3113; Una kitu, utafika mbali.

Rafiki yangu mpendwa,
Leo nataka nikupe maua yako, nikupe sifa kwa vitu ulivyonavyo, ambavyo ukiamua kuvitumia vizuri, utafanya makubwa sana kwenye maisha yako.
Ni vitu ambavyo unaweza kuwa unavichukulia kawaida, lakini kama utavipa uzito, utaweza kufikia malengo makubwa uliyonayo.

Wewe kuwa hai mpaka sasa ni kitu kikubwa sana, ambacho ukiamua kukitumia vizuri, utafika mbali.
Sihitaji kuelezea sana umuhimu wa uhai, tunajua kabisa hakuna unachoweza kufanya ukiwa umekufa.
Lakini ukiwa hai, unakuwa na muda na nguvu za kufanya mambo.
Kama utalinda muda na nguvu hizo zisipotee na kuweka kwenye mambo sahihi, hutaweza kubaki hapo ulipo sasa.

Wewe kuwa na watu ambao tayari wanakuamini ni kitu kikubwa, ambacho ukikitumia utafika mbali. Mpaka sasa kuna watu ambao unashirikiana nao, ambao wanakuamini. Inaweza kuwa watu wako wa karibu, wateja kwenye biashara na wengine wanaokuzunguka.
Mafanikio huwa yanahitaji sana watu, ukiendelea kufanya yale yanayopelekea uaminike, utaweza kuwashawishi wengi na wakawa njia ya wewe kupata unachotaka.

Umeanzisha biashara ambayo mpaka sasa inakwenda. Hata kama biashara hiyo haijapata mafanikio makubwa, lakini umekuwa na uthubutu wa kuanzisha na umepambana nayo mpaka pale ilipofika sasa. Ni kitu kikubwa sana ambacho unacho, ambacho siyo wengi wanacho. Wengi hawana uthubutu wa kuanzisha biashara, licha ya kutaka sana. Na hata wale wanaoanzisha, wengi biashara hizo zinakufa ndani ya muda mfupi baada ya kuanzisha.
Wewe kuwa kwenye biashara kwa kipindi ambacho umekuwepo, ni kitu kikubwa, kitumie vizuri na utafika mbali zaidi.

Wewe kuwa na malengo makubwa ya kufikia ubilionea ni kitu cha kipekee sana. Swala tu la kufikiri ni kitu unachoweza kukifikia, linakutofautisha na wengi sana ambao wanaona ni kitu kisichowezekana kabisa. Hicho ni kitu kikubwa ulichonacho, ambacho ukikitumia vizuri, kwa kuendelea kuamini unaweza na kuchukua hatua, lazima utafikia lengo hilo.

Wewe kuwa ndani ya jamii bora kabisa ya KISIMA CHA MAARIFA na BILIONEA MAFUNZONI ni kitu kikubwa sana, ambacho ukikitumia vizuri, utafika mbali sana. Ni wengi sana wanatamani kuwa kwenye jamii ya aina hii lakini hawapati nafasi hiyo ambayo umeipata wewe. Ithamini nafasi hiyo na kuifanyia kazi kwa uhakika ili upate mafanikio makubwa unayoyataka.

Rafiki, haya niliyogusia hapa ni machache sana kati ya mengi mazuri ambayo tayari unayo.
Ninachotaka ni kukukumbusha kwamba tayari una kitu ndani yako, usijichukulie poa.
Lakini chochote ulichonacho ndani yako hakitakuletea matokeo yoyote chenyewe.
Bali unahitajika kukifanyia kazi kwa uhakika ndiyo kiweze kuzalisha matokeo makubwa.

Dhana kubwa sana ambayo nataka wote tuondoke nayo hapa ni kila mtu ana zawadi za kipekee alizonazo.
Wengine wanaita uwezo mkubwa, wengine wanaita vipaji.
Lakini ukweli ni kila mtu kuna vitu anaweza kufanys vizuri kuliko watu wengine.
Anakuwa na msukumo wa kufanya bila ya kuchoka, hata kama hakuna anayemlipa.

Wajibu wako mkubwa kwenye safari yako ya mafanikio ni kujua vitu ambavyo wewe unaweza kuvifanya kwa ubora kuliko watu wengine, unapata msukumo wa kuvifanya bila kuchoka hata kama hakuna anayekulipa.
Hivyo ndiyo vitu ambavyo unapaswa kuvifanya kwa ukubwa zaidi ili upate mafanikio makubwa unayoyataka.
Vingine waache wengine wafanye, wewe komaa na hivyo ambavyo una upekee navyo.

Uzuri ni kwamba, wewe tayari unao huo uwezo wa kipekee, una vitu unavyofanya kwa ubora kuliko watu wengine wote.
Hicho ndiyo kitu ambacho unacho, hivyo basi, unapaswa kukitumia vizuri ili uweze kufika mbali zaidi.
Fanya zaidi vitu ambavyo uko vizuri zaidi kwenye kuvifanya na utaweza kufanya makubwa zaidi.

Epuka kuiga wengine au kushindana nao.
Hapo unaacha kitu chako na kuhangaika na vitu vya wengine, kitu kitakachopelekea ushindwe vibaya sana.
Cheza kwenye uwanja wako wa nyumbani, kwa kutumia kile ambacho tayari kipo ndani yako.

Kwenye maoni hapo chini tushirikishe ni kitu gani cha kipekee unacho na unakitumiaje kufika mbali zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe