Hasira ni miongoni mwa hisia hasi ambayo imekuwa ikiwagharimu watu wengi.
Mpaka sasa hakuna mtu ambaye anaweza kusema hajawahi kufanya maamuzi ya hasira ambayo yalipelekea kuharibu kazi, biashara na hata kuvunja mahusiano yetu.
Tatizo la hasira ni ukichaa wa muda na Mwanafalsafa Seneca anafananisha hasira na ukichaa wa muda.
Kwa nini ni ukichaa wa muda kwa sababu mtu anapokuwa na hasira anakuwa hawezi kufikiri kwa usahihi.
Mtu anapokuwa na hisia za hasira, hisia zinakuwa juu na fikra chini hivyo mtu anashindwa kufanya maamuzi sahihi.
Ziko hisia nyingi lakini hasira ndiyo hisia hasi ambayo haina hata faida.
Falsafa ya hasira ni hasara siku zote. Lakini wako watu ambao huwa wanajisifu kabisa kwamba mimi nina hasira ninaweza kukupiga, kukua, na mengine mengi na utashangaa anafanya kweli na pale ukichaa ukishaisha anaanza kuona hatia juu yake.
Kifupi hatuwezi kuepuka hisia ya hasira kwenye maisha yetu, kwa sababu wako watu ambao ni wajinga, washenzi, wakorofi ambao wanatuudhi kwa makusudi au pasipo sisi kupenda na inapelekea kukasirika.
Kibinadamu kila mtu anawakwa na hasira pale mtu anapokuwa ametendewa ndivyo sivyo.
Lakini changamoto inakuja pale ambapo sisi tunakuwa tunaiendekeza hasira ituendeshe vile inavyotaka ituendeshe bila kujidhibiti.
Wabudha wanasema kuruhusu hasira zikutawale ni kama kushikilia kaa la moto huku ukitaka kumrushia mtu mwingine. Kumbuka, wewe ndiyo utakaye ungua.
Pale mambo yanapokwenda tofauti na vile tulivyopanga tunaanza kupata hasira. Kwa mfano, mtu alikuahidi atakupatia fedha siku fulani halafu mtu asikupe fedha kama alivyokuahidi.
Tunapata hasira pale mtu anapotutukana lakini tunapaswa kujiuliza hasira zinatoka wapi?
Falsafa ya ustoa inatufundisha kuwa mtu anaanza kuwa na hasira pale anapokuwa anaanza kuhoji kitu kadiri ya tafsiri zake binafsi kwa mfano, kwa nini amenitukana, amenionaje? Ameniona mimi sifai?
Mwanafalsafa Epictetus anasema kile kitendo cha kutafsiri ndiyo kinaleta shida lakini tukichukulia kawaida haiwezi kutudhuru bali tafsiri zetu juu ya kitu ndiyo kinafanya kitu kionekane kibaya au kizuri.
Falsafa ya ustoa inatufundisha kuwa kiasili hakuna kitu kibaya wala kizuri ila tafsiri zetu juu ya kitu hicho ndiyo kinapelekea kitu kuwa kizuri au kibaya.
Baada ya kuangalia namna mtu anavyozalisha hasira, kinachofuata baada ya hapa ni namna gani tunaweza kukabiliana na hasira.
Jinsi ya kukabiliana na hasira ndiyo shabaha yetu ya msingi kabisa ya somo la leo. Tunawezaje kukabiliana na hasira?
Kitu muhimu cha kufanya pale unapokuwa na hasira ni kujichelewesha kuchukua hatua.
Cheza na hasira yako ikiwezekana ondoka eneo ambalo limesababisha wewe kuwa na hasira tulia kabisa mpaka hasira yako iishe na wala usichukue hatua yoyote ile.
Unapaswa kutulia kwa sababu ukichukua hatua unakuwa umetimiza lengo la yule aliyekukasirisha. Ukifanikiwa kumjibu aliyekuudhi maana yake umemsaidia kufanikisha lengo lake la kukuudhi.
Epictetus anasema mtu hasumbuliwi na kitu lakini tafsiri yake juu ya hicho kitu ndiyo kinamsumbua au maoni yake binafsi anayotoa ndiyo yanapelekea shida.
Hapa falsafa ya ustoa inatufundisha kwamba mitazamo yetu tuliyonayo juu ya kitu ndiyo inatupa matokeo mazuri au mabaya.
Kupata hasira juu ya mtu fulani ni uwezo wa kushindwa kuelewa mambo.Wengine wanapata hasira kwenye vitu vidogo bila hata kupata taarifa au uelewa wa kitu kwa undani au kuona vitu katika mitazamo tofauti.
Kitendo cha wewe kutawala hasira zako ni kitendo cha kuonesha kwamba umekua, umekomaa, hujajishikilia au kujishikiza kwenye kitu au vitu na uko huru hujafungwa na mambo ya nje. Lakini ukishakuwa na hasira na kuchukua hatua juu ya hasira hiyo maana yake unakuwa umempa nguvu au mamlaka yule aliyekukasirisha.
Hatua ya kuchukua leo; dhibiti hasira zako na usiruhusu hasira zikutawale kwa kuchukua hatua bali jicheleweshe kufanya chochote au kuchukua hatua na badala yake vuta pumzi ndani na kutoa nje au ondoka mazingira yaliyosabisha wewe kuwa na hasira.
Kitu kimoja zaidi, hatua ya kwanza kabisa ya hasira ni tafsiri ambayo mtu anakuwa nayo kuhusu jambo au kitu.
Pale mtu anapoamini kwamba ameumizwa au kutendewa isivyo kawaida au sawa ndiyo hasira huanza kuwaka.
Kumbe basi, hasira inapamba moto pale mtu anapoamua alipe kisasi kwenye kile anaona siyo sawa. Na akifanya hivyo hasira zikiwa zimemtawala na hawezi tena kujidhibiti anajikuta anafanya mambo ambayo baadaye anakuja kuyajutia na kusema laiti ningelijua.
Kila la heri.
CIO, Mwl Deogratius Kessy
Asante sana kwa Elimu hii juu ya kukabiliana hasira ambayo matokeo yake mara nyingi ni kuishia hasara
LikeLike
Karibu sana Mr BEATUS ELIAS Rwitana.
LikeLike
Asante kwa somo hili zuri.
Nikiudhiwa nitachukua muda au kuondoka mahali niliposababishiwa hasira ili niweze kupata utulivu na kuepuka madhara ambayo ningeweza kuyasababisha kwa kufanya maamuzi ya kujibu kwenye yale makwazo.
LikeLike
Vizuri sana NOTBRUGA.
Kila la heri.
LikeLike
Hasira ni hisia hasi, hasira ni ukichaa wa muda kwa sababu unapokuwa na hasira huwezi kufikiri kwa usahihi. Na Mara zote hasira ni hasara
Jambo muhimu kufanya unapojikuta una hasira, dhibiti
hasira hizo kwa kujizuia na kutokuchukua hatua yeyote
Na ikiwezekana ondoka ktk mazingira yaliyokusababishia
hasira hizo
SHUKLANI SANA MWL KESS kwa Somo Bora kbs.
LikeLike
kweli kabisa . Hasira hasara
LikeLike
Tujitahadhari.
LikeLike
kutumia muda kutoa pumzi ndani na kutoa nje kwa dakika fulani inaleta kupunguza hasira pamoja kuondoka eneo lililo sababisha hasira kujitokeza hii ninaweza kushudia invyosaidia maana nimekutana na kisanga kikataka kutisa utulivu lkn kwa njia hizi nimeanza upya.
shukrani kocha kufanya tuwe na ukomavu ili kushinda ukichaa wa muda.
LikeLike