Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea,

Leo ikiwa ni jumatano ya ukamilishaji, tunakwenda kuwa na siku bora kuwahi kutokea ya kuuza zaidi huku tukiongozwa na kauli mbiu yetu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA.

Habari njema ni kwamba leo tunaendelea na mbinu nyingine mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo.
Karibu sana tujifunze kwa pamoja na kwenda kuyafanyia kazi mara tu baada ya kujifunza na kuweka vitendo ili upate matokeo.

Mauzo ni vita lakini ni vita isiyoruhusu kumwaga damu.
Kwa kuwa mauzo ni vita, ndiyo maana tuko hapa kujifunza mbinu mbalimbali za kuweza kumtenganisha mteja na fedha zake.

Hizi ni mbinu za mauzo magumu, kuna wakati unajikuta unatumia mbinu hizi ili ukamilishe mauzo kwa sababu unakuta hujauza na mteja yuko mbele yako na unaona kuna hela mbele yako, unakuwa humwachi, ni kama vile una njaa na unaona chakula mbele yako.
Hebu fikiria Simba akiwa na njaa, ataweza kucheza na kitoweo alichokiona mbele yake? Atafosi kwa kila namna kuhakikisha anapata kile anachopata.
Na wewe kuwa kama Simba, una njaa, familia inakutegemea na unategemewa kulipwa kulingana na mauzo ambayo yako mbele yako. Ukiwa na msukumo kama huu mbele yako, utajisukuma kuuza bila kujali mteja anakuambia nini zaidi ya wewe kuangalia ushindi ambao ni mteja kukupa wewe hela yake kupitia kile unachouza.

15. Ukamilishaji wa anayeambatana naye -2

Ukamilishaji huu unakuwa unamhusisha mteja kuambatana na mtu mwingine ambaye siyo mnunuaji lakini anakuwa anaonekana kukwamisha ukamilishaji  wakati hahusiki moja kwa moja.

Wewe tayari unakuwa umeonga na mteja lakini yeye anakuwa anamtoa kwenye reli.
Kwahiyo, unamuuliza swali kwa heshima ambalo litamfanya aache kuwa kikwazo kwako.

Kwa mfano, unataka nikokotoe bei nafuu kwa kutumia fedha zake mwenyewe au na wewe utahusika kwenye malipo?

Baada ya kumuuliza hivyo, kama hausiki kwenye malipo atakuachia nafasi ya kuongea na mteja wako.
Wapambe huwa wanakuwa ni wajuaji, hivyo basi, usipokuwa na njia za kuwakata makali wataweza kukuharibia mauzo yako.

16. Ukamilishaji wa kuchukua mara moja.

Ukamilishaji huu unakuwa unautumia pale mteja anakuwa mgumu kufanya maamuzi.
Kwa kumwambia mteja,
Kama hakuna mapingamizi au sababu za kushindwa kuendelea na bidhaa au huduma yako sasa hivi, kamilisha malipo au weka sahihi yako hapo ili tukamilishe hili.

Sisi kama wauzaji bora kuwahi kutokea, wajibu wetu namba moja, ni kumsaidia mteja kufanya maamuzi.
Kwahiyo, lazima umsukume mteja kufanya maamuzi.

Kama hana pingamizi lolote, basi akamilishe malipo ili apate bidhaa au huduma yake na aendelee kuifurahia au kuitumia.

Hatua ya kuchukua leo; hakikisha mteja yoyote ambaye umeshaongea naye mpaka mwisho UNAMKAMILISHA na siyo kukukimbia kwa kukupa sababu zao pendwa, hivyo tumia mbinu hizi kumkamilisha mteja wako ambaye yuko kwenye mchakato wa mauzo.

Kitu kimoja zaidi, ili fedha iweze kuingia kwenye mfuko wako lazima umshawishi mteja kukamilisha malipo ya kile unachomuuzia iwe ni bidhaa au huduma unayotoa.

Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,

Mwl.Deogratius Kessy

Mwalimu/Mwandishi/Mkufunzi wa mauzo.
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz