3230; Ni kwa sababu bado hujapata ushindi.

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna juhudi nyingi na kubwa unazokuwa unaweka kwenye yale unayofanya.
Lakini kwa sababu bado hujazalisha matokeo yanayoonekana, wengi watapuuza juhudi zako.
Tena wapo ambao watakuona kama umechanganyikiwa kwa hayo unayofanya.

Ni mpaka pale unapoweza kuzalisha matokeo makubwa na ya tofauti ndiyo kila mtu anazitambua juhudi zako na kuziheshimu.
Ni muhimu sana ujue hili ili usikate tamaa kabla hujapata matokeo mazuri unayoyalenga kwa sababu watu wanapuuza juhudi zako.

Huwa wanasema mtu huwa anaonekana ni kichaa pale anapofanya mambo ya tofauti na ambayo hayajazoeleka.
Lakini pale mambo hayo yanapoleta matokeo makubwa na ya tofauti, mtu huyo anaonekana kuwa na akili kubwa.

Pata picha kama ungekuwa ni mtu mgeni kabisa hapa duniani na hujui jinsi ambavyo mazao mbalimbali yanapatikana.
Ukawaona watu wanachukua mbegu za mazao na badala ya kula, wanazifukia chini.
Hilo litakushangaza sana.
Na kama haitoshi, unaona watu hao wakimwagilia maji kwenye mbegu hizo.
Kama hujui kwamba mbegu zinafukiwa kwanza ardhini kabla ya kuota, utamwona anayefanya hivyo kama amechanganyikiwa.
Ni mpaka pale mbegu hizo zinapoota na kuzaa matunda ndiyo utamwona aliyezipanda alikuwa na akili.

Kamwe usikatishwe tamaa kama bado hujazalisha matokeo unayoyaona kwenye ndoto na maono yako.
Kwa sababu kabla ya matokeo, hakuna mtu yeyote anayeweza kukuelewa kwenye mambo ya tofauti unayofanya.
Waelewe kwamba hawatakuelewa, hivyo endelea na mapambano mpaka uzalishe ushindi.

Ukishapata ushindi kila mtu atakusifia na kusema una akili nyingi.
Kila mtu atapenda kujifunza kwako.
Lakini kabla ya ushindi, utaonekana huna lolote.

Hivyo basi, usiache mpaka umepata ushindi unaotaka kuupata, hata kama hakuna anayekuelewa.
Endelea kuvumilia na kupambana, ushindi utakaoupata utafuta yote unayopitia sasa.
Ukiweza kuziba masikio yako na kuweka juhudi mpaka upate ushindi, utaweza kufanya makubwa sana.

Kadhalika, jiandae kwa ngozi ngumu zaidi pale utakaposhindwa.
Maana hapo ndipo utapata fedheha za kila namna.
Ufazidi kudharauliwa na kuonekana umechanganyikiwa.
Utashauriwa sana kuachana na hayo unayofanya na kufanya yale ya kawaida ambayo yanafanywa na kila mtu.
Lakini kamwe usikubaliane na hilo.
Wewe endelea kuweka juhudi huku ukiuangalia ushindi ambao tayari upo ndani yako.
Utakapoudhihirisha ushindi huo, kila mtu atakuelewa na kukusifia.

Pambana mpaka utakapopata ushindi mkubwa kwenye maisha yako.
Huo ndiyo utakaokupa uhalali kwa wengine.
Kabla ya ushindi, jua wewe ni yatima, hilo lisikukatishe tamaa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe