Mstoa mwenzangu,

Kama tulivyojifunza jana kwenye makala ya kwanza ya ustoa, tunapaswa kuwa wanafalsafa kwa kuishi falsafa kwa matendo na siyo maneno.
Falsafa ni kupenda hekima,
na hekima ni kupenda kujifunza na kuchukua hatua.

Huwezi kuwa na furaha kama huna hekima. Ukiwa huishi falsafa, utakua ni mtu wa kununua matatizo ya watu kila siku.
Falsafa siyo kujionesha bali ni kuishi Ustoa.

Huwa tunajitengenezea hatari nyingi katika maisha yetu bila ya sisi wenyewe kujua. Huwa tunaongea tu na kuona hakuna shida lakini wale wanaotusikiliza au kupokea ndiyo wanakuja na tafsiri zao kupitia kile tulichoongea.

Tunazalisha matatizo au kununua matatizo kwa midomo yetu wenyewe. Tumekosa kuwa na kiasi ni nini tunapaswa kusema na wapi na kwa wakati gani.

Falsafa ya Ustoa inatufundisha kuwa, unapaswa kusema pale kitu ambacho unataka kusema ni muhimu sana na usiposema mambo hayatoenda.

Ni rahisi mtu kupona kidonda alichoumizwa na kitu kuliko kidonda cha maumivu aliyopata kwa maneno. Maneno huwa yanaumiza sana na tunaalikwa kuwa makini na kufikiri kile tunachotaka kuongea kwani unapoongea bila kufikiri ni kama unatupa jiwe gizani na hujui nani litampata.

Mwanafalsafa Epictetus yeye ana kitu kizuri sana cha kutushauri pale tunapokuwa tunaongea na watu wengine au tunapokuwa kwenye mazungumzo.

“In conversations,  avoid  talking at great length or excessively about your own affairs and adventures; however pleasant it may be for you  to  talk about the risks you have run, it  is not equally  pleasant for other people to  hear about your adventures. “

Katika mazungumo yoyote yale unayofanya epuka sana kuongelea mambo yako binafsi na matukio.
Unaporuhusu kuongelea mambo yako binafsi siyo kila mtu atapenda kusikia mambo yako binafsi.

Kuongelea mambo yako binafsi ni kama vile unatangaza hatari, unawaambia kuwa wewe uko hivi. Watu wakishakujua mambo yako, watakua wanakutumia kukuumiza vile wanavyotaka.

Hata kama una kitu, ishi kwa namna ambayo watu hawawezi kujua kama una kitu fulani. Ustoa siyo falsafa ya kujionesha kwa watu, kwamba una fedha , mali kiasi gani bali falsafa ya Ustoa ni kuishi maisha ambayo hakuna mtu anaweza kukuelewa kama unayo au huna. Kama ni utajiri, basi uwe utajiri ni kile kisichoonekana.

Usitengeneze matatizo na watu, kama una hela unajionesha una hela, unakaribisha matatizo kwako binafsi. Kifupi watu ambao hamna ukaribu na usiri kama hapa tunavyoishi kwenye kisima cha maarifa, hawapaswi kujua mambo yako, yaani wasikuelewe wakuone tu.

Kuwa na mafanikio makubwa, ni kutokueleweka na watu wanaokuzunguka. Kama watu wanakuelewa basi bado huishi misingi ya falsafa ya Ustoa. Ukishaeleweka tu, umesharuhusu matatizo na watu.

Wewe kama mwanafalsafa, usianike mambo yako hadhari, unapoweka mambo yako hadhari pale unapokuwa kwenye mazungumzo na watu wengine unakuwa unaibua chuki na wivu ambao hauna hata maana.

Utavunja mahusiano na watu wengi na kujiweka katika hali ya hatari, kila mtu atakufahamu na hivyo wewe utakua mtumwa kwa watu hao.

Kuna vitu ambavyo hupaswi hata kuviongelea kwa watu, wewe fanya kile ambacho ni sahihi na matokeo yataonekana na siyo kuanza kujisifu mbele za watu.

Epuka chuki na wivu usiokuwa na maana kwa kuacha kuanika mambo yako binafsi hadharani. Ukiwa na jambo kidogo unaposti kila mtu anajua kinachoendelea kwenye maisha yako na watu huwa wanakusanya taarifa zako na kisha kuzituma kukuhadaa. Tunza siri zako binafsi ili uwe salama na maisha yako.

Siyo kila mtu ni salama kwako, na siyo kila mtu ana stahili kuambiwa mambo yako binafsi. Jifunze kunyamaza wakati mwingine, kama wewe ukinyamaza hakuna atakayejua.

Unapoanika mambo yako binafsi hadharani ni kama vile unajitangazia kununua matatizo kwa lazima.

Kuna mambo matatu ambayo watu hawapaswi kujua kuhusu wewe ila ni wewe tu, kwa mfano afya siyo kila mtu anapaswa kujua afya yako.

Fedha, siyo kila mtu anapaswa kujua juu ya kipato chako, haya ni mambo ya ambayo watu wengine hawapaswi kuyajua bali inabaki na kuwa siri kwako na wale ambao unahisiana nao kihuduma kama Kocha anayekufuatilia.

Familia na mahusiano yako kiujumla, watu wa nje hawapaswi kujua nini kipo ndani ya mahusiano yako kifamilia, mambo ya familia yabaki kuwa ya familia tu.

Mambo hayo matatu hapo juu, yaepuke sana kuyaongelea kwenye mazungumzo yako. Epuka kuongea juu ya mambo yako binafsi hadharani.

Kwa mfano, unaweza kuongea habari za familia yako, mke, mume au watoto watu wakaingiwa na wivu. Kwa mfano, wanawake wana tabia ya kuhadithiana kwamba mume wangu yuko hivi, na anapoongea anakuwa anaongea na wanawake wenzake na wale wanawake wanakuwa na wivu, wanataka kile ambacho mwenzao anafanyiwa wao hawakipati hivyo wanajitahidi kwa kila namna kuweza kuhakikisha wanampata huyo mwanaume ili nao wapate kile wanachokisikia.

Hatua ya kuchukua leo; Siyo kila mtu anapenda kusikia juu ya mambo yako binafsi, usiongelee mambo yako binafsi hadharani bali iwe ni siri yako tu.

Kwahiyo, jifunze kuwa makini na mwenye hekima, usipende watu wakujue undani wako kwani watu wakishakujua tayari umejikabizi na kuwa mtumwa wao.
Kuwaambia watu mambo yako binafsi ni kama vile kuambia upepo siri zako na kutegemea kuwa mambo yako hayata sambaa kwa watu wengine.

Ya nini kujitesa roho, tulia na mambo yako, kama unataka sana kuwaambia watu, yaandike na ukifa watu watajua baada ya kusomewa.
Kila mmoja awe na hekima, kuepuka hili alilotushauri Mwanafalsa Epictetus.

Kila la heri rafiki yangu.

Mstoa mwenzako,
Mwl Deogratius Kessy.