3038; Kuamua unachotaka.

Rafiki yangu mpendwa,
Hatua ya kwanza muhimu ya kufanikiwa kwenye maisha ni kuamua nini hasa unachotaka.
Hayo ni maelezo mafupi na rahisi kueleza, lakini ambayo utekelezaji wake ni mgumu sana.

Kuna kutaka na kuna kuamua.
Kila mtu kuna vitu vingi anavyokuwa anataka, vitu anavyotamani awe navyo au kuvifikia.
Halafu kuna kuamua nini hasa unachokuwa unataka.
Kuamua ni kuchagua kitu kimoja na kuachana na vingine vyote.
Ni kujitoa kwa kila kitu kwenye kitu kimoja unachokitaka hasa ili kuhakikisha unakipata.

Kitu kimoja ambacho watu wengi huwa hawakijui au kuelewa ni kwamba pale mtu anapoamua nini hasa anachotaka na kujitoa kwa kila namna kupata anachotaka, huwa anaishia kupata hicho anachokuwa anakitaka.

Watu wengi wanakosa kile wanachotaka siyo kwa sababu hawana uwezo wa kukipata, bali kwa sababu hawajaamua kweli kukipata.
Kushindwa kuamua ni kikwazo kinachowazuia wengi wasipate mafanikio makubwa.

Kushindwa kuamua ni kukosa imani na uvumilivu wa kutosha kwenye kitu kimoja.
Ni kuwa na tamaa ya kupata vitu haraka na kwa njia za mkato ambazo hazihusishi kazi.

Ukishajiona unahangaika na fursa nyingi kwa wakati mmoja, ni kiashiria kwamba hujaamua kwenye fursa moja.
Kwa maneno mengine ni unakuwa hujajua nini hasa unachotaka, ndiyo maana kila kinachopita mbele yako kinakuwa muhimu kwako.

Watu wengi kwenye maisha hawashindwi kupata wanachotaka, bali ni hawajui nini hasa wanachotaka.
Hawafanyi maamuzi ya kile wanachotaka hasa na kujitoa kwa kila namna kukipata.
Maamuzi yana nguvu kubwa sana, yanapunguza usumbufu na kupeleka umakini kwenye kitu kimoja.

Taarifa hii ya kuweza kupata chochote unachotaka kwa kuamua ilipaswa kuwa nzuri na kupendwa na kila anayetaka mafanikio makubwa.
Lakini imekuwa kinyume chake, imekuwa taarifa ya kutisha kwa wengi, kwa sababu inaondoa kichaka cha kujificha kwa wale ambao hawajajitoa hasa na hawapo tayari kuweka juhudi kubwa.

Watu wasiofanikiwa huwa hawapendi waonekane uzembe wao ndiyo umewazuia wasipatikane.
Kama watachagua kitu kimoja na kuachana na vingine, halafu wasifanikiwe kwenye kitu hicho, inakuwa imedhihirisha wazi kwamba ni wazembe.
Kuepuka hilo watu wanahangaika na mengi, ili wanaposhindwa wawe na sababu ya kwamba walitingwa na mengi.

Kama utaamua nini hasa unachotaka na kuamua kujitoa kwa kila namna kukipata, ni lazima utaishia kukipata.
Hakuna namna maamuzi na juhudi kubwa vinaweza kushindwa, hasa pale vinapopewa muda wa kutosha.

Maamuzi ni neno linalochukuliwa kikawaida sana, lakini ambalo ni zito na lenye maana kubwa.
Wengi hudhani maamuzi ni kutamka tu.
Ukweli ni maamuzi ni dhamira ya kweli kutoka ndani ya mtu ya kujitoa kwa kila namna kwenye kitu fulani.

Mafanikio yote makubwa huwa yanaanzia kwenye maamuzi makubwa, makali na yanayosimamiwa kwa uhakika.
Kama hujapata kile unachotaka, usianze kuangalia nani wa kumlaumu, bali angalia ni maamuzi gani ambayo bado wewe hujayafanya kwa uhakika.

Kuamua ndiyo mstari mwembamba sana unaotenganisha kutaka na kupata.
Wengi wanayataka mafanikio, lakini ni wachache sana wanaoyapata mafanikio wanayoyataka.
Na hayo yote yanaanzia kwenye kukosekana kwa maamuzi thabiti ya nini hasa mtu anachotaka kwenye maisha yako.

Tunaposoma hadithi za walioweza kufanya makubwa kwenye maisha yao, tunaona mahali walipofika na kufanya maamuzi ambayo ndiyo yaliyobadili kila kitu kwenye maisha yao.
Waliendelea kusimamia kile walichochagua licha ya kupingwa, kukataliwa, kukatishwa tamaa na hata kudhihakiwa.

Kama bado hujaamua nini hasa unachotaka na kuweza kukomaa nacho, una fursa kubwa ya kuweza kufanya hivyo sasa.
Ni vigumu kwa wengi kuamua kwa sababu wanaona kama watajinyima fursa nyingi nzuri zinazoweza kuja.
Lakini ukweli ni kuamua kunakupa fursa kubwa ndani ya kile ulichochagua, kwa sababu unaweka umakini wako wote hapo.

Amua kile hasa unachotaka na yasimamie maamuzi yako bila kuyumbishwa na chochote.
Utaishia kupata kile hasa unachokuwa umeamua kukipata.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe