3153; Kiburi cha umasikini.

Rafiki yangu mpendwa,
Tofauti kati ya matajiri na masikini imekuwa inaendelea kukua kwa kasi kubwa.
Masikini wamekuwa wanaendelea kuwa masikini zaidi na zaidi, huku matajiri wakiendelea kupata utajiri mkubwa zaidi na zaidi.

Wengi wamekuwa wanatoa sababu zao mbalimbali juu ya tofauti hiyo, lakini zimekuwa ni za juu juu tu.
Sababu halisi na kiini hasa kinachoendekea kuwatofautisha masikini na matajiri ni kiburi cha umasikini.

Masikini wamekuwa na kiburi fulani hivi ambacho kimekuwa hakiwasaidii zaidi tu ya kuwapoteza.
Kwa upande wa pili matajiri wamekuwa na unyenyekevu ambao umekuwa msaada mkubwa sana kwao.

Kwenye kujifunza, masikini wamekuwa na kiburi kwamba tayari wanajua kila kitu na hakuna kipya cha kujifunza.
Wakati matajiri wamekuwa wanyenyekevu kwenye kujifunza, hata kama ni kitu wanachorudia kujifunza.

Kwenye kuanzisha na kujenga biashara masikini wamekuwa na kiburi kwamba wanaweza kuendesha biashara zaidi ya moja kwa wakati mmoja, kitu kinachowasumbua sana.
Wakati matajiri wamekuwa wanyenyekevu wa kujenga biashara moja kwa wakati mpaka ifikie mafanikio ndiyo wanaingia kwenye nyingine.

Kwenye ukaaji wa kwenye mchakato masikini wamekuwa na kiburi kwamba hawahitaji mchakato wowote, badala yake wanafanya kwa hisia, pale wanapojisikia.
Wakati matajiri wamekuwa na unyenyekevu wa kuheshimu mchakato na kuufuata kwa msimamo bila kuacha.

Kwenye mafanikio ya wengine masikini huwa na kiburi cha kuona waliowazidi mafanikio wana bahati au walisaidiwa kufika walipofika hivyo hawahangaiki kujifunza chochote kwao.
Wakati matajiri wamekuwa na unyenyekevu wa kuona waliowazidi mafanikio kuna kitu wanakijua ambacho wao hawajui, hivyo huwa tayari kujifunza kwao na kuchukua hatua za tofauti, kitu kinachowapa matokeo ya tofauti.

Kwenye kuweka akiba na kufanya uwekezaji endelevu masikini wamekuwa na kiburi kwamba hawawezi kujitesa hivyo wanatumia kipato chao chote na cha ziada, wakiamini wataanza kuweka akiba na kuwekeza pale kipato chao kitakapokuwa kikubwa.
Wakati matajiri wanakuwa na unyenyekevu wa kuanza kuweka akiba na kuwekeza hata kipato kinapokuwa kidogo sana na wanaendelea kukuza tabia hiyo kadiri kipato kinavyoongezeka.

Kwenye kushirikiana na wengine masikini wana kiburi kwamba wao ni jeshi la mtu mmoja hivyo wanaweza kufanya kila kitu peke yao, kitu kinachowachosha sana na kuwapunguzia uzalishaji na ufanisi.
Wakati matajiri wana unyenyekevu wa kujua hawawezi kufanya kila kitu peke yao, badala yake wanahitaji ushirikiano wa watu wengine, kitu kinachowapa matokeo mazuri.

Kwenye kugatua majukumu yao masikini wamekuwa na kiburi kwamba hakuna mtu yeyote anayeweza kufanya kile wanachofanya wao kwa ubora wanaofanya, hivyo huendelea kufanya wenyewe na kufurahi pale wanapotegemewa kwenye kitu hicho.
Wakati matajiri wamekuwa na unyenyekevu kwamba wapo wengine wengi wanaoweza kufanya kile wanachofanya vizuri tu na kuwatafuta kisha kuwapa majukumu nayo na hivyo kuweza kukua zaidi.

Kwenye kukimbizana na fursa mpya kila wakati, masikini wamekuwa na kiburi kwamba wanaweza kuzitambua na kuzifanyia kazi fursa zote mpya wanazokutana nazo na hilo limekuwa linachukua muda wao mwingi.
Wakati matajiri wana unyenyekevu wa kujua kwamba fursa kuu kwao ipo kwenye kile wanachofanya na hivyo hawahangaiki na fursa mpya zinazojitokeza kila wakati.

Masikini wamekuwa na kiburi cha kuamini kuna siri ya mafanikio ambayo imefichwa na matajiri na wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kutafuta njia ya mkato ya kufanikiwa bila kuweka kazi, mwishowe wamekuwa wakitapeliwa na kupoteza fedha na muda.
Matajiri wamekuwa na unyenyekevu wa kuamini siri kuu ya mafanikio ni kuweka kazi na hakuna njia ya mkato ya kufanikiwa, wanaweka kazi kubwa kwa muda mrefu na wanayaona mafanikio.

Tofauti hizo zinaweza kuonekana ni ndogo sana kwa tukio la mara moja.
Lakini zinavyokwenda hivyo kwa muda mrefu, mfano kwa miaka 10, ndiyo unawapata watu wawili ambao wanatofautiana sana, hata kama walianzia mahali wanapolingana.

Ni kiburi kipi cha umasikini ambacho ulikuwa nacho kwa muda mrefu kabla ya kukubali kukaa kwenye huu mchakato wa Bilionea Mafunzoni kwa uhakika na msimamo?
Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini.

Amua leo kuvunja kila aina ya kiburi cha umasikini.
Achana kabisa na mtazamo wa masikini jeuri.
Kuwa mnyenyekevu na utaziona fursa nyingi za kujifunza na kuchukua hatua ili kufanya makubwa zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe