3216; Fokasi, Muda Na Msimamo.

Rafiki yangu mpendwa,
Kila kitu kinafanya kazi,
Kila biashara inalipa,
Kila kazi inaweza kukupa chochote unachotaka.
Lakini bado tunaona watu wanahangaika na mambo mengi na hawapati kile wanachotaka.

Siyo kwamba watu hao hawajui wanachotaka, wanakuwa wanajua sana.
Siyo kwamba wanakuwa hawajui wanachopaswa kufanya, wanakijua sana.
Na wakati mwingine siyo kwamba ni wavivu au wazembe, wanaweza kujitahidi sana tu.
Lakini hayo ambayo yalipaswa yamsaidie mtu, ndiyo yanakuwa kikwazo kwake.

Kwa kujua kile anachotaka, anakuwa anatamani sana kukipata kwa haraka.
Kwa kujua anachopaswa kufanya ili kupata, anahangaika kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja na hivyo yote anayagusa juu juu tu.
Na hali ya uchapakazi ambayo mtu anakuwa nayo anajikuta akipoteza nguvu nyingi kwenye mambo ambayo hayana tija kabisa.

Baada ya mtu kujua unachotaka na unachopaswa kufanya ili kukipata, unahitaji muunganiko wa vitu vitatu ambavyo kwa pamoja vina nguvu sana.
Vitu hivyo ni Fokasi, Muda na Msimamo.

Tukianza na fokasi, hapa ndipo wengi sana wanakwama, hasa pale wanapoona wamechelewa.
Wanakazana kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja, kitu kinachotawanya sana nguvu zao.
Hivyo wanatumia nguvu nyingi lakini matokeo yanakuja madogo, kwa sababu nguvu hizo wanazitawanya sana.
Kama wangekusanya nguvu hizo kwenye eneo moja, ambapo ndiyo kufokasi, wangezalisha matokeo makubwa zaidi.

Tukienda kwenye muda, tunajua dhahiri kwamba mambo mazuri yanahitaji muda kujijenga.
Lakini inapokuja kwenye ufanyaji, watu huwa wanasahau kabisa hilo.
Wanapoweka juhudi na wasione matokeo, wanaona juhudi hizo hazifanyi kazi.
Hivyo wanaacha na kwenda kwenye kitu kingine.
Huko nako hali inajirudia.
Ni lazima mtu ukubali kwamba muda unahitajika kwenye kujenga kitu chochote kikubwa.
Hakuna juhudi unazoweka zikapotea, bali zinakuwa zinajikusanya tu, wakati sahihi ukifika matokeo yatazalishwa kwa wingi na ukubwa.

Mwisho kuna watu ambao wamejipa muda mrefu kwenye kufanya kitu, lakini bado hakuna hatua kubwa ambazo wamepiga.
Wanaweza kulalamika jinsi ambavyo wamekuwa kwenye kitu fulani kwa muda mrefu.
Unaweza hata kuwaonea huruma kwa jinsi wameweka muda mrefu kwenye kitu.
Lakini unapochunguza kwa undani jinsi wanavyofanya ndiyo unaona wapi wamekuwa wanajikwamisha.
Wengi sana wanashindwa kufanya kitu kwa msimamo bila kuacha.
Wanaweza kupata shauku na hamasa ya kufanya kitu, wanafanya kwa siku chache kisha wanaacha.
Wanasubiri tena hamasa nyingine.
Kwa hiyo licha ya kuwa kwenye kitu kwa muda mrefu, matokeo makubwa yanakosekana kwa sababu ya kutokuwepo kwa ufanyaji kwa msimamo.

Fokasi, katika mengi ya kufanya, chagua moja ambalo ndiyo utalipa kila ulichonacho.
Jipe muda wa kutosha, mambo yote mazuri yanahitaji muda kujijenga na kukua.
Na fanya kwa msimamo bila kuacha, hata kama unafanya kidogo kidogo, wewe usiache kufanya. Inyeshe mvua, liwake jua, wewe fanya.

Ukiweka vitu hivyo vitatu pamoja, unakuwa kiumbe hatari sana hapa duniani.
Kwa sababu ni lazima utapata kila unachotaka, bila ya kujali ni njia ipi uliyoitumia.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe