3063; Kataa kushindwa.

Rafiki yangu mpendwa,
Kitu kimoja ambacho nimekuwa narudia sana kukisema ni kwamba watu huwa hatupati kile tunachotaka, bali kile tunachokubali, tunachokivumilia.

Na nimekuwa nikitumia mifano rahisi ya miji mikubwa.
Ni vigumu sana ukasikia mtu amekufa kwa njaa kwenye mji wowote mkubwa.
Lakini ndani ya miji hiyo, kuna wengi ambao hawana mahali pa kulala.

Watu hao wasio na pa kulala huwa wanalala popote, hasa nje ya majengo ya biashara au majengo ambayo hayajakamilika kiujenzi.

Watu wa aina hiyo hawatavumilia kulala wakiwa na njaa, lakini watavumilia kulala nje.
Na ndiyo maana hutasikia wamekufa njaa, japo wataendelea kubaki hawana makazi yao.

Kwa sababu wamekataa kufa njaa, pale wanapokosa chakula, watafanya chochote kile ili tu wale. Watafanya kazi yoyote ili waweze kula, wakikosa wataomba na wakikosa watakuwa tayari hata kuiba.
Jambo muhimu kwao ni kula kwanza.
Na wakishashiba, mengine hayana ulazima kwao.

Kitu kikubwa sana tunachojifunza kwenye mfano huo ni kwenye maisha hatupati kile tunachotaka, bali tunachokubali au kupokea.
Wasio na makazi lazima watakuwa wanataka sana kupata makazi.
Lakini wanapokosa makazi, wanakuwa tayari kulala popote.
Wangekuwa wamekataa kabisa kulala popote, wangepambana kwa kila namna kupata makazi.
Kama ambavyo wamekataa kufa njaa, wanakuwa tayari kufanya chochote ili kupata chakula.

Kuna somo kubwa sana hapa kuhusu safari yetu ya mafanikio.
Mafanikio yako kwenye maisha yanategemea zaidi wewe kukataa kushindwa kuliko kutaka kufanikiwa.

Angalia, kila mtu anataka kufanikiwa, lakini ni watu wangapi wanaofanikiwa kweli? Ni wachache mno.
Wengi hawafanikiwi kwa sababu wanakubali, kupokea na kuvumilia kushindwa.
Pale wanaposhindwa kupata kile wanachotaka, wanakubali kupokea chochote kinachopatikana.

Kamwe huwezi kufanikiwa kwa kuwa na ulaini wa kiasi hicho.
Lazima ukatae kata kata kupokea na kukubali chochote ambacho ni chini ya kile unachotaka.
Lazima ujiwekee viwango vya juu kabisa vya mafanikio ambapo hutapokea chochote chini ya hapo.
Ni lazima upambane kwa kila namna, kufa na kupona ili ufanikiwe.

Mara ya kwanza namjua Kocha wa mafanikio Dan Pena niliona video kwenye mtandao wa YouTube ikiwa imeandikwa; Ni heri nife kuliko kuishi masikini (I will rather die than being poor).
Mara moja nikajiambia huyu ndiye mtu ninayetaka kumsikiliza.
Maana nakumbuka nikiwa mdogo, niliwahi kumwambia Mama yangu maneno makali sana ambayo mpaka leo huwa ananikumbusha.
Tulikuwa shamba na akawa ananiambia wewe hupendi kulima, maisha yako yatakuwa magumu.
Na hapo nikamjibu kwenye maisha yangu lazima nitakuwa tajiri, iwe kwa njia halali au zisizokuwa halali.
Sijui hata hiyo kauli niliitoa wapi, lakini tangu nikiwa mdogo nilichagua kuukataa umasikini.
Sasa nimekua na nimejua kuna njia halali nyingi za kupata mafanikio na utajiri, nimeondoa hilo la njia zisizo halali.

Kwenye safari yetu ya ubilionea tumetangaza vita na umasikini.
Tumeukataa umasikini kwa kila namna, hatutaki kujihusisha nao kwa namna yoyote ile.
Tunauchukia sana umasikini kiasi kwamba hatutaki hata kuutamka, hatutaki hilo neno lituzoee.
Tumemkataa huyo masikini na washirika wake wote ambao ni ujinga, uvivu, uzembe, kufuata mkumbo na kuridhika na vitu vidogo.

Kila mtu anataka utajiri,
Lakini ni watu wachache sana ambao wameukataa kabisa umasikini.
Unataka ushahidi?
Ni wangapi ambao wanadhibiti matumizi yasizidi kipato?
Ni wangapi ambao wanajilipa wenyewe kwanza, kwa kuweka akiba kwenye kila kipato kabla hata hawajakitumia?
Wangapi ambao wanafanya uwekezaji kwenye akiba wanazoweka?
Wangapi wanakazana kuongeza kipato chao?

Kama unataka utajiri na hufanyi hivyo vitu hapo juu, hakuna namna utaupata utajiri.
Kwa sababu unakuwa hujaukataa kweli umasikini.
Bado unaendelea kukumbatia tabia za kimasikini.

Kutaka ushindi kunaweza kukupa hamasa ya kuupambania huo ushindi, lakini ni kukataa kabisa kushindwa ndiko kunakufanya uwe mtu hatari.
Pale unapoondoa chaguo la kushindwa kwenye maisha yako, ndipo unapopambana kufa na kupona ili ufanikiwe.
Kataa kabisa kukubali na kupokea chochote ambacho siyo unachotaka hasa.
Fanya kila linalohitajika (siyo kila unaloweza) ili upate kile unachotaka.
Kwa sababu hata asili itakuwa tayari kukupa kile unachotaka, kama utakataa chochote chini ya hapo.

Sikutaka kuandika mengi kwenye ukurasa huu, ila kuna hili wazo limenijia hapa ambalo naona nisipolitaja sitakuwa nimetenda haki.
Watu wengi ambao wanasema hawana muda, siyo kweli kwamba hawana muda, ni kwamba tu kitu wanachosema hawana muda nacho siyo kipaumbele cha kwanza kabisa kwao.
Iweje mtu apate muda wa kula mara tatu kila siku, kuoga, kujisaidia, halafu akose muda wa kusoma kitabu?
Unaipata picha?
Basi, tuishie hapo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe