3126; Usichezee ‘matirio’

Rafiki yangu mpendwa,
Hebu pata picha mtu amenunua basi lenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 30, lakini anaamua kulitumia kama usafiri binafsi.
Kwa hakika utashangazwa na jinsi rasilimali hiyo itakavyokuwa imetumika vibaya.

Au mtu ananunua kompyuta yenye uwezo mkubwa wa kurahisisha majukumu mengi, ila mtu anaamua kuitumia kusikiliza muziki pekee.
Japo mtu huyo anakuwa na uhuru wa kutumia vitu vyake atakavyo, anapovitumia chini ya kiwango kilichozoeleka, anaishia kuwashangaza watu.

Sasa njoo kwenye hili kosa ambalo umekuwa unalifanya kila siku.
Una akili na mwili wenye uwezo wa kufanya makubwa sana bila ya ukomo wowote.
Lakini unaamua kutumia uwezo huo mkubwa kufanya kazi au biashara yako kwa mazoea, kuangalia tv, kuzurura kwenye mitandao na kufuatilia maisha ya wengine.

Kwa hakika ni matumizi mabaya mno ya rasilimali kubwa ambayo tayari unayo.
Upo hapa duniani kwa kusudi maalumu, ambalo ni kugusa maisha ya watu wengi zaidi kwa namna chanya, na kuwaacha wakiwa bora zaidi ya walivyokuwa kabla ya kukutana na wewe.

Umekuwa kikwazo kwako wewe mwenyewe kwa muda mrefu sasa.
Kuna fursa nyingi za kufanya makubwa ambazo zimekuwa zinajitokeza ila umekuwa unashindwa kuzitumia vyema.

Na kwa hili huna cha kujitetea.
Unaweza kusema kuna vipaji ambavyo umekosa ndiyo maana umeshindwa kufanya makubwa.
Lakini kuna watu anbao wanafanya makubwa mno huku wakiwa na vipaji vichache kuliko wewe.

Matumizi sahihi ya ‘matirio’ makubwa uliyonayo ili uweze kuzalisha matokeo makubwa pia ni kama ifuatavyo;
1. Kuwa na malengo na mipango mikubwa ambayo unaifanyia kazi hatua kwa hatua.
2. Kujifunza endelevu ili kujenga ujuzi unaohitajika ili kupata kile unachotaka.
3. Weka kazi kubwa na kwa juhudi kubwa sana.
4. Jenga tabia sahihi ambazo zinarahisisha maamuzi yako na hatuz unazochukua.
5. Kuwa na fokasi kubwa na kujikinga na usumbufu wa kukimbizana na vitu vipya kila wakati.

Kwenda kinyume na hayo matano ni kujidharau wewe mwenyewe.
Kupoteza ‘matirio’ mengi uliyonayo kwa kuhangaika na mambo yasiyo na tija.

Wale unaowaona wamepiga hatua kubwa kuliko wewe, siyo kwamba wana uwezo mkubwa sana kukiko wewe, bali wamechagua kutumia vizuri uwezo ambao tayari wanao, ambao hata wewe mwenyewe unao pia.

Inzi na nyuki wote wanaruka ruka siku nzima.
Lakini wakati nyuki anaishia kuzalisha asali tamu na yenye manufaa, inzi anakuwa amesambaza magonjwa kwa kukaa kwenye vinyesi na mazingira mengine machafu.
Nyuki hatumii muda wake kumshawishi inzi aachane na mambo yake ya kijinga, bali anakazana na wajibu wake wa kuzalisha asali.

Amua sasa kama unakuwa nyuki au unakuwa inzi.
Usiharibu na kutumia vibaya uwezo mkubwa uliopo ndani yako.
Kwa chochote ambacho umeshaweza kufanya mpaka sasa, unaweza kufanya kwa ukubwa zaidi ya ulivyowahi kufanya.
Uwezo tayari unao, ni matumizi sahihi tu kwa upande wako ndiyo yanahitajika ili uweze kuzalisha matokeo bora na makubwa zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe