Barua ya III; Urafiki wa kweli na wa uongo.
Rafiki yangu Mstoa,
Kuna watu ambao huwa tunawachagua wawe karibu yetu kwenye maisha.
Watu hao, hatulazimiki kuwa nao kama ilivyo kwa ndugu, bali tunakuwa tumechagua kwa hiari yetu wenyewe kuwa karibu nao.
Watu hao ni marafiki.
Marafiki ni watu muhimu sana kwenye maisha yetu.
Ni watu ambao wanaweza kutuelewa bila ya kutuhukumu.
Ni watu ambao wanaweza kutusikiliza pale tunapotaka kusikilizwa.
Lakini pia ni watu ambao wanaweza kutushauri vizuri pale tunapohitaji ushauri.
Hivyo ndivyo urafiki unavyopaswa kuwa, wenye manufaa kwa pande zote mbili na watu kukua pamoja.
Lakini kwenye uhalisia sivyo urafiki wa watu wengi ulivyo.
Urafiki wa watu wengi umekuwa wa kimaslahi zaidi, kitu ambacho kinaleta hali ya kutokuaminiana baina ya marafiki.
Unakuta mtu ana rafiki, lakini hayupo tayari kumshirikisha mambo yake muhimu.
Hilo ni tatizo kubwa kwenye urafiki, ambalo siyo geni, kwani limekuwepo tangu enzi na enzi.
Kwenye barua yake ya tatu kwenda kwa rafiki yake Lucilius, Mstoa Seneca anamjibu alivyomwandikia kuhusu rafiki yake mwingine.
Lucilius alikuwa amemweleza Senaca jambo kuhusu rafiki yake mwingine, lakini akamtahadharisha asimwambie rafiki huyo.
Hapo ndipo Seneca anaposhangazwa kwamba anamwitaje mtu rafiki yake kama hawezi kumwamini na kumwambia mambo yake muhimu?
Kwenye barua hii, Seneca anashirikisha mambo muhimu sana ya kuzingatia kuhusu kujenga urafiki wa kweli.
Kwa kuwa wote tunahitaji kujenga urafiki imara, tunapaswa kujifunza mambo haya na kuyazingatia.
1. Mwamini rafiki yako kama unavyojiamini wewe mwenyewe.
Seneca anaeleza kwamba msingi mkuu wa urafiki ni kuaminiana.
Unaposema mtu ni rafiki yako, kwa maana kwamba umechagua mwenyewe na siyo kulazimishwa, basi unapaswa kumwamini kama unavyojiamini wewe mwenyewe.
Kama kuna mambo yako ambayo huwezi kumwambia yule unayesema ni rafiki yako, basi huo siyo urafiki.
Badala yake unatumia tu neno urafiki kama unavyoita watu wengine.
Urafiki wa kweli ni ule unaojengwa kwenye msingi wa kuaminiana bila ya shaka yoyote.
Hatua ya kuchukua;
Waangalie wale wote unaowaita marafiki zako, kisha jiulize je upo tayari kuwaambia kila kitu kuhusu wewe? Kama kuna ambao unaona huwezi kuwaambia mambo yako ya ndani, jua hao siyo marafiki zako wa kweli.
Jenga marafiki wa kweli ambao utawaamini na kuwa tayari kuwashirikisha mambo yako yote.
Nukuu;
“But if you consider any man a friend whom you do not trust as you trust yourself, you are mightily mistaken and you do not sufficiently understand what true friendship means.” – Seneca
“Kama unamchukulia mtu kama rafiki yako, lakini humwamini kama unavyojiamini mwenyewe, unakosea na huelewi maana halisi ya urafiki wa kweli.” – Seneca
2. Kabla ya urafiki hukumu, baada ya urafiki amini.
Kinachowafanya watu wengi washindwe kuwaamini wale wanaowaita marafiki zao ni kwa sababu wamejenga nao urafiki kwa haraka sana.
Watu wengi wanakutana na mtu mahali, wanaona wanaendana kwa yale wanayopendelea na hapo urafiki unakuwa umejengeka.
Kwa kuwa urafiki huo umejengwa haraka, wanakuwa hawajajuana kwa undani, hivyo wanashindwa kuwa wawazi kwa kila mmoja.
Kinachofuata kinakuwa kipindi cha kuchunguzana ndiyo waaminiane. Sasa kwa sababu urafiki umeshaanza, kuchunguzana kunakosa nguvu kwa sababu mtu hawezi tena kuuona uhalisia, hisia za urafiki zinakuwa zimeshaingia.
Seneca anasema hivyo ni kinyume na urafiki unavyopaswa kujengwa. Kuchunguzana kunapaswa kuanza kabla ya urafiki kujengeka. Na urafiki ukishajengeka kinachohitajika ni kuaminiana.
Seneca anaendelea kueleza kwamba unapaswa kuchukua muda mrefu kutafakari kama mtu anafaa kuwa rafiki yako. Na ukishakubali kwamba anakufaa, basi unapaswa kumpokea kwa moyo wako wote.
Hatua ya kuchukua;
Wachunguze watu kwa kina kabla hujawakubali kuwa marafiki zako. Na ukishajidhihirishia kwamba wana vigezo unavyoangalia kwenye urafiki, wapokee na kuwaamini.
Nukuu;
“When friendship is settled, you must trust; before friendship is formed, you must pass judgment.” – Seneca
“Baada ya urafiki kujengeka, unapaswa kuamini; kabla ya urafiki kujengeka, unapaswa kuhukumu.” – Seneca
3. Usiwafundishe marafiki zako vibaya.
Jinsi marafiki zetu wanakuwa kwetu, ndivyo tunavyokuwa tumewafundisha sisi wenyewe.
Yaani marafiki zetu wanatupa kile ambacho tunategemea watupe.
Hiyo ina maana kwamba kama tunataka marafiki zetu watupe vitu vyenye manufaa kwetu, tunapaswa kuwafundisha hivyo.
Seneca anasema kama unaonyesha hali ya kutokuwaamini marafiki zako, hawatakuamini pia.
Na kama unakuwa na wasiwasi kwamba wanakudanganya, wanakudanganya kweli.
Hakuna kitu ambacho watu wanaweza kufanya kwako kama wewe mwenyewe hujawafundisha na kuwaruhusu.
Unapokuwa na marafiki zako wa kweli, unapaswa kuwaamini na kuwashirikisha mambo yote ya msingi, hasa yale unayohofia.
Marafiki wanakuwa vile unavyowategemea wawe.
Hatua ya kuchukua;
Chagua marafiki sahihi na wa kweli kisha wachukulie vile unavyotaka wawe na watakuwa hivyo.
Kwa kuwa watakuwa wanathamini urafiki wako, hawatataka kukuangusha, hivyo wataenda na wewe vile unavyowategemea.
Nukuu;
“Some, for example, fearing to be deceived, have taught men to deceive; by their suspicions they have given their friend the right to do wrong.” – Seneca
“Wanaoogopa kudanganywa, wanawafundisha watu jinsi ya kuwadanganya; wanaowatuhumu rafiki zao wanawapa nafasi ya kuwakosea.” – Seneca
4. Uwazi na usiri.
Kuna watu ambao ni wa wazi kupitiliza, wanaweka mambo yao wazi kwa kila mtu. Halafu kuna watu ambao ni wasiri kupitiliza, ambao hawaelezi mambo yao kwa mtu yeyote yule.
Seneca anasema wote hao wanakosea, hupaswi kuweka mambo yako wazi kwa kila mtu na pia hupaswi kufanya mambo yako siri kwako mwenyewe.
Seneca anatuambia tunapaswa kueleza mambo yetu kwa watu wachache na siri zetu kwa marafiki wetu wa karibu.
Hiki ni kitu ambacho watu kwa zama hizi wamekisahau kabisa na kimekuwa chanzo cha magonjwa ya akili ambayo yanawasumbua watu wengi kwa sasa, kama msongo na sonona.
Mitandao ya kijamii imewafanya watu kuanika maisha yao yote kwenye mitandao hiyo, kitu kinachowafanya wajilinganishe na wengine na kujiona wapo nyuma na hivyo kupata sonona.
Wengine wanaamua kuweka siri zao zote ndani yao, wasiwe na mtu yeyote wa kumcheulia, kitu kinachojenga msongo mkubwa ndani yake.
Kila mtu anahitaji kuwa na mtu anayemwamini na kumweleza mambo yake. Maana mambo yakikaa ndani ya mtu yanajengeka na kuleta msongo. Lakini yakizungumzwa, hata kama hayatapatiwa majibu, inaleta ahueni.
Kazi kubwa wanayofanya wataalamu wa kisaikolojia ni kuwasikiliza watu bila kuwahukumu, na hilo hutatua matatizo mengi ya watu.
Hatua ya kuchukua;
Usiweke mambo yako wazi kwa kila mtu, wengi hawana cha kukusaidia na kama ni matatizo watafurahia unayo.
Lakini pia usiwe na siri unazoweka ndani yako mwenyewe, waeleze marafiki zako wa kweli, ambao hawatakuhukumu kwa namna yoyote ile, hilo litatua mzigo mkubwa kwako.
Nukuu;
“It is equally faulty to trust everyone and to trust no one.” – Seneca
“Ni makosa kumwamini kila mtu kama ilivyo makosa kutokumwamini yeyote.” – Seneca
5. Kuwa na kiasi.
Pale mtu anapojikuta yupo upande mmoja na unampa changamoto, huwa anahamia upande wa pili kabisa.
Kwa mfano kama mtu amegundua ni muwazi sana na hilo linamwathiri, anabadilika na kuwa msiri kabisa.
Na kama mtu amekuwa msiri na kuona hilo lina athari kwake, anabadilika na kuwa muwazi sana.
Seneca anatuambia mabadiliko ya aina hiyo siyo sahihi.
Kuwa muwazi kabisa siyo sahihi na pia kuwa msiri kabisa siyo sahihi.
Tunapaswa kuwa na kiasi kwenye uwazi na usiri. Tusiweke mambo yetu wazi kwa kila mtu, lakini pia tusiwe na siri ambazo hatuwezi kumwambia mtu yeyote.
Hatua ya kuchukua;
Huwa inashauriwa mambo matatu usiyaweke wazi kwa kila mtu; utajiri,afya na mahusiano. Unaweza kuongeza mengine ili kuleta utulivu kwenye maisha yako. Ila kuwa na marafiki wachache ambao unawaamini na utawashirikisha hayo ya msingi kabisa kwako.
Nukuu;
“No, men should combine these tendencies, and he who reposes should act and he who acts should take repose.” – Seneca
“Hakuna mtu anayepaswa kuwa kwenye upande mmoja, mwenye uwazi anapaswa kuwa na usiri pia na mwenye usiri kuwa na uwazi kwa watu wake wa karibu.” – Seneca
Rafiki yangu Mstoa, tumejifunza mambo mazito hapa kuhusu urafiki wa kweli na wa uongo.
Tukijitafakari kweli, wengi tunaowaita marafiki siyo marafiki zetu wa kweli, maana hatuwezi kuwaamini na kuwaambia kila kitu chetu.
Tunaishi kwenye zama zenye usaliti mkubwa, unaweza kumweleza mtu mambo yako wakati mpo marafiki, lakini mnapokosana anayatumia mambo hayo kukuadhibu.
Hilo limekuwa linatufanya tuwe na tahadhari kubwa, tusiwe tayari kueleza mambo yetu ya ndani kwa marafiki zetu.
Lakini kubaki na mambo hayo inatuumiza sana, maana yanajenga msongo mkubwa ndani yetu.
Hivyo hatuna budi bali kuweka kazi na kujenga marafiki wa kweli.
Tuwaangalie watu wote wanaotuzunguka, tuwachunguze kwa kina na pale tunapojidhihirisha kwamba wana vigezo tunavyotaka ili wawe marafiki zetu, basi tunawaamini na kuwa wawazi kwao.
Hili halitaki tuwe na haraka, tunapaswa kwenda nalo kwa umakini, kwani tukikosea madhara yake ni makubwa.
Tuchukue muda wetu kujenga marafiki wa kweli ili tuweze kujenga maisha ambayo tunayafurahia.
Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr Makirita Amani.
Asante sana mstoa Makirita.
Kwenye maisha tunahitaji marafiki tunaoaminiana.
kuna hiki jambo mtu anasema usianike/kuwambia watu mambo yako hayo watu si wazuri wakitaka kuzuia mambo yako.Kana kwamba kuna ushirikina unazungumzia aje na unaamini kwamba watu wakijua mpango wako mapema ni mbaya kiimani??
LikeLike
Sawa. Vizur sana
LikeLike
Karibu.
LikeLike
Hapo siyo kiimani, bali fitna tu.
Kuna watu wakijua moves zako wanaenda kukublock, hata kama hilo haliwanufaishi moja kwa moja.
LikeLike
Sawa kabisa ila kama hawana access kwenda kukublock wao wakabaki kuona picha kinachoendelea mbali na wao kufika hakuna ukweli kwamba wakijua utafeli hakuna imani kubwa hivyo nje ya fitina.
LikeLike
Ndiyo, hakuna imani yoyote, ni fitins tu.
LikeLike
Swala la marafiki ni changamoto kweli, niwazi kwakuwa urafiki Mwinyi hutokea kama ajali .
Nashukuru kwa muongozo huu.
LikeLike
Vizuri.
LikeLike
Asante kocha wengi tulionao ni washirika na siyo marafiki. Unaweza kuwa na watu 100 lakini rafiki wa Kweli akawa mmoja.
LikeLike
Kabisa.
LikeLike
Asante sana kocha kwa kweli swala la urafiki ni changamoto kwasababu marafiki ukimkosea anatumia hiyo siri kukuadhibu pia marafiki hawana usiri kwa hiyo nimejifunza mengi hapa pia nimefurahi sana nitalifanyia kazi
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike
Habari Kocha Amani,
Mstoa Seneca ameeleza ukweli unaoishi mpaka Sasa, ni kweli wengi tumeishia kukwama katika malengo yetu ama Kwa kuwa wa Wazi sana au wasiri mno. Tumekosa misingi na hasa kwenye kujifunza. Naamini Kwa kuendelea kupata mafunzo haya ya ustoa, Kuna mambo yatabadilika kwenye fikra zetu hasa kwa wale watakao chukua hatua.
LikeLike
Ni kweli kabisa unayosema. Muhimu tuchukue hatua ili mafunzo haya yawe na tija kwetu.
LikeLike
Asante kwa somo hili,kumbe natakiwa nisiwe msiri sana pia nisiwe muwazi sana. 🙏🙏
LikeLike
Ndiyo.
LikeLike
Urafiki wa kweli ni bidhaa adimu sana.
LikeLike
Kabisa
LikeLike
Ukweli ni kwamba watu wengi hawajui nini maana ya rafiki, marafiki wa kweli ni nadra sana kupatikana, pia hakuna siri ya watu wawili.
LikeLike
Ni kweli kwenye ugumu wa kupata marafiki wa kweli.
Na kwenye siri, njia bora ya kutunza siri zako ni kutokuwa na mambo mengi ya siri, hasa yasiyokuwa na tija.
LikeLike
Asante Kocha. Hakika mambo haya matano ni kama Seneca aliyaandika jana, kumbe ni zaidi ya miaka 2000 iliyopita. Hii ya kabla ya urafiki hukumu baada ya urafiki amini, huwa inaenda hadi kwenye mahusiano mengine. Watu wana kuwa hawajuani vizuri, wanaanzisha mahusiano kisha ndo wanaanza kuchunguzana matokeo yake hawatachunguzana na kujuana vizuri kwa sababu tayari kuna hisia zimejengeka. Lakini kwa kufuata ushauri huu, urafiki na mahusiano mengi yanaweza kupona.
LikeLike
Ni kweli kabisa na hasa kwenye mahusiano, wengi wanakuja kujua wamefanya makosa wakiwa wameshachelewa sana.
LikeLike
Tutafute marafiki wa kweli Kwa kuwachuguza kwanza
Asante
LikeLike
Hakika.
LikeLike
Marafiki wa kweli imekua bidhaa adimu sana kwenye zama hizi kama ilivyo uaminifu,napaswa kuweka umakini na kuwachunguza wale naotaka wawe marafiki zangu kabla sijaanzisha urafiki nao.
LikeLike
Kabisa.
LikeLike
ni muhimu kwa kila mmoja wetu kupaata rafiki wa kweli
LikeLike
Hakika.
LikeLike
Asante kocha,nitajitahidi kujenga marafiki wa kweli baada ya kuwachunguza mda mrefu ili niweze kujenga maisha ninayofurahia.
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike
Marafiki -marafiki wa kweli kabisa ni wachache, angalia pote ulipopita hadi marafiki wangapi bado mpo wote,ndiyo maana kwa sasa naheshimu marafiki wazuri nilionao na kuweka kazi mbele.Binafsi nampongeza sana rafiki wa kweli wa mda wote.
LikeLike
Vizuri sana.
LikeLike