3286; Kushangazwa na dunia.

Rafiki yangu mpendwa,
Kanuni rahisi ya furaha inahusisha matarajio na uhalisia.
Pale matarajio yanapokuwa makubwa kuliko uhalisia, mtu unakosa furaha.
Na pale matarajio yanapokuwa madogo kuliko uhalisia, mtu unapata furaha.

Inapokuja kwenye matarajio na uhalisia, dunia huwa inatushangaza.
Tunapokuza sana kimoja, kingine huwa kidogo mpaka kutushangaza.
Hivyo dunia inaweza kutushangaza kwa uchanya, pale uhalisia unapokuwa mkubwa kuliko matarajio.
Au ikatushangaza kwa uhasi, pale uhalisia unapokuwa mdogo kuliko matarajio.

Itakuwa ni vyema kama dunia itatushangaza kwa uchanya.
Hivyo tunachopaswa kufanya ni kuweka matarajio yetu chini sana, huku tukiweka juhudi zetu juu sana.
Hapo matokeo yoyote yatakayokuja, lazima yatatushangaza kwa uchanya.

Hivyo sivyo wengi wanavyofanya.
Kwa sababu watu wanapenda kujipa matumaini hewa.
Ni matumaini hewa kwa sababu juhudi wanazoweka zinakuwa haziendani kabisa na matarajio wanayokuwa nayo.

Matumaini yanakuwa sahihi pale juhudi zinapozidi matarajio yanayokuwepo.
Na kwa kuwa dunia lazima itakushangaza, anza wewe kwa kuishangaza dunia.
Ishangaze dunia kwa juhudi kubwa sana unazoweka ambazo ni zaidi ya matarajio unayokuwa nayo.
Weka juhudi ambazo hakuna mwingine anayeweka kwa kiasi hicho.

Japokuwa dunia itakupa matokeo ya tofauti na matarajio, hilo lisikushangaze kwa namna yoyote ile.
Kubali kila matokeo yanayokuja na yatumie ili kufanya kwa ubora zaidi.

Kumbuka huidai dunia chochote,
Ulikuja ukaiacha na utaondoka ukaiacha.
Wajibu wako ni kujua kile unachotaka, kuweka juhudi kubwa kwenye kukipata na kupokea kila aina ya matokeo yatakayopatikana.
Tumia matokeo hayo kuboresha zaidi ili kusogea karibu zaidi na kile unachotaka.

Waache wengine washangazwe na dunia, wewe nenda nayo kwa namna sahihi kwako ili kupata kile unachotaka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe