3039; Gharama ya kulipa.

Rafiki yangu mpendwa,
Kila kitu kwenye maisha huwa kina gharama ambayo mtu anapaswa kulipa ili kukipata.
Gharama hiyo siyo tu kwenye fedha, bali pia kwenye kazi, muda, nguvu n.k.

Thamani ambayo watu wanakipa kitu, inaendana na gharama ambayo wamelipa kukipata.
Kama kitu kinapatikana kirahisi, watu wanakipa thamani ndogo na kutokukiheshimu kabisa.
Lakini kama kitu kimepatikana kwa ugumu, watu wanakipa thamani kubwa na kukiheshimu sana.

Mfano mzuri ni kwenye eneo la fedha.
Watu wakipata fedha kwa urahisi, bila ya kuweka juhudi kubwa, huwa hawaiheshimu, hivyo wanaishia kuitumia hovyo na kupoteza yote.
Lakini mtu anapokuwa ameweka juhudi kubwa kuipata fedha, anaiheshimu sana na kuitumia kwa umakini mkubwa.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye kuwa ndani ya kundi fulani.
Kama kujiunga na kundi lolote lile ni rahisi, yaani hakuna ada ya kulipa au ada ni ndogo na hakuna wajibu mkubwa mtu anaokuwa amepewa, watu wengi hujiunga, lakini hawaheshimu wala kuthamini kuwa ndani ya kundi hilo.
Wanajifanyia vile wanavyotaka wao wenyewe bila kujali taratibu za kundi hilo, kwa sababu hawaoni hatari yoyote kama watapoteza nafasi waliyopata.

Kwa kifupi, masharti ya kujiunga na kundi fulani yanapokuwa madogo, kila mtu anakuwa na sifa ya kujiunga. Hivyo hata wale ambao hawajajitoa kweli nao wanapata nafasi ya kujiunga.
Mwishowe wanakuwa mzigo kwenye kundi, kwani wanakuwa hawafuati taratibu zilizopo kwenye kundi na mwishowe kundi zima linakosa maana.

Makundi ambayo yanapata watu bora na kudumu sana ni yale yanayokuwa na gharama kubwa ya mtu kulipa ili kuwa ndani yake.
Na siyo gharama tu kwa fedha, bali kwa vigezo na masharti na wajibu ambao mtu anakuwa amepewa kwenye kundi husika.
Kadiri uwajibikaji kwenye kundi unavyokuwa mkubwa, ndivyo wachache wanavyoweza kupata sifa na ndivyo wanavyojitoa kweli ili waendelee kubaki kwenye kundi.
Hiyo inaliimarisha sana kundi na kuliwezesha kudumu na kila mtu kufanikiwa sana.

Makundi yanayokuwa rahisi kujiunga ili kupata watu wengi, yanaishia kuzoa kila mtu. Wengi wanaojiunga wanakuwa hawapo tayari kujitoa kwa jambo lolote kubwa, hivyo kundi linakosa maana na maisha yake kuwa mafupi.

Ugumu wa kujiunga na kundi fulani unawachuja wale kweli waliojitoa na ambao wapo tayari kulipa gharama kubwa inayohitajika ili kuwa ndani ya kundi husika.
Kadiri wanavyolipa gharama kubwa, hasa kwenye kuwajibika, ndivyo wanavyojitoa zaidi kwa ajili ya kundi na hivyo kulipa kundi nguvu kubwa zaidi.

Gharama nyingine kubwa ya kujiunga na kundi lolote lile ni kuacha ubinafsi na kujali maslahi mapana ya kundi.
Kundi linalodumu na kufanikiwa ni lile ambalo watu waliopo ndani yake wanafanya mambo siyo kwa ajili yao binafsi, bali kwa ajili ya kundi.
Wanafanya vitu hata kama kwao wenyewe hawataki, ila kama vina manufaa kwa kundi au ndiyo mahitaji ya kundi basi wanakamilisha.

Kadiri vigezo vya kujiunga na kundi vinapokuwa juu na adhabu ya kutotimiza vigezo kuwa kali, ndivyo wanaojiunga wanavyokuwa bora na kutimiza vigezo hivyo. Hayo yote yanachangia kwenye uhai na mafanikio ya kundi.
Wanaoingia gharama kubwa kuingia na kubaki kwenye kundi wanakuwa waaminifu sana kwenye kundi na kujitoa kweli.
Wanaoingia kirahisi huwa siyo waaminifu, hawajali wala kujitoa.

Kadiri inavyokuwa vigumu kujiunga na kundi fulani, ndivyo wachache tu na waliojitoa kweli wanapata nafasi ya kujiunga na ndivyo maisha na mafanikio ya kundi yanavyokuwa makubwa.
Ukiangalia mifano iko dhahiri kabisa.
Timu bora kabisa za michezo yoyote ile ni zile ambazo zinachagua wachezaji kwa vigezo vya juu na kuwaweka kwenye mazoezi makali. Timu za hovyo zinazoa yeyote anayepatikana na hazina mazoezi makali.

Kadhalika majeshi imara ni yale ambayo yana vigezo na masharti makali ya kujiunga, huku mafunzo yakiwa makali sana. Kwa hatua hizo wengi wanakosa sifa za kujiunga na hivyo wanaopata nafasi na kubaki kwenye jeshi ni wale waliojitoa kweli kweli. Kwa njia hiyo jeshi linapata watu bora na kuwa imara sana.

Kama mpaka sasa hujaelewa ninachojaribu kukufafanulia hapa ni dira na mwelekeo wa KISIMA CHA MAARIFA na BILIONEA MAFUNZONI.
Kama kundi, uhai na mafanikio yetu yanategemea sana ubora wa watu walio ndani yake.
Na ili watu wawe bora, lazima masharti na vigezo vya kuwa mwanachama viwe vya juu sana.
Pale watu wengi wanapoweza kumudu masharti na vigezo hivyo, inakuwa rahisi kujiunga na watu wanaopatikana wanakuwa siyo bora.

Hivyo basi, tutaendelea kusimamia vigezo na masharti ya kuwa mwanachama wa kundi hili.
Hakutakuwa na kulegeza kwa aina yoyote ile.
Kuwa na vigezo na masharti ya juu kutawapoteza wengi ambao hawajajitoa kweli kuwa ndani ya kundi.
Lakini ni watu wanaopaswa kupotea ili kundi liweze kudumu.

Gharama kubwa sana ya kulipa ili kuwa kwenye kundi hili ni kukaa kwenye mchakato kwa asilimia 100 na kwa msimamo wa hali ya juu bila kuyumba.
Kama hilo linakushinda, hakuna namna utatoboa ndani ya kundi hili.

Unaweza kuwa unatamani sana kuwa na kuendelea kubaki ndani ya kundi hili, lakini ikawa huna tu bahati ya kuwepo, kwa sababu ya kuwa na vikwazo vingi vinavyokuzuia kukaa kwenye mchakato.
Labda tu huwezi kuamka asubuhi na mapema kila siku kushiriki kipindi cha #AmkaNaBM.
Hapo inakuwa hakuna namna, asili inakuwa imekutenga na kundi hili.
Au huna biashara unayoijenga kwa mchakato wa kundi hili, au huwezi kuweka fokasi kwenye biashara kama kundi linavyokutaka.

Na kubwa zaidi ni kama huwezi kuliamini kundi kwa njia ya klabu na kushirikiana nalo kwa undani kwenye safari yako ya mafanikio.
Kama unajali maslahi yako zaidi kuliko ya klabu, kama huwezi kushiriki mikutano kwa sababu inaingilia mambo yako, kama huwezi kushirikiana na wengine kwenye klabu ili kukuza biashara za wote.

Mambo ni mengi na yanaeleweka, lakini kikubwa ni gharama ya kulipa kwenye mchakato ili uendelee kubaki kwenye kundi.

Naweka maisha yangu yote kwenye kujenga hii jamii ya tofauti na ninataka iwe na maisha marefu sana kuliko hata mimi mwenyewe.
Hivyo zoezi la kuwaondoa wote ambao hawajajitoa kweli, wote ambao hawakai kwenye mchakato na kuweka kipaumbele kwenye jamii hii litakuwa endelevu.

Ni lazima ujitoe hasa ndiyo uweze kubaki kwenye jamii hii.
Milango ya kutoka ni rahisi mno, ni usikae tu kwenye mchakato.
Milango ya kuingia ni migumu mno, hasa ukiwa umeshaingia na kutoka.
Itakuwa rahisi sana kwako kuingia ikulu na kwenda kumwona raisi wa nchi, kuliko kuingia ndani ya hii jamii baada ya kuwa umepata nafasi na kuipoteza.
Naamini bila ya shaka yoyote ile hicho ndiyo kitakuwa kipimo sahihi cha kama jamii hii itafanikiwa au la, namna watu wanavyong’ang’ana kuipata nafasi na kubaki ndani yake.

Kama kila mtu anaweza kujiamulia kuingia na kutoka vile anavyotaka yeye, hakuna jamii tutakayokuwa tunajenga hapa. Kitakuwa tu ni kama kijiwe ambapo watu wanakutana bila ya lengo lolote maalumu, wanaenda tu kupiga soga kusogeza muda.
Hilo sitaliruhusu ndani ya jamii hii tunayojenga.
Kutakuwa na gharama kubwa sana ya kulipa kwenye mchakato, ambayo kama hujajitoa kweli utaomba poo.
Utaomba ukapumzike kidogo kwanza halafu utarudi.
Na hapo ndipo milango itakapojifunga milele.
Utalia machozi ya damu na hakuna mlango utakaofunguka kwako.

Itakuwa rahisi kwako kutubu na kusamehewa dhambi ya kuua na kuruhusiwa kuuoka ufalme wa mbinguni.
Lakini itakuwa vigumu mno kwako, yaani haitawezekana tena kuipata nafasi kwenye jamii hii baada ya kuwa umeusaliti mchakato.
Hili linasimama sawa kwa wote bila ya upendeleo wowote ule.

Ni imani yangu hili limeeleweka vyema kabisa na kila mmoja wetu atakaa mahali pake ili tuweze kujenga jamii hii ya tofauti.
Gharama zake haziwezi kuwa rahisi, lazima uzilipe kwa ukamilifu kwa kukaa kwenye mchakato.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe