3287; Mabadiliko ya watu.

Rafiki yangu mpendwa,

Moja ya vitu vigumu sana kutokea ni watu kubadilila.
Mabadiliko huwa ni kitu kigumu sana kwa watu kiasi kwamba ukiona yametokea kweli, basi mtu anakuwa amelipa gharama kubwa sana.

Katika hali za kawaida, watu huwa hawabadiliki.
Kile ambacho kwa nje tunaweza kuona kama ni mabadiliko ya mtu, huwa ni mtu kurudi kwenye uhalisia wake baada ya kuchoka kuigiza.

Pale unapoona mtu amerudi nyuma ukilinganisha na alivyokuwa anafanya awali, anakuwa hajarudi nyuma, bali hakuwa vizuri kama ulivyodhani.
Huenda ulikuwa unamwona kwenye nyakati nyepesi na kudhani anafanya makubwa, kumbe siyo.

Hata pale unapoona watu wamepiga hatua fulani kubwa kwenye maisha yao, siyo kwa sababu ndiyo wamekuwa bora kuliko walivyokuwa huko nyuma. Bali wanakuwa wamepata fursa ya kudhihirisha uwezo mkubwa ambao tayari upo ndani yao.

Ni asili ya binadamu kwamba watu huwa hawabadiliki. Hivyo chochote unachokiona kama mabadiliko kwa mtu, ni anakuwa tu amechoka kuigiza na kuamua kuwa halisi kwao.

Kumbuka hili mara zote ili usishangazwe na watu.
Na kwa upande wako, yaishi maisha yako halisi mara zote ili watu waweze kukutegemea kwa uhakika kwenye kile unachofanya.
Pale watu wanapokuwa na uhakika na mtu, wanafanya naye kazi kwa muda mrefu na manufaa yanakuwa mazuri kwa wote.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe