3238; Akili ikikosekana, haya yawepo.

Rafiki yangu mpendwa,
Warren Buffett amekuwa anasema unapotaka kuajiri, angalia vitu vitatu, uadilifu, akili na nguvu. Na anaendelea kusisitiza kama sifa ya kwanza haipo, hizo mbili zitakumaliza kabisa.

Hizo ni sifa tatu muhimu sana kuzingatia ili kupata watu sahihi.
Lakini pia ni sifa ambazo siyo rahisi kuzipata kwa walio wengi.
Hasa kipengele cha akili.
Ni watu wachache sana ambao wana akili kubwa na uwezo wa hali ya juu.
Na watu hao kuwaajiri siyo rahisi, kwa sababu labda wanakuwa wanafanya mambo yao au wameajiriwa mahali pengine ambapo wanapata maslahi mazuri.

Unapokuwa unaanza au bado upo chini na huwezi kumudu kupata wafanyakazi wenye akili kubwa na uwezo wa hali ya juu, basi hakikisha unazingatia sifa hizi tatu; njaa, unyenyekevu na uaminifu.

Njaa ni sifa muhimu sana kuiangalia kwa watu unaowaajiri au unaotaka kushirikiana nao.
Njaa ni pale mtu anapokuwa anajua kitu anachotaka na amejitoa kweli kukipambania mpaka akipate.
Watu wenye njaa ya kufika mahali fulani tayari wanakuwa na msukumo mkubwa ndani yao.
Siyo watu wa kusubiri mpaka wewe uwasukume. Njaa yao ni msukumo tosha kwao.
Utawajua wenye njaa kwa msukumo wanaokuwa nao kwenye kile wanachotaka.
Ukikutana na asiye na njaa, utamjua tu, uvivu na uzembe unakuwa mwingi na inakuwa kazi kubwa kwako kumfanya afanye kazi.
Watu wa aina hiyo ni wa kuachana nao.

Unyenyekevu ni utayari wa kujifunza na kuchukua hatua kwenye yale ambayo mtu amejifunza.
Watu wengi ambao hawana akili na uwezo mkubwa, ni wa kuelekezwa nini wanapaswa kufanya.
Kama watakuwa na ujuaji, kwa kukataa kujifunza na kufanya vile wanavyotaka wao, wanakuwa mzigo mkubwa.
Fanya kazi na wale ambao wana utayari wa kujifunza na kufuata taratibu mbalimbali ambazo umeziweka.
Epuka sana wale wajuaji na ambao wanadhani wana njia bora kuliko utaratibu ulioweka wewe.
Watu hawa huishia kutengeneza matatizo ambayo yanakugharimu kuyatatua.

Uaminifu lipo wazi, unahitaji kushirikiana na watu ambao ni waaminifu.
Na hapa pia, kama uaminifu utakosekana, hivyo viwili vya mwanzo vitakumaliza kabisa.
Fikiria una mtu mwenye njaa kali ya mafanikio na ni mnyenyekevu sana, lakini siyo mwaminifu.
Njaa yake kali itamsukuma kufanya makubwa na unyenyekevu wake utakuhadaa kumwona ni bora.
Kukosa kwake uaminifu kutakuletea matatizo makubwa.
Utaujua uaminifu wa mtu baada ya kufanya naye kazi na kuangalia kama maneno yake yanaendana na matendo.
Kama kuna mkanganyiko wowote kati ya maneno na matendo, jua wazi uaminifu hakuna.

Rafiki, sifa hizo tatu siyo za kumuuliza mtu akakujibu. Maana kila mtu tayari anajinadi kuwa na sifa nyingi nzuri.
Hizo ni sifa za kuangalia wewe mwenyewe wakati unafanya kazi na mtu.
Hivyo unapochuja watu wa kufanya nao kazi, kuwa na maswali ambayo yatakusaidi kupata wale ambao unaona watakuwa na sifa hizo.
Lakini kazi hasa ya kujua kama sifa hizo zipo ni pale unapofanya nao kazi.
Unapaswa kuendelea kuwafuatilia watu unaojihusisha nao mara zote na kuangalia kama hizo sifa zipo.

Pale unapojidhihirishia bila ya shaka yoyote kwamba kuna sifa kati ya hizo tatu zinakosekana kwa mtu, usiendelee naye.
Unaweza kujiambia mtu atabadilika na hata yeye mwenyewe kukuahidi hivyo.
Lakini mabadiliko siyo rahisi kiasi hicho.
Hivyo usipoteze muda na nguvu na watu ambao siyo sahihi kwako.
Una kazi kubwa zaidi kwako kufanya kuliko kuwabadili watu.

Fanya kazi na wale ambao tayari wanazo sifa unazozitaka.
Na usihofie kwamba huwezi kuwapata.
Hii dunia ina watu wengi sana.
Na kati ya hao wengi, wapo wale ambao wana sifa unazotaka.
Ni wewe kuweka kazi kuhakikisha unawapata na kufanya nao kazi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe