3056; Unajivuruga mwenyewe.

Rafiki yangu mpendwa,
Kutokana na ugumu na changamoto za safari ya mafanikio, watu wengi huwa wanatafuta watu wa kuwapelekea lawama pale mambo yao yanavyokwenda tofauti na matarajio.

Hapo watu huona wazi kwamba wamevurugwa na wengine ambao wamefanya tofauti na walivyotarajia.

Lakini huo siyo ukweli, hakuna mtu yeyote yule anayekuvuruga kwenye mambo yako.
Ukweli ni kwamba inajivuruga wewe mwenyewe.

Na unajivuruga kwa matarajio makubwa unayokuwa nayo, ambayo hayaendani na uhalisia.

Ni vigumu sana kumvuruga mtu ambaye anaupokea uhalisia kama ulivyo na kuutumia kuboresha safari yake ya mafanikio.

Watu wa aina hiyo hawalazimishi dunia iende kama wanavyotaka wao, bali wanaenda na dunia vile inavyokwenda na kubadilika kulingana na matokeo yanayopatikana.

Watu imara kwenye safari ya mafanikio ni wale wanaoichukulia safari yao kama wajibu wao wa msingi.
Wanajua kama watafanikiwa au kushindwa hayo yote ni juu yao wenyewe.

Watu wanajivuruga sana wao wenyewe na kujizuia kufanikiwa kwa kutaka dunia iende kama wanavyotaka wao.
Pale mambo yanapokwenda tofauti na matarajio, watu hao huona kama wamesalitiwa.

Wanachokuwa wamesahau ni jinsi ambavyo mambo mengi wanayofanya yapo nje ya udhibiti wao.

Chukua mfano mtu amekutukana au kukuibia. Kwa haraka haraka unaweza kuona mtu huyo amekuonea.
Lakini huo siyo ukweli. Ukweli ni kwamba mtu huyo anakuwa amekuonyesha uhalisia wake.

Sasa wewe kumlaumu mtu kwa kukuonyesha uhalisia wake ni sawa na kumlaumu mbwa kwa kubweka. Mbwa huwa wanabweka, ndiyo asili yao.
Kadhalika, wezi huwa wanaiba na wasiojali huwa wanatukana.
Badala ya kumlaumu mtu kwa kuona amekuvuruga, unapaswa kufurahia, kwa sababu amekuonyesha uhalisia wake.
Tangu hapo, utakuwa unaenda naye kwa tahadhari.

Nirudie kwa msisitizo, ni vigumu sana kumvuruga au kumkwamisha mtu ambaye anapokea uhalisia kama ulivyo badala ya kutaka uhalisia uwe vile wanavyotaka wao.
Kwa maneno mengine, ukitaka utulivu (na furaha) kuwa na mategemeo madogo sana kwa wengine au vitu vingine vilivyo njie ya uwezo wao.

Hawakazani kutaka mambo yawe rahisi kama wanavyotaka wao, badala yake wanakazana kuwa imara ili waweze kukabiliana na ugumu wowote wanaoweza kukutana nao.

Nguvu ya kweli kwenye maisha ni zao la kupokea uhalisia kama ulivyo. Ni kuwa imara na kutokuyumbishwa na chochote kile kinachotokea, hata kiwe kizuri au kibaya kiasi gani.
Kukubali uhalisia ndiyo hatua ya kwanza na muhimu kwenye safari ya mafanikio.

Somo kubwa sana tunaloondoka nalo hapa ni kuchagua kuyaishi maisha yako, kujitoa kwa kila namna kwenye kufanya kazi na kuyapokea matokeo kama yanavyokuja kwako kisha kuboresha zaidi.
Kama hulazimishi mambo yaende kama unavyotaka wewe, hakuna kitakachoweza kukuangusha au kukuvuruga.

Kukubali na kupokea uhalisia kama ulivyo haimaanishi kukata tamaa na kuona hakuna unachoweza kufanya.
Badala yake inamaanisha uwezo wako ni wa juu sana kiasi cha kuweza kutumia kila aina ya matokeo unayoyapata kuboresha zaidi safari yako ya mafanikio.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe