3064; Usawa usiowezekana.

Rafiki yangu mpendwa,
Sisi binadamu huwa tunapenda sana usawa kwenye kila eneo la maisha.
Tunapenda vitu vyote viende sawa ili tuyafurahie maisha yetu.
Lakini ukweli mchungu ni kwamba, hakuna usawa kwenye mambo yote na wala hautakuja kuwepo.

Mambo yote kwenye maisha huwa yanakwenda kwa kanuni za asili, ambazo haziangalii usawa bali msimamo uliopo.
Watu huwa wanatamani sana asili iende vile wanavyotaka wao, lakini asili huwa haiendi hivyo.
Na hapo ndipo wengi huvurugwa.

Moja ya eneo ambalo limewavuruga sana watu kwenye safari ya mafanikio ni kutaka usawa kati ya kazi na maisha.
Mafanikio makubwa yamekuwa yakitaka mtu aweke kazi sana.
Wakati huo huo watu wamekuwa wakitaka kuwa na usawa kati ya kazi na maisha.
Kwamba muda fulani uwe wa kazi tu na muda mwingine uwe wa maisha tu.

Hili ni jambo ambalo watu wengi sana wamelijaribu kwenye safari ya mafanikio na kuishia kushindwa vibaya.
Mafanikio makubwa hayataki utenganishe kazi na maisha, bali yanataka ufanye vyote kuwa kitu kimoja.
Mafanikio makubwa yanataka mtu uwe tayari kufanya kazi muda wote, kwa sababu fursa na changamoto huwa zinajitokeza muda wowote.

Kwa kutenganisha kazi na maisha kwenye safari ya mafanikio makubwa ni kupunguza kasi ya mafanikio au hata kuyazuia kabisa.
Mafanikio makubwa yanahitaji umakini na juhudi kubwa pia.
Siyo kitu unachoweza kufanya kwa urahisi.

Safari hiyo ni ngumu sana mwanzoni,
Hapo ndipo panapohitaji mtu aweke kila alichonacho.
Na hapo ndipo panapoamua kama mtu atapata mafanikio makubwa au atayakosa.

Inasaidia sana pale kile unachokuwa unafanya kinapokuwa ndiyo kitu unachopenda zaidi kufanya.
Hiyo itapunguza hitaji la wewe kutaka mapumziko au burudani.
Kama unachofanya ndiyo burudani kuu kwako, utakuwa tayari kukifanya muda wote bila ya kutaka mapumziko kwa ajili ya maisha.

Na kwa kuwa safari ya mafanikio unachagua kwa uhuru wako mwenyewe, chagua kile unachopenda sana ili usisumbuke na kutafuta usawa ambao haupo.

Kwenye ajira, wengi sana hutaka usawa wa kazi na maisha, kwa sababu wengi hawapendi kazi wanazofanya.
Ndiyo maana mwanzo wa wiki huwa wanachukia na mwisho wa wiki kufurahia.
Hilo limekuwa kikwazo cha mafanikio kwa wengi waliopo kwenye ajira.

Wanapokosea wengi wanaotoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri ni kwenda na mtazamo huo huo wa kutenganisha maisha na kazi, kitu kinachopelekea washindwe vibaya.

Mafanikio makubwa huwa yanahitaji mtu atoe kafara kubwa pia.
Na moja ya kafara hizo ni kuweka muda wako wote na maisha yako yote kwenye kile unachofanya.
Hilo linamtaka mtu kusema hapana kwa mengine yote isipokuwa anachofanya.
Hilo linataka mtu kuweka maisha yake yote kwenye hicho anachofanya.
Mtu anapofikiria tu kuhusu swala la usawa, kuhusu kupata muda wa kupumzika, anakuwa ameanza kupoteza.
Madhara ya fikra hizo huanza kuonekana mapema sana kwa matokeo mabaya yanayojitokeza.

Kwenye safari ya mafanikio makubwa, hakujawahi kuwa na usawa wa kazi na maisha, bali kunaweza kuwa na vipaumbele.
Muda mwingi kipaumbele kinakuwa kwenye kazi, na hapo mtu anapaswa kuweka kazi hasa.
Na muda mwingine kipaumbele kinakuwa kwenye maisha, kulingana na uhitaji unaokuwepo.

Njia bora ya kwenda na hilo la kazi na maisha siyo kwa kuwa na sheria fulani ya usawa unayokuwa unaifuata, bali kwenda jinsi mambo yanavyotaka.
Kama kazi inakutaka muda mrefu zaidi kulingana na unyeti wake, unaipa muda huo mrefu. Na kama kazi ina ahueni kwa kipindi fulani unaweka muda na umakini kwenye maisha.
Ni vipaumbele na mahitaji na siyo sheria yoyote ile.

Uzuri ni kwamba, kwenye safari ya mafanikio makubwa, mambo huwa yanaenda yakibadilika.
Mwanzoni hitaji la kazi linakuwa kubwa sana kiasi cha maisha kuonekana kama hayapo kabisa.
Lakini kadiri mtu anavyoendelea kufanikiwa ndivyo hitaji la kazi linapungua na maisha kupata nafasi.
Hiyo ni mbele sana ya safari na siyo wakati ambapo mtu anakuwa anaanza.

Ukweli ni kwamba safari ya mafanikio makubwa ni ngumu sana sana.
Hitaji la usawa wa kazi na maisha ni kitu ambacho hupaswi hata kukifikiria mwanzoni mwa safari hiyo.
Unachopaswa kufikiria ni wapi panahitaji kipaumbele zaidi na kupeleka hapo umakini na juhudi zako.
Hilo linataka sana uwe unapenda kile unachofanya ili usiwe na starehe nyingine yoyote unayoitaka nje ya kitu hicho.
Pale unachofanya kinapokupa raha, hutafikiria kuhusu usawa wa maisha na kazi, utaifanya kazi kwa sababu siyo tena kazi kwako, bali mchezo unaokupa raha.

Ukishajiona unaharakisha kazi ili uende kwenye starehe na mapumziko, jua umechagua njia isiyokuwa sahihi na mafanikio makubwa kwako yatakuwa magumu sana.
Chagua vyema kile unachofanya ili uweze kukipa kila ulichonacho bila ya kuhangaika na usawa wa kazi na maisha.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe