3222; Haya matatu yanakushindaje ukiwa hai?

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna mambo mengi unayowajibika nayo kwenye maisha yako.
Mambo hayo ni mengi na yote yanakutegemea wewe moja kwa moja bila kujali wingi na ukubwa wake.

Katika hayo mengi, kuna mambo matatu ambayo kwa namna yoyote ile hupaswi kukubali yakakushinda.
Mambo hayo matatu unapaswa kuyafikia kwa viwango vya juu kabisa bila kuruhusu chochote kuwa kikwazo kwako.

Jambo la kwanza ni afya.
Una wajibu wa kuwa mtu mwenye afya bora kabisa kipindi chote cha maisha yako.
Hilo linawezekana na linakutegemea wewe moja kwa moja.
Inapokuja kwenye afya, wewe ndiye mwenye uwezo wa kila kitu.
Kwa sababu inahusisha ulaji wako, ufanyaji wa mazoezi na kujikinga na hatari mbalimbali.
Unapaswa kuwa mtaalamu wa mwili wako, kuzingatia yote yanayohitajika ili kuwa na afya bora kabisa.

Jambo la pili ni utajiri.
Una wajibu wa kuwa na utajiri mkubwa kwenye kipindi chote cha maisha yako.
Wewe ndiye mwenye ufunguo wa utajiri mkubwa kwenye maisha yako.
Kwani unachohitaji ni kila mara kuhakikisha unaongeza kipato chako huku ukidhibiti matumizi yako.
Tofauti ya mapato na matumizi unaweka akiba na kuwekeza, mara zote, kwa msimamo bila kuacha.
Hupaswi kukubali wala kuruhusu umasikini kuwa sehemu ya maisha yako.

Jambo la tatu ni hekima.
Una wajibu wa kuwa mtu mwenye hekima kwenye kipindi chote cha maisha yako.
Hekima ni zao la kujifunza na kuchukua hatua kwenye yale unayojifunza ili kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.
Hili ni jambo ambalo lipo ndani ya uwezo wako, maana fursa za kujifunza zipo nyingi na za wazi na kuchukua hatua ipo ndani ya uwezo wako.
Hakikisha kila mara kuna mambo mapya unayojifunza na hatua unazochukua ili kuyafanya maisha yako kubwa bora zaidi.

Kuna mambo mengine yanaweza kukusumbua kwenye maisha yako, lakini kamwe hayapaswi kuwa haya matatu.
Haya yanapaswa kuwa vizuri mara zote, kwa sababu yanakutegemea wewe moja kwa moja.
Huna wa kumlaumu kama utakuwa na afya mbovu, masikini na mpumbavu.

Dhamiria kuwa vizuri kwenye maeneo hayo matatu ya maisha yako na utaweza kuwa na maisha bora kabisa kadiri unavyotaka wewe mwenyewe.

Kamwe usikubali mambo hayo matatu kukushinda unapokuwa hai.
Yapambanie kwa kila namna mpaka kuyafikia, hayo ndiyo yanayojenga maisha yako kwa uhakika.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe