3303; Wa kumfuata mwenzake.

Rafiki yangu mpendwa,

Pale unapokuwa unashirikiana na watu wengine, na wewe ukawa uko mbele zaidi ya hao wengine, huwa unafanya nini ili muweze kwenda pamoja?

Kwa walio wengi huwa wanapunguza kasi yao na kuwasubiri hao wengine ili waambatane nao.
Hapo wanakuwa wameshusha viwango vyao ili kuweza kueleweka na wengine ambao viwango vyao chini.

Kwa wachache wanaopata mafanikio makubwa wanayokuwa wanayataka, huwa wanawataka wengine kuongeza kasi ili wawafikie.
Wanakataa kushusha viwango vyao ili kueleweka na wengine.
Badala yake wanawataka hao wengine kukuza viwango vyao ili wawafikie na kuweza kushirikiana vizuri.

Rafiki, swali linakuja kwako unatumia njia ipi?
Je unapunguza kasi ili wengine wakufikie mwende pamoja?
Au unaendelea na kasi yako na kuwataka wengine nao waongeze kasi ili waweze kukufikia.

Kujenga mafanikio makubwa, lazima ushirikiane na wale wanaoongeza kasi ili kukufikia.
Hao wanakupa msukumo wa kuendelea kufanya makubwa zaidi.

Watu wote wanaojihusisha na wewe wanatakiwa kuielewa sheria yako rahisi inayosema; panda kufikia viwango vyangu au nisikuone kwenye maisha yangu.

Simamia viwango vyako mara zote ili kuhakikisha wengine wanapambana kuvifikia ndiyo waweze kushirikiana na wewe.
Kataa mengine yote ambayo yapo chini ya viwango vyako, hivyo ndivyo unavyoweza kujenga mafanikio makubwa na ya uhakika.

Ni muhimu kila wakati kujikumbusha malengo yako makuu ili usiingie kwenye mtego wa kudhani kuwafurahisha wengi zaidi ndiyo mafanikio.
Mafanikio kwako ni kupata matokeo makubwa unayoyadhamiria.
Hilo halitawezekana kama pia unataka kila mtu ajisikie vizuri.

Mafanikio makubwa yanamtaka mtu ajitoe kisawasawa. Wale wanaotaka wewe ushushe viwango ndiyo muweze kushirikiana badala ya wao kukuza viwango, siyo ambao wanaweza kukusaidia wewe kupata mafanikio makubwa unayoyataka.

Wajibu wako mkubwa kwenye maisha ni kupata kile unachotaka hasa na siyo kuwafanya wengi wajisikie vizuri.
Na ili kupata unachotaka, lazima uwasukume wengi wapandishe viwango vyao ili kufikia viwango vyako wewe.
Hakikisha hilo ndiyo unalofanya na siyo kinyume na hapo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe