3214; Kupoteza kabla ya kupata.

Rafiki yangu mpendwa,
Kufanya biashara na ujasiriamali ni sawa na kucheza mchezo ambao unaanza kwa kupoteza kabla ya kupata.
Na hilo ndiyo limekuwa linawakwamisha wengi wanaoanza wasiendelee.

Unapoianza safari, unaanza kwa kupoteza muda.
Hapa unajikuta ukitumia muda wako mwingi kwenye kujenga biashara ambayo una ndoto nayo itakuja kuwa kubwa.
Unajikuta ukiwa na mambo mengi unayopaswa kufanya, wakati muda unaokuwa nao ukiwa ni mchache.
Kwa namna biashara inavyokuwa inakuhitaji, huwezi kupata muda kwa ajili ya mambo mengine nje ya biashara hiyo unayoijenga.

Kinachofuata ni kupoteza fedha.
Unapoianza safari unakuwa na mipango mikubwa na mizuri, hivyo unakuwa na matumaini makubwa.
Unaweka fedha ulizokusanya au kupata ili kufikia ndoto kubwa uliyonayo.
Lakini kwa ugeni wa mwanzo, kunakuwa na mengi ambayo hukuwa unayajua na hivyo kujikuta ukipoteza fedha kwa mambo ambayo hayajawa sahihi kama ulivyopanga na kutegemea.

Utapoteza usingizi.
Kwa kuwa muda umeshapotea na fedha nazo huna tena kama wakati unaanza, hupati usingizi mzuri.
Unahitaji muda mwingi wa kukamilisha majukumu mengi uliyonayo.
Lakini pia kwa sababu fedha nazo huna, unakosa usingizi kwa kuwaza utapata wapi fedha zaidi kwa ajili ya kukamilisha majukumu makubwa yaliyo mbele yako, mfano kulipa wasambazaji au wafanyakazi.

Kukosa muda, fedha na usingizi kunakupelekea upoteze watu wa karibu.
Kwa kuwa maisha yako yanabadilika na kuwa kama umevurugwa, wengi hawatakuelewa na hilo litadhoofisha mahusiano yako na kuishia kupoteza watu hao.
Utapoteza marafiki, utashindwa kuelewana na ndugu na ndoa inaweza kuishia kwenye talaka, kama msogo utakuwa mkubwa.

Swali ni nini fidia ya hayo yote unayopoteza?
Na jibu lipo wazi, fidia ni kupata uhuru wa kifedha na muda hivyo kuweza kufanya chochote unachokuwa unataka kufanya.
Uhuru huo utapunguza makali ya baadhi ya yale uliyopoteza wakati wa kuanza.

Swali jingine ni kama ni rahisi hivyo mbona wengi hawafanyi?
Majibu ni uhalisia wa kila jambo, maelezo huwa ni rahisi kuliko utendaji, hivyo kama umeona ni rahisi kwenye maelezo, subiri mpaka wakati wa kufanya ndiyo utaelewa.
Pia inahitaji roho ngumu sana kuendelea na mchezo ambao umeanza kwa kupoteza kwa kiasi kikubwa.

Swali la mwisho ni itachukua muda kiasi gani mpaka kuanza kupata ushindi?
Jibu ni hakuna ajuaye kwa uhakika ni baada ya muda gani utaanza kupata manufaa.
Kitu pekee ambacho una uhakika nacho ni hiki; kama utaendelea kucheza bila kuacha, lazima utakutana na ushindi.
Hivyo basi, wajibu wako mkubwa ni kuhakikisha pamoja na upotevu ambao utaupitia mwanzoni, hupotezi kila kitu na kushindwa kuendelea.
Ukiweza kuendelea na mchezo bila kuacha licha ya upotevu, ushindi ni wako kwa uhakika.

Karibu kwenye huu mchezo na kila unapopoteza, jua ni maandalizi ya kupata zaidi baadaye.
Wajibu wako mkubwa ni kudumu kwa muda mrefu zaidi na utaweza kufanya makubwa zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe