Rafiki yangu katika Ustoa,

Tunaishi kwenye jamii yenye maneno, karibu kila siku tunasikia maneno yakisemwa juu yetu sisi wenyewe na hata watu wengine.

Kuna wakati tunayasikia maneno mabaya na kuna wakati tunasikia maneno mazuri yakisemwa. Hatuwezi kuwazuia wengine wasituseme kwani hakuna mtu ambaye hasemwi, kama maiti inasemwa sembuse wewe uliye hai?

Hakuna mtu ambaye anaweza kumpiga teke mbwa aliyekufa. Kama watu wanakusema juu ya kitu fulani basi jua kuna kitu ndani yako. Mti ambao una matunda, ndiyo mti ambao unashambuliwa na wengi.
Una thamani ndiyo maana unasemwa.

Maneno yote tunayosikia juu yetu au juu ya wengine tunaweza kuyaita umbea tu kwa sababu hatuna ushahidi. Kitu chochote ambacho huna ushahidi ni umbea huo. Lazima kama wanamafanikio, tuweze kuongea na ushahidi, kama hatuna ushahidi basi huo ni umbea.

Kuna wakati tunaletewa habari za umbea juu yetu. Kuna habari njema huwa tunazisikia lakini kuna wakati tunasikia habari mbaya juu yetu, na huwa zinatuumiza.

Kama hujui jinsi ya kukabiliana na habari ambazo unazisikia juu yako au wengine, lazima utapata taabu.

Vipi kama mtu akija na kunisema vibaya au nimesikia wakinisema vibaya nitawajibu vipi?
Niwarudishie maneno? Niwafungulie mashtaka au niwaoneshe kwamba mimi ni nani?

Aliyekuwa mwalimu na Mwanafalsafa wa Ustoa Epictetus, anatushirikisha jinsi ya kuwajibu watu ambao wanatusema vibaya.

Epictetus anasema, kama mtu anakusema vibaya, na ikiwa ni kweli, basi jirekebishe.

Siyo kila ambayo tunayasikia watu wakisema ni uwongo, mengine ni kweli kabisa. Watu hawawezi kukusingizia kila kitu kuhusu wewe. Na waswahili wanasema, lisemwalo lipo, kama halipo, basi linakuja.

Ukisikia watu wanakusema juu ya jambo lolote lile, wewe kaa chini na kujiuliza je, haya ambayo nimeyasikia ni ya kweli? Kama ni ya kweli, basi jirekebishe.

Waswahili wanasema, mjumbe hauwawi, mtu akikuletea jambo, kama ni kweli basi jirekebishe. Na yako mengi ambayo tunayasikia juu yetu, lakini tunaishia kuwachukia wale ambao wanasema vibaya juu yetu.

Huwezi kuwazuia watu wasikuseme, ila unaweza kujirekebisha tu ikiwa ni kweli.

Kama watu wanakuongelea vibaya juu yako, mke, mume, watoto, biashara, mahusiano yako kiujumla, ikiwa ni kweli basi jirekebishe kimya kimya. Mtu anavyoongea habari juu yako ni kama anarusha jiwe gizani, kuna mawe yakirushwa, yako ambayo hayatakupata na yako ambayo yatakupata.

Wewe ni mwanafalsa wa Ustoa, ikiwa unasemwa na ni kweli, jirekebishe mara moja bila kurudisha maneno. Na usiweke chuki juu ya yule aliyekuambia.

Vipi kama maneno wanayosena siyo kweli? Vizuri, wala usiwe na wasiwasi ikiwa mtu anakusema vibaya na siyo kweli yaani ikiwa ni uwongo, cheka na endelea na maisha yako.

“If evil be said of thee, and if it be true, correct thyself; if it be a lie, laugh at it.” ― Epictetus

Kama mtu anakusemea maovu juu yako, na ikiwa ni kweli, jirekebishe. Na ikiwa ni uwongo, cheka juu ya kile ulichosikia au ulichoambiwa.

Hatua ya kuchukua;
Ikiwa unasemwa na ni kweli, jirekebishe na ikiwa ni uwongo cheka juu ya kile ulichosikia.

Kama kitu siyo sahihi usifanye. Na kama kitu siyo kweli usiseme.

Kuna wakati unaweza ukawa umetulia na unaendelea na mambo yako. Mara ghafla anakuja mtu na kukuambia, mtu fulani anakusema vibaya.

Sasa badala ya kutaharuki, wewe kuwa mpole, wala usitake kujitetea, na kutaka kuwaonesha kwamba wao hawako sahihi ila wewe ndiyo uko sahihi.

Dawa ya moto ni moto. Mtu akija, akikuletea umbea, au akikuambia mtu fulani anakusema vibaya, wala usitake kujitetea bali mjibu, mbona kuna mengine mengi mabaya  ambayo hayajui zaidi ya hayo ambayo angepaswa kusema.

Kama mtu akija anakuletea umbea, ukimwambia mbona kuna mengine ulikuwa hujui, utakuwa umemkata wenge, yaani ataanza kujiuliza kama kwa haya niliyosikia anasema kuna mabaya mengine ambayo siyajui,  ataishiwa pozi. Atajisemea huyu mtu ni wa namna gani, mimi nilijiona kinara kumbe kuna mengine ambayo siyajui. Utakua umemchanganya na mtihani wa umbea utakua umefeli kwake.

If anyone tells you that a certain person speaks ill of you, do not make excuses about what is said of you but answer, “He was ignorant of my other faults, else he would not have mentioned these alone. Epictetus

Kama mtu yeyote akikuambia mtu fulani anakuongelea vibaya, wala usijipe sababu ya kujitetea kuhusu kile kilichosemwa, mwambie alikuwa hajui mabaya yangu mengine, asingepaswa kuorodhesha haya peke yake.

Watu wakija na moto, wakate moto, wachanganye zaidi ili wabaki wasikuelewe.

Sina uhakika kama itakufaa lakini kama mtu anakuletea umbea, na mhusika yuko karibu, mwambie subiri kidogo, halafu mwite mhusika kisha mwambie ongea kile unachotaka kuniambia na mhusika akiwepo.

Kwa njia hii, utapunguza umbea na maneno yasiyokuwa na maana kwako. Kumbuka, kila unalolisikia juu yako, kama ni kweli jirekebishe na kama ni uwongo cheka na endelea na maisha yako.

Rafiki na mstoa mwenzako,
Mwl Deogratius Kessy