3035; Huwajibiki kumridhisha yeyote.

Rafiki yangu mpendwa,
Moja ya vitu vinavyotuchelewesha kufanikiwa kwenye maisha ni kujipa wajibu mwingi usiotuhusu.

Na moja ya wajibu tuliojipa ambao unatutesa bure ni kutaka kumridhisha kila mtu.
Huu ni wajibu unaotuchosha na usio na tija yoyote kwetu, kwa sababu hauna mchango kwetu kufikia mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumekuzwa tukiogopa kuingia kwenye matatizo na watu wengine.
Kuanzia kwa wazazi wetu, walimu, jamii na mamlaka mbalimbali.
Tunakazana kufuata kila utaratibu tunaoambiwa na kila ushauri tunaopewa ili tu tusiwavuruge wengine.

Unaweza kuyaendesha maisha yako kwa namna hiyo, ya kutaka kumridhisha kila mtu, lakini haitakuwa na manufaa kwako.
Kwanza bado siyo wote wataridhishwa na yale unayofanya.
Na zaidi utakuwa umejizuia wewe mwenyewe kufanya makubwa unayoyataka kwenye maisha yako.

Unahitaji kufika mahali na kuamua hutaendelea tena na hayo maisha ya kutaka kumridhisha kila mtu.
Amua kuyaishi maisha yako kwa uhuru, ukifanya yale ambayo ni muhimu kwa upande wako hata kama siyo yanayowafurahisha wengi.

Kama unachofanya hakivunji sheria mbalimbali zilizopo, hupaswi kukwamishwa kukifanya kwa sababu ya watu ambao hawatafurahishwa.
Kama kitu ni muhimu kwako na mafanikio yako unapaswa kukifanya, bila ya kujali watu gani utawavuruga kwa kufanya hivyo.

Kwenye haya maisha, kuna watu watachagua tu kukuchukia, bila ya kujali umefanya nini.
Hivyo kama lengo lako ni upendwe na kila mtu, tayari unakuwa umeshindwa kabla hata ya kuanza.
Hata ukifanya yote yanayowafurahisha wengine, bado kuna watu watachukizwa tu na unayofanya.

Unachopaswa kujua na ambacho kitakupa uhuru mkubwa kwenye safari yako ya mafanikio ni kwamba huhutaji ruhusa ya mtu yeyote ndiyo uyaendee mafanikio yako. Huhitaji kumridhisha yeyote ndiyo uweze kufanikiwa. Wala hulazimiki kumfurahisha kila mtu ndiyo ufanikiwe.

Unachohitaji ni wewe kuwa huru, kufanya vitu vya tofauti na kutoa thamani kubwa kwa wale wanaojali.
Chagua tatizo au hitaji ambalo watu wanalo, lifanyie kazi kwa kina na wape suluhisho la uhakika.
Hiyo inakupa fursa kubwa ya wewe kuweza kufikia mafanikio makubwa unayoyataka.

Kuna watu watachagua kutokukupenda au kukubaliana na wewe kwa sababu umechagua kuyaishi maisha yako.
Watu hao wangetamani sana kuwa huru kama wewe ila hawana ujasiri huo.
Na hivyo watakuchukia kwa kitendo cha wewe kuamua kuwa huru.
Wanatamani sana na wewe ungefanya mambo ya kawaida kama wao ili usiwe wa tofauti na kupata mafanikio makubwa kuliko wao.

Wengi watakufanya ujione una hatia kwa kuchagua kuyaishi maisha yako na kuachana na mazoea yaliyopo kwenye jamii inayokuzunguka.
Wangetaka sana uteseke kama wao kwa kufuata taratibu mbalimbali zilizopo ambazo hazina tija yoyote.
Lakini usikubali kamwe kunasa kwenye hizo hatia zao.

Kama hujamuumiza yeyote,
Kama hujavunja sheria zozote,
Na kama hujaenda kinyume na misingi yako binafsi,
Usikubali kuyumbishwa na matakwa ya wengine.
Huwajibiki kumridhisha na kumfurahisha kila mtu.
Unawajibika kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako na yatakayowagusa wengine kwa namna bora kabisa.

Wapo watakaosema wewe ni mbaya, hujali na una tamaa ya kujiridhisha mwenyewe.
Waache waamini hivyo na wewe endelea kupambana na mambo yako.
Kwa sababu hata ukijaribu kujieleza kwao, bado watatafuta namna ya kukuonyesha haupo sahihi.

Kilicho sahihi kwako kwenye haya maisha ni wewe kupata mafanikio unayoyataka.
Wapo wengi watakaojipa utakatifu wa kukosoa kila unachofanya na namna unaendesha mambo yako.
Wapo watakaojipa wajibu wa kukupa ushauri ambao hujawaomba.
Lakini unapaswa kuwapuuza.
Kwa sababu kwanza hawana mambo makubwa wanayohangaika nayo, wangekuwa nayo wasingepata muda wa kuhangaika na wewe.
Na pili, chochote wanachokushauri siyo sahihi, kwa sababu wanaona mambo ya nje tu, hakuna cha ndani wanachokiona au kukielewa.

Ingekuwa kuridhisha na kufurahisha kila mtu ndiyo kufanikiwa, watu wengi sana kwenye jamii zetu wangekuwa na mafanikio makubwa.
Maana wengi wana utiifu mkubwa wa kujaribu kuridhisha na kufurahisha kila mtu.
Lakini uhalisia ni kinyume kabisa na hilo.
Wale wanaokazana sana kuridhisha na kufurahisha kila mru ndiyo ambao hawana mafanikio kabisa.
Ndiyo wanaodharaulika na wengi zaidi kwenye jamii.

Kuna somo kubwa sana hapo,
Ili ufanikiwe, lazima uwe tayari kuwaudhi wengi.
Kwa maudhi hayo, wapo watakaokuchukia, lakini watakuheshimu sana.
Na wapo watakaokupenda na kukukubali kwa yale unayosimamia.
Na hao ndiyo unaowahitaji ili upate mafanikio makubwa unayoyataka.

Mtu mmoja amewahi kusema kama hakuna watu wanaokuchukia, basi jua pia hakuna watu wanaokupenda.
Ili upendwe kweli na aina fulani ya watu, lazima ukubali kuchukiwa na aina fulani ya watu.
Ni lazima uchague kwa makusudi kabisa watu ambao hutawaridhisha wala kuwafurahisha kwa kuchagua kuyaishi maisha yako.
Na hapo ndipo utawapata ambao wanakupenda kwa ujasiri ulioonyesha.

Mara zote kumbuka wajibu wako wa kwanza ni kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Mengine yote yasiyokuwa na mchango kwenye hilo unapaswa kuachana nayo mara moja.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe