3267; Kuzingatia na Kuepuka.

Rafiki yangu mpendwa,
Mara nyingi watu wamekuwa wanafundishwa na kushauriwa kuhusu mambo ya kuzingatia ili kupata mafanikio wanayokuwa wanayataka.
Hayo ni mambo ambayo wanapaswa kuyafanya ili wapate matokeo wanayotaka kupata.

Mambo ya kuzingatia ni muhimu, lakini hayo pekee hayatoshi kumpa mtu mafanikio makubwa anayokuwa anayataka.
Kwani huwa kuna mambo yasiyo muhimu au hata yenye madhara ambayo huwa yanajipenyeza kwenye mipango ya mtu.
Mambo hayo huwa yanajipenyeza kwenye nafasi zinazopatikana kulingana na udhaifu ambao mtu anakuwa nao.

Ni kwa sababu hiyo ndiyo inapaswa mtu pia kuwa na mpango wa mambo ya kuepuka kufanya. Hapa ni kuzuia yale mambo yanayojipenyeza na kumkwamisha mtu kupata mafanikio anayokuwa anayataka.
Kwa kupanga kwa makusudi kuyaepuka hayo mambo, kunayanyima nguvu ya kujipenyeza na kuleta madhara kwenye mipango yako.

Hivyo basi, kama ambavyo unapanga mambo ya kuzingatia ili kufanikiwa, hakikisha pia unapanga mambo ya kuepuka ili yasikukwamishe kwenye mafanikio yako.

Tuangalie mfano wa biashara ili tuelewane vizuri zaidi.

Ili kujenga biashara yenye mafanikio makubwa, unapaswa kuzingatia mambo haya;
1. Kutoa thamani kubwa kwa wateja.
2. Kujenga timu bora ya kuendesha biashara hiyo.
3. Kutengeneza wateja bora na kwa uendelevu.
4. Kutengeneza faida kwa uhakika.
5. Kulitawala soko au eneo fulani la soko.
6. Kuendelea kukua kadiri muda unavyokwenda.

Hayo yote ni mambo ya kujumlisha au kuongeza ili biashara iweze kufanikiwa.
Lakini kufanya hayo pekee bado haitoshi, kwani kuna ambayo huwa yanajipenyeza na kuvuruga.
Hayo ndiyo unapaswa kuyaepuka ili kujenga biashara yenye mafanikio.

Yafuatayo ni mambo ya kuepuka kwenye kujenga biashara yako;
1. Epuka gharama zinazokuwa zinaongezeka kwenye biashara kadiri kipato kinavyoongezeka.
2. Epuka kuhangaika na mambo ambayo hayana mchango kwenye ukuaji wa biashara yako.
3. Epuka watu ambao hawaja mchango kwenye maendeleo ya biashara.
4. Epuka wateja ambao siyo sahihi kwa biashara yako, wale ambao hawaielewi thamani unayoitoa.
5. Epuka kufuata mkumbo au kuiga wengine kwenye yale wanayofanya.
6. Epuka kukimbizana na fursa mpya kila wakati kabla biashara yako haijaweza kujiendesha yenyewe bila kutegemea uwepo wako.

Hayo ya kuepuka ni ya kukataa au kuondoa kabisa kwenye mipango yako ili jugudi kubwa unazoweka zisikwamishwe na mambo madogo madogo ambayo unaweza usione madhara yake kwa haraka.

Kwenye safari yako ya mafanikio usiangalie tu ya kuzingatia, bali pia angalia ya kuepuka ili ifanikiwe.
Kama ambavyo Charlie Munger alikuwa akisema; “ninachotaka kujua ni wapi nikienda nitakufa ili nisiende hapo.”
Wewe kila mara jiambie; “ninachotaka kujua ni nini nikifanya kitaua biashara yako ili nisikifanye.”

Kuepuka matatizo kuna nguvu na manufaa kuliko kuja kuyatatua baada ya kutokea.
Ukizingatia na kuepuka kwa pamoja, inajenga nguvu ya kuzalisha matokeo makubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe