Mazoezi 10 Ya Falsafa Ya Ustoa Yatakayofanya Uwe Na Maisha Bora.

Habari Mstoa Mwenzangu,
Karibu kwenye mwendelezo wa mafunzo yetu ya falsafa ya Ustoa, mafunzo ambayo ni ya kutuwezesha kuchukua hatua ili kuwa na maisha bora.

Hapa tunakwenda kujifunza mazoezi kumi ya Falsafa ya Ustoa, ambayo tukiyafanya kuwa sehemu ya maisha yetu tutaweza kujenga maisha bora sana.

Karibu tujifunze na kuchukua hatua kwenye haya tunayojifunza.

Moja; Tafakari ya asubuhi.

Kabla hujaianza siku yako, tenga muda wa kujitafakari, ukiyatafakari maisha yako na siku iliyo mbele yako.
Kuna mambo manne ya kufanya wakati wa tafakari ya asubuhi;
1. Shukuru kwa siku mpya uliyoiona, siyo wote wameweza kuamka wakiwa hai au wakiwa na afya kama wewe.
2. Panga jinsi utakavyoyaishi maadili ya Ustoa kwenye siku yako, yaani Hekima, Haki, Ujasiri na Nidhamu.
Angalia ni mambo gani utakayoyafanya kwenye siku yako ili kuimarisha maadili hayo.
3. Jikumbushe kwamba kuna vitu viko ndani ya uwezo wako na vingine nje ya uwezo wako. Vilivyo ndani ya uwezo wako ni fikra zako na matendo yako, dhibiti hivyo, vingine vyote achana navyo.
4. Jitathmini maeneo unayohitaji kuendelea kujiboresha kwenye maisha yako ili kuwa na maisha bora.

Mbili; Kuwa na mtazamo wa juu.

Ukiwa ndani ya msitu, utaiona miti ni mikubwa. Ukiwa juu zaidi ya msitu utaiona miti ikiwa midogo.
Kitu chochote tunaweza kukiona ni kikubwa sana tunapokiangalia kwa karibu, lakini tukikiangalia kwa juu, kwa mbali, kinakuwa kidogo sana.
Kufanya zoezi hili kaa eneo tulivu na fumba macho yako. Jione ukipanda juu ya anga na kuiangalia dunia kwa chini.
Kama umewahi kuona picha ya anga ilionyesha dunia, inaonekana ikiwa ndogo sana.
Jua ndivyo mambo yote yanayokusumbua hapa duniani yalivyo madogo, usiyape sana uzito.

Tatu; Kuwa na mtu wa mfano na jipime naye.

Kuna watu ambao wameweza kufanya makubwa sana hapa duniani. Japo hawakuwa wamekamilika, waliweza kuacha alama kubwa ambayo mpaka leo inakumbukwa.
Wanaweza kuwa hai au wamekufa.
Chagua mtu wa mfano kwako (role model) kisha jipime naye kwa kila hatua unayopiga.
Lengo siyo kuwa kama yeye, bali kujisukuma kuwa bora zaidi.
Kuwa huru kuchagua yeyote unayemkubali sana, au hata kuwa na watu tofauti kwenye maeneo tofauti ya maisha yako.
Kwa kila unachofanya, jiulize mtu wa mfano kwako angefanyaje.
Kwa kuendelea kujifunza kuhusu mtu wako wa mfano, utaona fursa za kujisukuma na kuwa bora zaidi.

Nne; Wasaidie wengine.

Falsafa ya Ustoa inaamini binadamu wote ni ndugu moja, raia wa nchi moja ambayo ni ulimwengu.
Tupo hapa duniani ili kushirikiana kila mmoja kuwa na maisha bora.
Hivyo badala ya kujiangalia tu wewe nini unataka, angalia pia nini unawapa wengine.
Kadiri unavyowapa wengi zaidi yale wanayotaka, ndivyo na wewe unavyopata zaidi kile unachotaka.

Tano; Fanya safari ya mapumziko kiakili.

Watu wengi wamezoea kwamba ili kupata mapunziko na kubadili mazingira, lazima wasafiri kwenye tofauti na walipozoea.
Hilo ni zuri katika kubadili mazingira na hata fikra.
Lakini huhitaji kusubiri mpaka usafiri ndiyo upate mapumziko ya kiakili.
Unaweza kufanya safari ya mapumziko kiakili ukiwa hapo hapo ulipo.
Unachofanya ni kufumba macho yako na kupitisha kwenye fikra zako mazingira ya tofauti na pale ulipo.
Kwa njia hii unakuwa na udhibiti wa mtazamo wako bila kujali eneo gani upo.

Sita; Andika.

Kuandika ni sawa kuyapakua mawazo uliyonayo kwenye akili yako na kuyahifadhi ili usiyapoteze.
Kuandika pia kunakusaidia kupangilia vizuri mawazo yako.
Uandishi unasaidia pia kupunguza msongo wa mawazo.
Kila siku tenga muda ambapo utayaandika mawazo yaliyo kwenye akili yako na tafakari unazofanya.
Uandishi huu siyo kwa ajili ya wengine, bali kwa ajili yako binafsi.

Saba; Zama ndani.

Mambo mengi kwenye maisha ni kama kitunguu, kuna maganda mengi kwa nje kabla ya kufika kwenye kina.
Watu wengi wanapotezwa na maganda ya nje, mwonekano wa juu juu tu wa kitu na kuishia kufanya maamuzi ambayo siyo sahihi.
Mara zote zama ndani kwenye jambo lolote lile, usikimbilie kufanya maamuzi kwa mwonekano wa nje au taarifa za juu juu. Chimba kwa undani ili uweze kuujua ukweli na kufanya maamuzi sahihi yatakayofanya uwe na maisha bora.

Nane; Tafakari ya kulala.

Kabla ya kuimaliza siku yako na kulala, fanya tafakari ya jinsi siku yako nzima ilivyoenda.
Kwenye tafakari yako jiulize na kujijitu maswali haya;
1. Je nimeishi kulingana na maadili ya Ustoa leo?
2. Je nimewatendea wema watu wote niliojihusisha nao leo?
3. Ni madhaifu gani nimeweza kuyashinda leo?
4. Nimejisukumaje kuwa mtu bora zaidi leo?
5. Mambo gani ya kwenda kufanya kwa ubora zaidi kesho?
Kwa kufanya tafakari hii ya mwisho wa siku utaweza kuona yapi umefanya vizuri na yapi unahitaji kuyaboresha zaidi siku inayofuata, kitu kinachofanya uendelee kuwa bora.

Tisa; Taswira hasi.

Binadamu huwa tunavizoea vitu tulivyonavyo na kuvichukulia poa.
Ni mpaka pale tunapovipoteza ndiyo tunaona umuhimu wake na kutamani tungeweza kuwa navyo tena, kitu ambacho hakiwezekani.
Kuondokana na hali hii ya mazoea kwenye tulivyonavyo, fanya zoezi la taswira hasi.
Kwa zoezi hili unapata picha kila kitu ulichonacho umekipoteza na unaanza upya kabisa. Watu wako wa karibu wote wamekufa, mali zote umepoteza, kazi umefukubwa na biashara umefunga.
Jaribu kuyaishi maisha yako bila ya vitu ulivyozoea na utapata mafunzo makubwa mawili;
1. Utavithamini sana vitu ulivyonavyo.
2. Utakapovikosa hutaumia sana, kwa sababu ulishapata taswira ya kutokuwa navyo.

Kumi; Utese mwili kujenga nidhamu.

Wakati zoezi la taswira hasi likiwa ka fikra, kuna upande wake wa pili ambao ni zoezi la kuutesa mwili ili kujenga na kuimarisha nidhamu yako binafsi.
Kwenye zoezi hili unaunyima mwili wako vitu ambavyo umeshazoea na unavyo. Kwa kujinyima vitu hivyo kwa muda, unaufundisha mwili kutii akili na kutokuendeshwa na tamaa za mwili.
Lakini pia zoezi hili linauandaa mwili, ili pale unapokutana na hali ya kukosa vitu ulivyozoea usiumie sana.
Baadhi ya mambo unayoweza kufanya kwenye zoezi hili ni kama yafuatayo;
1. Kufunga kwa kutokula kwa siku nzima, licha ya kuwa na chakula.
2. Kula chakula cha hadhi ya chini kwa muda fulani japo unaweza kumudu chakula cha hadhi ya juu.
3. Kuogea maji ya baridi wakati wa baridi kali wakati unaweza kupata maji ya moto.
4. Kulala chini kwenye sakafu wakati una kitanda na godoro.
5. Kutembea kwa mguu sehemu ambayo umezoea kwenda na gari.
Ufanye mwili wako ujue unaweza kupoteza kila kitu na bado maisha yakaendelea.

Yafanye mazoezi haya kumi ya Ustoa kuwa sehemu ya maisha yako ya kila siku utaweza kuwa imara kiakili na kimwili, ukakabili yaliyo ndani ya uwezo wako na kuwa na maisha bora.
Usikubali kuendelea kuishi maisha yako kwa mazoea, ishi kwa misingi na mazoezi haya ya Ustoa ili kuyafanya maisha yako kuwa bora bila ya kujali nini kinachokuwa kinaendelea.

Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr. Makirita Amani.