3131; Subiri.

Rafiki yangu mpendwa,
Kadiri ninavyojifunza, kufuatilia na kuishi maisha ya kujenga mafanikio makubwa, ndivyo ninavyozidi kuona jinsi ambavyo kushindwa kwa walio wengi kunatokana na kukosa subira.

Kabla sijaendelea kutetea hilo na kukushawishi uwe na subira zaidi, tuangalie mfano wa asili kabisa kwenye hilo.

Ili mti uote, unahitaji vitu vinne; ardhi yenye rutuba, maji, hewa ya oksijeni na mwanga wa jua.
Mimea huwa inatumia mwanga wa jua kuzalisha chakula chake yenyewe, hivyo basi, mwanga huo wa jua huwa ni hitaji muhimu zaidi kwenye ukuaji.

Sasa basi, hapo ndipo penye mtego mkali sana. Miti inayopata mwanga mwingi wakati wa uchanga, huwa inakua kwa haraka sana, lakini mazao yake huwa ni dhaifu. Kwa mfano mbao itakayotokana na miti iliyokua kwa haraka huwa siyo imara, zinaliwa kwa urahisi na wadudu na haziwezi kutengeneza kitu chochote imara.

Miti inayoota chini ya kivuli cha miti mingine mikubwa, huwa haipati mwanga mwingi, hivyo uzalishaji wake wa chakula hauwi mkubwa na hilo kupelekea ukuaji wake kuwa wa tararibu sana. Lakini mazao yake huwa imara sana. Mbao inayotokana na miti ya aina hii huwa imara, haiharibiwi kirahisi na wadudu na inatengeneza vitu imara.

Hapo asili inatupa somo kubwa sana kuhusu kusubiri.
Chochote kinachokua haraka, huwa pia kinaharibika haraka.
Na kwa kuwa kanuni za asili huwa zinafanya kazi kila eneo bila kushindwa, hivyo ndivyo pia inavyokuwa kwenye safari ya mafanikio.

Mafanikio yoyote yanayopatikana kwa haraka, huwa yanapotea kwa haraka pia.
Na hilo lina ushahidi mwingi ambao ni wa wazi kabisa, kwa wale waliopata mafanikio ya haraka na kuishia kwenye anguko kubwa.

Kuna vitu viwili vikubwa ninavyotaka tuondoke navyo hapa na kwenda kuvifanyia kazi kwenye safari yetu ya mafanikio.

Moja ni pale unapokuwa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka, lakini hupati matokeo iliyokuwa unategemea kupata, kuwa na subira.
Mara nyingi sana watu huwa wanakimbilia kufanya vitu vya tofauti kabla hawajaweka muda wa kutosha kwenye vile walivyoanza navyo.
Pamoja na juhudi kubwa unazoweza kuweka, kuna vitu inabidi uvipe muda ndiyo viweze kukupa matokeo unayotaka.
Sehemu kubwa sana ya safari ya kujenga mafanikio makubwa ni kuwa na subira.
Na wengi wanaoshindwa siyo kwa sababu hawajui wanachotaka, au hawajui nini wanapaswa kufanya, bali wanakuwa wamekosa subira.

Mbili ni kuna wakati unahitaji kukataa fursa nzuri za ukuaji wa kasi kwa sababu unakuwa hujajenga misingi imara ya kuhimili ukuaji huo.
Hili ni gumu sana kuelewa na kukubali, lakini lina nguvu kubwa sana.
Ndiyo, unajifunza na kuweka juhudi kubwa ili kupata matokeo makubwa.
Halafu unakutana na fursa kubwa ya kukupa matokeo makubwa na kwa haraka, ila kwa uwezo wako wa sasa, huwezi kuhimili fursa hiyo.
Wengi hukimbilia kukubali fursa hiyo na kupata mafanikio ya haraka ambayo yanaleta anguko kubwa.
Kwa walio wengi wanaona kusema hapana kwenye fursa ni kuikosa milele. Ambacho hawajui ni kwamba kusema hapana kwenye fursa fulani, kunakujenga kuweza kunufaika na fursa kubwa zaidi.
Pale unapokutana na fursa nzuri lakini ni kubwa kuliko uwezo wako wa kuihimili, epuka tamaa ya kuipokea kwa sababu unataka ukuaji wa haraka.
Badala yake jijengee kwanza uwezo wa kuhimili fursa kubwa ili uweze kuzitumia kwa manufaa.

Ukishafanya kilicho sahihi, kinachofuata ni wewe kusubiri.
Endelea kufanya kilicho sahihi na endelea kusubiri.
Endelea kujifunza na kuwa bora na endelea kusubiri.
Endelea kufanya kwa ubora zaidi na endelea kusubiri.
Rudia kufanya hayo yote kwa msimamo bila kuacha na endelea kusubiri.
Kwa mwenendo huo, utajenga msingi imara sana ambao unaweza kuhimili kiwango chochote cha mafanikio utakachokipata.

Inahitaji uwe na msimamo mkubwa kuwa na subira kwenye zama hizi ambazo kila mtu anaonekana kufanikiwa haraka kuliko wewe.
Lakini pia ukiangalia jinsi wengi wanavyoanguka na kupotea, unazidi kuona jinsi subira ilivyo muhimu kwenye hii safari.
Fanya yaliyo sahihi na kuwa na subira. Hapo ndipo penye nguvu kubwa mno ya kukupa mafanikio yoyote unayoyataka.

##NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe