3037; Uwajibikaji haukwepeki.

Rafiki yangu mpendwa,
Mafanikio ya aina yoyote ile kwenye maisha huwa yanaambatana na uwajibikaji.
Ni uwajibikaji wa hali ya juu sana ndiyo unaozalisha mafanikio makubwa ambayo watu wanayapata kwenye maisha yao.

Mafanikio pia yanategemea sana watu ambao mtu anaambatana nao.
Kwa sababu hakuna mtu anayeweza kufanya kila kitu peke yake, watu wanahitajika sana katika kukamilisha majukumu mbalimbali yanayozalisha mafanikio.

Sasa basi, kila panapohusika watu na uwajibikaji nao unahusika.
Unapaswa kuwawajibisha watu ambao unajihusisha nao kwenye kila eneo la maisha yako.

Kama utashindwa kuwawajibisha watu unaojihusisha nao, wewe ndiye unaishia kuwajibika kwa watu hao.
Utaishia kubeba mzigo mkubwa wa watu ambao watakuwa kikwazo kwako kufikia mafanikio unayoyataka.

Watu lazima wawajibishwe ili kutekeleza yale wanayopaswa kutekelezwa.
Uwajibikaji ndiyo unaowasukuma watu kuacha uvivu na uzembe na kufanya.

Kwa asili sisi binadamu ni wavivu na wazembe, hatufanyi kitu chochote mpaka pale inapokuwa kuna madhara kwa kutokukifanya.
Ndiyo maana watu husubiri mpaka tarehe za mwisho kuchukua hatua fulani wanazopaswa kuchukua.
Hiyo ina maana kama kusingekuwa na tarehe za mwisho, kuna wengi wasingefanya kabisa.

Hivyo ndivyo ilivyo kwenye uwajibikaji,
Kama huwezi kuwawajibisha watu unaojihusisha nao, hakuna kitakachowasukuma kufanya.
Na kama watu hawana msukumo wa kufanya, wanakuwa mzigo kwako.
Unaishia kuwajibika kubeba mzigo huo wa watu au hata kuachana nao.

Ndiyo maana tunasema uwajibikaji haukwepeki.
Ni uchague kuwawajibisha watu au uwajibike wewe mwenyewe.
Unawajibika kuwawajibisha watu au utawajibika wewe mwenyewe.

Hakuna uwajibikaji rahisi,
Kuwawajibisha watu kunakutaka uwasukume kutoka kwenye mazoea yao na wafanye vitu vya tofauti. Wengi hawatapenda hilo. Hivyo kama utataka kuwafurahisha, hutawawajibisha na hivyo yanayopaswa kufanywa hayatafanyika.

Kuwajibika wewe mwenyewe ni kazi mara mbili, ufanye kazi yako mwenyewe halafu ufanye na kazi ya wengine ambao umeshindwa kuwawajibisha.

Ni muhimu sana unaposhirikiana na watu wengine kukubaliana tangu awali ni mambo gani wanayopaswa kutekeleza.
Kisha wewe kuwawajibisha kwenye kutekeleza kama mlivyokubaliana, bila ya kupokea sababu zozote zile.

Uwajibikaji ndiyo unawaweka watu kwenye kile wanachopaswa kufanya.
La sivyo ni rahisi sana kuyumbishwa na mambo mengi mapya yanayokuwa yanajitokeza kila mara.

Wawajibishe au utaeajibika kwao.
Hakuna namna unaweza kukwepa uwajibikaji.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe