Kiasili sisi binadamu ni watu wa kulipa kisasi, pale mtu anapotutendea ndivyo sivyo huwa hatukubali tunahakikisha tunalipa kisasi.

Tusipolipa kisasi katika jamii zetu ni kama vile kuonekana mjinga, ila unapolipa kisasi ndiyo unaonekana mjanja.

Jamii imekuwa inakomeshana kwa njia ya visasi. Yote hii ni kwa sababu ya chuki iliyombika ndani ya moyo.

Chuki inatawala mahali popote pale ambapo hakuna nyumba ya upendo. Upendo unapokuwepo ndani ya mtu humsaidia kuvumilia yote.

Wakati mwingine watu wanataka kulipa visasi vya wivu. Mtu anapoona mwenzake amefanikiwa katika eneo fulani anakazana na yeye awe kama yeye, bila kujua malengo binafsi ya mtu, hii ni kama vile kudandia treni kwa mbele na matokeo yake ni mauti.

Kwa mfano, tuna visasi vya wivu wa kimapenzi, pale mtu wako wa karibu uliyempenda na kumwamini, anapokutendea ndivyo sivyo unajisikia vibaya, kwa nini anifanyie hivi na wewe unapatwa na hasira unajiambia ngoja na mimi nitamuonesha kazi, hivyo unajikuta unalipa visasi.

Tunalipa visasi siyo tu kwenye mahusiano bali pia hata kwa washindani wetu wa biashara, wasaidizi wetu pale tunapoona hawakubaliani na sisi huwa tunawatafutia dawa yao ambayo ni kuwalipia kisasi kwa kutumia mabavu yetu, nguvu ya kimadaraka tuliyonayo katika jamii, serikali, taasisi au hata nguvu ya fedha tunaamua kuwaliza kabisa wale ambao wanaenda au walikwenda kinyume na sisi.

Watu wengi wanaona kulipa kisasi ndiyo njia bora ya kuwaadhibu wale waliotuudhi na kutuumiza. Tunatumia tafsiri hasi ya dawa ya moto ni moto, kwamba mtu akikufanyia ubaya unapaswa na wewe umrudishie ubaya.

Ni kawaida ya watu wengi pale wanapoumizwa na watu wengine kitu cha kwanza kufikiria ni kulipa kisasi kwa adui yake au yule aliyemuumiza.

Kwenye maisha makwazo hayana budi kuja, kama tulivyojifunza kwenye masomo ya falsafa ya nyuma kwamba unapoamka asubuhi jiandae kukutana na watu ambao watakuudhi na kwenda kinyume na wewe.

Kwa mtu asiyekuwa na maarifa kama haya unayoendelea kupata ni rahisi kupata shida na wakati mwingine kuona dunia ni chungu na siyo sehemu salama kuishi.

Tunakubali kuteseka sisi wenyewe pale tunaporuhusu watu wengine watawale maisha yetu, watawale aili zetu na kutubebesha mizigo mingi ambayo hata hatustahili kuibeba.

Kwa nini uteseke? Kwa nini uvumilie maumivu yote hayo, unalipa kisasi ili nini?

Habari njema ni kwamba aliyekuwa mtawala wa Roma na mwanafalsafa wa ustoa Marcus Aurelius anatufundisha kisasi bora cha kuwafanyia wale waliotuudhi na kutuumiza.

Marcus anasema, kisasi bora ni kutokuwa kama adui yako. Yaani the best revenge is not to be like your enemy.

Njia bora ya kiustoa ya kulipa kisasi ni kutokuwa kama adui yako.

Njia bora ya kumuadhibu yule aliyekuudhi na kukuumiza ni kumtendea mema kadiri ya mabaya anayokufanyia kwenye maisha yako.

Hakuna kisasi ambacho kinamuumiza adui yako zaidi kama hii, hii ni adhabu kali kuliko adhabu yoyote ile unayoijua wewe.

Mtu anakutendea ubaya lakini wewe unamrudishia wema hakika utamwachia maswali mengi kichwani, utakua kama vile umemwekea kaa la moto kichwani, atajiuliza iweje mtu huyu mimi ninamtendea mabaya lakini yeye ananitendea mazuri?

Hatua ya kuchukua leo;

Moja, usiishi maisha ya kulipa kisasi, kisasi bora ni kutokuwa kama adui yako.

Mbili, kama adui yako hakusalimii, wewe msalimie tena kwa tabasamu zuri.

Tatu, kama adui yako anakurushia maneno mabaya, anakusengenya, anakupiga majungu wewe usimrudishie tena kisasi kwa kuanza kumrushia makombora ya umbea , majungu na mengine yanayofanana na hayo.

Tatu, usiwe na wivu na mtu, ishi maisha yako utapata ulivu

Nne, chagua kujisamehe na kuwasamehe wengine kwa yale yote waliokutendea.

Tano, mtu akikukosea au ukimkosea mtu omba msamaha. Msamaha ni tiba ya kuondoa uchungu ulioumbika ndani ya moyo.

Kitu kimoja zaidi kulipa kisasi inatokana na watu kutokuwa na mioyo ya kusamehe, kumbuka unasamehe kwa ajili yako wewe mwenyewe ili maisha yako yaende.

Sina uhakika kama itakufaa lakini kuanzia leo, jiambie kwamba kisasi bora kwenye maisha yako ni kutokuwa kama adui yako.

Kutokusamehe ni kama kunywa sumu ya panya huku ukisubiri adui yako afe.

Rafiki na mstoa mwenzako,
Mwl Deogratius Kessy