3246; Ushindi unaotaka.

Rafiki yangu mpendwa,
Ushindi wowote unaoutaka kwenye maisha yako, unawezekana kama tu utaacha kuwa na mashaka na kukataa kushindwa.
Hivyo ndivyo vitu viwili ambavyo vimekuwa vinawakwamisha watu wengi kupata ushindi.

Mashaka hayapaswi kupewa nafasi kama mtu unataka kupata ushindi mkubwa.
Ukishakuwa tu na mashaka, unakuwa umeshikilia breki na hivyo huwezi kuendelea mbele kwa kasi kubwa.
Mashaka yanakufanya urudi kuchunguza kitu mara mbili mbili badala ya kwenda mbele kwa kasi kubwa.
Kuwa na mashaka ni kukubali kushindwa.

Ushindi unaoutaka kwenye maisha ni kukataa kushindwa.
Japokuwa kwenye safari yako ya kupata ushindi unakutana na hali mbalimbali za kukukwamisha, wewe unakataa kukubaliana nazo.
Badala yake unaendelea kusonga mbele, kukiendea kile unachotaka.
Na hivyo ndivyo unavyopata ushindi mkubwa kwenye maisha yako.
Unaposhindwa na ukakubali, hapo ndipo unakuwa umemaliza safari yako na kuwa umeshindwa.
Lakini unaposhindwa na ukakataa, safari ya ushindi inakuwa inaendelea.

Ili uendelee kubaki kwenye safari kwa muda mrefu zaidi, ambao ndiyo ushindi wenyewe, unapaswa kupuuza yote ambayo hayahusiani na ushindi unaoutaka.
Yaani unakuwa kipofu na kiziwi kabisa kwa yale yote ambayo hayakupi ushindi unaokuwa unautaka.
Ni kwa njia hiyo ndiyo unaweza kuvuka vikwazo mbalimbali vilivyopo kwenye safari yako ya kupata ushindi.

Ukijali sana kila unachokutana nacho kwenye safari yako ya ushindi, utapoteza muda mwingi kwenye mambo ambayo hayana mchango kwenye ushindi wako.
Pambania ushindi wako,
Ona tu kile unachotaka kupata,
Na dunia itafanya kila namna kuhakikisha unakipata.

Ushindi hautakuwa rahisi, lakini haimaanishi kwamba haiwezekani.
Uwepo wa waliopata ushindi ni kiashiria kwamba ushindi unawezekana.
Lakini kwa waliopata ushindi kuwa wachache wakati wanaoutaka ni wengi ni kiashiria kwamba siyo rahisi.
Wewe jitoe hasa kuupata ushindi mkubwa unaoutaka na usikubali kuyumbishwa na chochote kile.

Usiwe na mashaka ya aina yoyote ile kwenye safari yako ya ushindi.
Amini bila ya shaka yoyote ile kwamba utashinda.
Unapokutana na vikwazo usiviangalie kama kushindwa, bali vione kama hatua za wewe kuufikia ushindi mkubwa unaoutaka.
Nenda hivyo na kwa hakika utapata chochote kile unachokitaka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe