Huwa tunatengeneza picha ya hofu ambayo hata haipo kiuhalisia, tunatengeneza hofu na wasiwasi kisha hofu na wasiwasi vinatutengeneza na kuwa na wasiwasi na hofu katika akili zetu.

Wakati mwingine huwa tunafikiria tutalivukaje daraja kabla hata hatujalifikia, huwa tunaanza kuwa na hofu ya mambo yajayo, kwa kujiuliza maswali kama vile, vipi kama hiki au kile kikitokea? Kwa mfano, vipi kama nikiajiri msaidizi hatoweza kuniibia kweli? Hofu na wasiwasi unaingia ndani na kuacha kuajiri tena.
Vipi kama mke au mume niliyenaye akiniacha? Mtu anakuwa anaingiwa na wasiwasi na hofu na kuanza kujiandaa kwa kujenga nyumba ya pembeni kwa siri na hata kuwa na mtu mwingine kimahusiano ili hata likitokea la kutokea anakuwa yuko vizuri. Mambo haya yote yanaletwa na hofu.

Yaani, unakuwa na vitu ambavyo bado hata havijatokea, lakini watu wanajenga taswira inayowapa hofu kubwa.

Na kadiri mtu anavyokuwa na hofu, ndivyo hofu hiyo inavyochochea hofu zaidi ndani yake.

Mwanafalsafa Seneca anatufundisha njia bora za kukabiliana na hofu na wasiwasi ili kuwa na maisha tulivu.

Chanzo cha hofu,

Tofauti yetu sisi binadamu na viumbe wengine ni uwezo wetu wa kupangilia mambo yajayo. Tuna uwezo wa kufikiri na kutengeneza taswira yoyote kwa mambo yajayo. Ni pale uwezo huo unapotumika vibaya, ambapo mtu anatengeneza taswira mbaya ndipo hofu na wasiwasi huzaliwa.

Sehemu kubwa ya vitu ambavyo huwa tunavihofia huwa hata havitokei. Na hata pale vinapotokea, madhara yake huwa siyo makubwa kama tulivyokuwa tunahofia.

Hivyo hiyo inatosha kusema hofu na wasiwasi ni matumizi mabaya ya uwezo mkubwa ulio ndani ya kila mmoja wetu.

Seneca anaeleza kuna hofu kubwa mbili zinazowasumbua wengi, ambazo ni hofu ya kifo na hofu ya umasikini (au tamaa ya utajiri).

Hatua ya kwanza ya kukabiliana na hofu ambayo Seneca anafundisha ni kujua kwamba kuna mambo yapo ndani ya udhibiti wetu na mengine yapo nje ya udhibiti wetu. Hivyo tunapaswa kujua yaliyo ndani ya uwezo wetu na kuyafanyia kazi na yaliyo nje ya uwezo wetu kuyakubali jinsi yalivyo. Kwa mfano, una hofu ya kifo, huwezi kudhibiti kifo ni kitu ambacho kipo nje ya uwezo wako na unachotakiwa kufanya ni kutumia muda wako vizuri.

Hatua ya pili ni kuwa na tafsiri sahihi ya mambo yanayotokea. Mambo huwa yanatokea kwa namna yanavyotokea. Tafsiri ya kwamba mambo ni mazuri au mabaya ni sisi wenyewe tunaitengeneza. Hivyo kwa kuacha kuweka tafsiri mbaya kwenye mambo yanayotokea kunasaidia kupunguza hofu na wasiwasi.
Hapa kwenye tafsiri unapaswa kuwa makini sana.

Hatua ya tatu ni kuishi kwenye wakati ujao. Kama tulivyoona, hofu na wasiwasi ni zao la taswira tunazojijengea kwenye wakati ujao. Kama tukiacha kuhangaika na wakati huo ujao na kuishi kwenye wakati uliopo, tutapunguza sehemu kubwa ya hofu na wasiwasi.

Tunapaswa kutumia uwezo mkubwa wa akili zetu kukabiliana na yale yaliyo mbele yetu sasa badala ya kuhangaika na yajayo, ambayo bado hatujayafikia. Kwa mfano, unafikiria uzee wako utakuwaje?

Je, utawezaje kuvuka wasiwasi?

Falsafa ya Ustoa inashauri njia mbalimbali ambazo mtu akizichukulia hatua ataweza kuvuka wasiwasi wowote alionao.

Njia Tano Za Kuvuka Wasiwasi Ni Kama Ifuatavyo;

  1. Dhibiti tafsiri yako ya ndani juu ya mambo mbalimbali. Kinachotusumbua siyo kinachotokea, bali tafsiri tunayokuwa nayo kwenye kila kinachotokea.
  2. Kuacha kuishi kwenye wakati ujao na kuishi kwenye wakati uliopo, maana huo ndiyo wakati pekee unaoweza kuuathiri.
  3. Hoji imani na hisia zako kabla hujakubaliana nazo.
    Pale jambo linapotokea, kuna imani na hisia tunazokuwa nazo juu ya jambo hilo. Kukubaliana nazo haraka ni chanzo cha wasiwasi mkubwa. Unapaswa kuzihoji kama ni sahihi na kupata ushahidi wake. Kwa kuchukua hatua hiyo, nyingi zinakosa ushahidi na hivyo kuwa umeua nguvu yake ya kukupa wasiwasi.
  4. Kudhibiti tamaa pia inasaidia kukabiliana na wasiwasi. Pale unapokuwa na tamaa kubwa kwenye kitu fulani, wasiwasi na hofu vinakuandama kwa wingi na ukali zaidi

Hatua ya kuchukua;

Kuwa na mtazamo wa juu.
Wakati mwingine mambo unayokabiliana nayo yanakupa hofu na wasiwasi mkubwa kwa sababu unayapa ukubwa uliopitiliza. Unayaona ni makubwa sana kuliko uhalisia wake. Kuvuka hili unapaswa kuwa na mtazamo wa juu.

Pata picha umepanda juu sana angani na kuiangalia dunia kwa chini. Ukiwa juu sana angani dunia inaonekana kama mpira mdogo tu. Na hapo unajionea mwenyewe jinsi mambo unayoyahofia yalivyo madogo sana.

Kitu kimoja zaidi, Kwa kuacha kuyakuza mambo, unayanyima nguvu ya kukupa hofu na wasiwasi.

Rafiki na Mstoa mwenzako,
Mwl Deogratius Kessy