kitu ambacho kinaondoa mazoea na kukupa matokeo ya tofauti.

Kila siku jichukulie ndiyo unaianza biashara yako.
Pamoja na wateja ambao tayari unao sasa, chukulia wote wamekuacha na huna mteja tena.
Weka juhudi za kutosha kila siku kuzalisha mafanikio mapya.
Mafanikio yoyote ya nyuma yasahau kabisa, kwani hayo yana hatari ya kukuangusha.

Hakuna kitu kinalevya na hatari kama mafanikio.
Mafanikio yana tabia ya kuleta kiburi na mazoea kwa mtu, vitu ambavyo vinakaribisha anguko kubwa.
Chochote unachofanya kwa mazoea na kulinda usipoteze, kinaishia kuwa na changamoto ambazo zitapelekea kupoteza zaidi.

Kila siku jiweke kwenye hali ya hatari ya kupoteza kila ulichonacho na hiyo itakusukuma ufanye kwa ukubwa na utofauti.

Hivi umewahi kugundua kwamba wakati ambao upo bize sana ndiyo pia wakati ambao unafanya makosa machache sana yasiyo na tija?
Ndiyo huwa iko hivyo, unapokuwa umetingwa hasa, huwa huhangaiki na mambo yasiyokuwa na tija na hivyo kupunguza makosa yasiyo na tija pia.

Sahau mafanikio yoyote ambayo umeshayapata huko nyuma na anza upya kila siku.
Kuwa na njaa ya mafanikio mara zote na jisukume sana katika kuchukua hatua mpya kwa yale unayokabiliana nayo.
Usifanye kitu leo kwa sababu ulikifanya jana pia, hata kama utakifanya kama jana, lakini sababu ya kukifanya leo inatakiwa kuwa tofauti na ya jana.

Usilinde sana chochote ambacho umeshakipata, itakuzuia kuchukua hatua mpya na hatari na hivyo kukunyima matokeo mapya na makubwa.
Mara zote shambulia kama ndiyo unaanza, ukiwa na hasira ya kufanya makubwa zaidi.

Jiweke kwenye hatari ya kupoteza makubwa kama utafanya kwa mazoea. Hilo litakusukuma uachane na mazoea na ufanye kwa utofauti ili kutokupoteza kwenye hatari uliyojiweka.

Kukosa hamasa na msukumo huwa ni zao la mazoea, ambayo hujitokeza pale mtu anapolinda matokeo ambayo ameshayapata badala ya kushambulia ili kupata matokeo mapya na bora zaidi.
Kama unataka kuwa na hamasa isiyoisha, kila wakati anza upya.
Sahau matokeo ambayo umeshayapata na jichukulie unaanza upya kabisa.
Ni hali hiyo ya kuanza upya ndiyo inayokuweka kwenye hali ya kujisukuma sana ili kupata matokeo bora zaidi.

Mafanikio yoyote ambayo umeshayafikia, jua unaweza kwenda zaidi ya hapo.
Lakini kilochokufikisha hapo ulipofika sasa, siyo kitakachokupeleka mbele zaidi.
Achana na mazoea yote ya nyuma na kulinda mafanikio hayo ambayo umeshayapata.
Badala yake anza upya kila wakati ili kuwa na njia bora za kupata matokeo ya tofauti.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe